Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wapigakura Ngorongoro ruksa vitambulisho mbadala

Cd37829e96fa3b0f4306c03e3806cff8.jpeg Wapigakura Ngorongoro ruksa vitambulisho mbadala

Fri, 26 Nov 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetoa fursa kwa wapiga kura Jimbo la Ngorongoro mkoani Arusha, kutumia vitambulisho mbadala endapo kama wapo waliopoteza kadi ya mpiga kura au zimeharibika.

Vitambulisho hivyo mbadala ni leseni ya udereva, kitambulisho cha uraia kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) au hati ya kusafiria. Taarifa hiyo ilielezwa kwa wakazi wa Jimbo la Ngorongoro wakati wa utoaji wa elimu ya mpiga kura inayotolewa na maofisa wa NEC katika vitongoji vya Kata za Oldonyo Sambu na katika vitongoji vya Kata ya Olbalbal katika Tarafa ya Ngorongoro.

Elimu ya mpiga kura inatolewa kwa wakazi hao kwa njia ya ana kwa ana katika kaya, mikusanyiko kama mikutano ya koo, vitongoji, kata, maeneo zinapofanyika shughuli za kijamii kama biashara, malisho, majosho, vicoba ikiwa ni maandalizi ya Uchaguzi Mdogo wa Mbunge Jimbo la Ngorongoro utakaofanyika Desemba 11, mwaka huu.

NEC imeamua kuchukua uamuzi wa kuongeza wigo wa utoaji elimu ya mpiga kura kuhakikisha wapiga kura wanajitokeza kwa wingi kupiga kura na pia kupunguza idadi ya kura zinazoharibika. Elimu ya mpiga kura inamwezesha mpiga kura na wadau wengine wa uchaguzi kushiriki vyema katika michakato ya uchaguzi.

NEC imepewa mamlaka ya utoaji wa elimu ya mpiga kura kupitia kifungu cha 4C cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343. Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Ngorongoro unafanyika ili kujaza nafasi iliyoachwa wazi kutokana na kifo cha Mbunge William Ole Nasha ambaye pia alikuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji). Alifariki Septemba 27, mwaka huu jijini Dodoma.

Chanzo: www.habarileo.co.tz