Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wapinzani walia siasa kuvuruga elimu, wataja vipaumbele bajeti ya elimu 2019/2020

57327 ELIMU+PIC

Tue, 14 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Aprili 29, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako aliwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake bungeni jijini Dodoma, akitaja kuwa Serikali imejielekeza katika maeneo nane ya vipaumbele.

Alivitaja vipaumbele hivyo kuwa ni kusimamia na kuendeleza elimu ya juu, vyuo vya ufundi, shule za sekondari na msingi.

Vipaumbele vingine ni dhamira ya kukuza ujuzi na ufundi, huduma za maji, elimu ya afya na mazingira pamoja na kuweka miundombinu ya teknolojia ya habari na mawasiliano. Kutekeleza hayo, Profesa Ndalichako aliomba Sh1.38 trilioni ili kutekeleza vipaumbele hivyo.

Wakati Serikali ikilenga katika maeneo hayo nane, kambi rasmi ya upinzani katika hotuba iliyosomwa na Waziri Kivuli wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Suzan Lyimo inasema elimu inayotolewa nchini haina ubora unaoridhisha hasa madaraja ya elimu ya msingi na sekondari.

Hotuba hiyo inataja maeneo kadhaa ya udhaifu ikiwamo utoaji wa maamuzi ya kisiasa bila kujali athari zake katika mfumo wa elimu. Kwa mfano, hotuba inasema kushushwa kwa viwango vya ufaulu na utoaji wa elimu bure ni matokeo ya maamuzi ya kisiasa ambayo hayakufanyiwa utafiti awali.

‘’…Wahitimu wa msingi na sekondari wanapikwa nusunusu hivyo kutokuwa na uwezo wa kuendelea na elimu ya juu na kushindwa kuingia kwenyue soko la ajira,’’ inasema sehemu ya hotuba.

Pia Soma

Maeneo mengine ya udhaifu ni kubadilishwa kwa mitalaa mara kwa mara bila kuwashirikisha walimu ambao ndio wadau wakubwa.

‘’Mitalaa haiangalii maarifa na pia haitoi ujuzi ili mwanafunzi aweze kuendeleza vipaji vyake. Mtalaa umekuwa zaidi wa kuwakaririsha wanafunzi,’’ inasema.

Hotuba ya upinzani inashangaa kuona baadhi ya miradi ya maendeleo ikitengewa bajeti ya fedha za wahisani ambazo ama huchelewa kutolewa au kutotolewa kabisa

Kambi Rasmi ya Upinzani imeshangazwa sana kwamba hata fedha za mradi wa mafunzo ya KKK (Kusoma, Kuandika, na Kuhesabu) na mradi wa kuimarisha ubora wa elimu ya sekondari au mradi wa kuendeleza elimu ya ualimu, tunategemea wafadhili watusaidie kwa asilimia mia moja,’’ inafafanua.

Udhaifu mwingine ni shule kutokuwa na washauri na wanasihi wanaoweza kuwashauri wanafunzi

kuchagua vyuo na kozi, kushuka kwa bajeti ya elimu kwa miaka mitatu mfululizo.

Kambi ya upinzani inasema kuna miradi ambayo imekuwa ikitengewa fedha za maendeleo, lakini fedha hizo zimekuwa hazipelekwi kabisa na kama zikipelekwa ni kwa kiasi kidogo.

‘’Mradi namba 6324 (Ukarabati wa Maktaba za Mikoa) mwaka 2017/18 mradi huu ulitengewa shilingi milioni 500; na mwaka 2018/19 ulitengewa shilingi bilioni 2.5. Kwa miaka yote miwili hakuna hata senti moja iliyopelekwa,’’ inasema hotuba.

Mapendekezo kambi ya upinzani

Moja, Serikali iongeze kasi ya kuajiri walimu maradufu ili waendane na wimbi kubwa la wanafunzi wanaojiunga na elimu ya awali na msingi. Serikali itengeneze mpango wa bajeti wa miaka mitano kwa ajili ya ajira za walimu ili kutatua kabisa tatizo la upungufu wa walimu

Mbili, kuwapo kwa haja ya kuweka mkakati maalumu wa kuongeza udahili wa wanafunzi wa kike katika vyuo vikuu kwa masomo ya sayansi ili:- mosi, kuwa na uwiano au usawa wa kijinsia katika fursa za ualimu wa masomo ya sayansi; lakini pili kuziba pengo la upungufu mkubwa wa walimu wa sayansi nchini

Tatu, Serikali ifikirie pia kujenga vyuo vya ualimu wa ufundi stadi ili kukabiliana na upungufu wa walimu katika vyuo hivyo na hivyo kuweza kuzalisha wahitimu wengi wa ufundi stadi wenye ujuzi ambao watahitajika sana kuendesha uchumi wa viwanda.

Nne, Serikali kutenga angalau Sh 20,000 kama ruzuku kwa kila mwanafunzi mmoja wa shule ya msingi na Sh 50,000 kwa mwanafunzi wa sekondari.

Tano, Serikali ianzishe fungu maalum kwa ajili ya kuweka fedha za mikopo ya elimu ya juu, ili fedha za miradi halisi ya maendeleo ziweze kuonekana na kufuatiliwa utekelezaji wake.

Sita, kutenga fedha za kujenga na kuimarisha miundombinu ya maji, elimu ya afya na usafi wa mazingira shuleni (SWASH) ili kusaidia jitihada za kupunguza utoro na kuboresha ufaulu wa mtoto wa kike.

Saba, Serikali iunde timu ya uchunguzi itakayofanya ukaguzi wa utendaji wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), ili kubaini uwezo wa watunzi wa vitabu, kwani imekuwa ni kawaida kuchapa vitabu vyenye makosa.

Nane, Serikali kupitia TET iwape mikataba watunzi binafsi kwa kipindi cha mpito ili waweze kuwaelekeza kazi watendaji waliopo sasa.

Wasemavyo wadau wa elimu

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI), Dk Jimson Sanga anakubaliana na hoja ya kuwekeza vilivyo katika utafiti, japo anapendekeza utafiti ufanyike kutokana na mahitaji ya sasa ya Taifa.

“Kwa wakati huu ambao dunia inalalamikia ukosefu wa ajira, utafiti mwingi ulenge kumuandaa mhitimu awe chanzo cha kuwaajiri walio chini yake au anaolingana nao kielimu, ”anasema Sanga na kuongeza kuwa ili sekta ya elimu iimarike, Serikali haina budi kuhuisha baraza la elimu.

“Baraza hilo liundwe na watu wenye weledi kama ambavyo sheria imeelekeza na mahitaji ya nchi. Baraza litamshauri waziri kuhusu vitabu, utafiti, ubora wa elimu na masuala ya mitalaa, ”anaeleza.

Mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Ubunifu Tanzania (EIT), Benjamini Nkonya anasema haoni haja ya kuongezwa kwa fedha za bajeti kama wanavyoshauri wapinzani. Kwa mtazamo wake, hakuna uhusiano kati ya ongezeko la bajeti na wanafunzi kufanya vizuri. Kilicho muhimu anasema ni kusimamia vizuri fedha zilizopo. “Kuna kipindi tulikuwa na bajeti asilimia 20 wakati tunajenga shule za kata, lakini ndiyo wakati ambao elimu ilishuka,’’ anasema.

Chanzo: mwananchi.co.tz