Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wapigakura Buyungu, kata 77 kuamua nani ni nani leo

11456 Kura+pic TanzaniaWeb

Sun, 12 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wananchi wa Jimbo la Buyungu wilayani Kakonko, Mkoa wa Kigoma leo wanapiga kura kuchagua mbunge baada kifo cha aliyekuwa mbunge wao, Kasuku Bilago, Mei 26. Pia uchaguzi huo unakwenda sambamba na ule wa madiwani katika kata 77 za Tanzania Bara.

Uchaguzi huo mdogo ambao ni wa nne kufanyika nchini tangu Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani wa Oktoba 2015, ulitangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Julai 10 na vyama vya siasa vilivyosimamisha wagombea vilianza kampeni Julai 15 na mwisho ilikuwa jana.

Hata hivyo, uchaguzi huo unafanyika kukiwa na taarifa kwamba takriban kata 40 wagombea wake wamepita bila kupingwa, huku wengine wakienguliwa kutokana na sababu za kisheria.

Licha ya taarifa hizo, NEC bado haijatoa taarifa rasmi ya kuwapa wagombea hao ushindi.

Mbali na sababu za kurudia uchaguzi katika Jimbo la Buyungu, uchaguzi mdogo katika kata hizo ulitangazwa kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za baadhi yao madiwani kufariki dunia, lakini kubwa ni wale wa upinzani kuvihama vyama vyao na kujiunga na CCM.

Tofauti na kampeni za uchaguzi mdogo wa Februari 17, wa ubunge katika majimbo ya Kinondoni, Dar es Salaam na Siha mkoani Kilimanjaro, kampeni za Buyungu zimeshuhudiwa zikifanyika kwa usalama, amani na utulivu huku kukiwa hakuna malalamiko kama yale ya Kinondoni.

Uchaguzi wa Kinondoni ulighubikwa na malalamiko ya vyama vya upinzani kudai mawakala wao hawakutendewa haki na msimamizi wa uchaguzi.

Kampeni za udiwani

Wakati katika sehemu nyingi kampeni zilihitimishwa bila malalamiko makubwa, kampeni za udiwani wa Kata ya Turwa wilayani Tarime mkoani Mara, ziliingia dosari baada ya mkutano wa kumnadi mgombea udiwani wa Chadema kushindwa kufanyika.

Mkutano huo ulisambaratishwa na polisi siku nne kabla ya siku ya mwisho wa kampeni. Awali, ulitarajiwa kuhutubiwa na mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, lakini ulitawanywa kwa maelezo kwamba kulikuwa na zuio lililowekwa na msimamizi wa uchaguzi wa kata dhidi ya chama hicho.

Sekeseke hilo liliisha kwa polisi kuwatia mbaroni mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko na wananchi wengine zaidi ya 10 akiwamo mwandishi habari wa gazeti la Tanzania Daima, Sita Tuma. Zitto alitarajiwa kuhutubia mkutano huo kumnadi mgombea wa Chadema.

Baadaye, katibu wa Chadema Mkoa wa Mara, Chacha Heche alidai katika taarifa yake kuwa chama chake kimezuiwa kufanya mikutano ya kampeni kuanzia Agosti 8 hadi jana.

Hata hivyo, barua ya msimamizi msaidizi wa uchaguzi Kata ya Turwa, Peter Julius ilieleza kuzuia kampeni za upinzani kwenye kata hiyo kwa maelezo kuwa vyama hivyo vimekiuka kifungu cha 124A cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura ya 343, inayohusu maadili ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani ya mwaka 2015.

Sehemu zingine zinazofanya uchaguzi kampeni hazikuwa na joto kubwa la kisiasa.

Hata Buyungu ambako vyama vikubwa vya Chadema na CCM vilipeleka makada wake wazito hadi kampeni zinafikia ukingoni joto la kisiasa halikuwa kubwa.

CCM katika kampeni zake mbali na kuwatumia vigogo wa chama, iliwatumia baadhi ya makada wake wapya akiwamo aliyekuwa mbunge wa Ukonga kwa tiketi ya Chadema, Mwita Waitara aliyejiuzulu ubunge na kuhamia CCM hivi karibuni.

Waitara alikwenda Buyungu, Tarime na baadaye Ruangwa na Nachingwea mkoani Lindi kuwanadi wagombea udiwani.

Chama hicho pia kiliwatumia makada wake akina Nape Nnauye (mbunge wa Mtama); katibu mkuu wake mstaafu, Yusuph Makamba na Dk Cyril Chami aliyewahi kuwa mbunge wa Moshi Vijijini na waziri katika wizara mbalimbali.

Upinzani hawakuwa na vigogo wazito katika kampeni za Buyungu, lakini Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alimfanyia kampeni mgombea ubunge wa Chadema pamoja na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe alifanya kampeni za mgombea wao.

Baadaye Zitto alizunguka katika maeneo kadhaa ya uchaguzi nchini kufanya kampeni kwa wagombea wa upinzani hasa Ukawa.

Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu Chadema alifanya mikutano mbalimbali ya kampeni ikiwamo mkoani Tanga alikokwenda kumnadi mgombea udiwani wa chama chake. Wakati uchaguzi huu unafanyika leo, tayari NEC imetangaza kufanyika kwa uchaguzi mwingine Septemba 15, katika kata 21 na majimbo matatu ya Ukonga (Dar es Salaam), Korogwe Vijijini (Tanga) na Monduli (Arusha).

Chanzo: mwananchi.co.tz