Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wapigakura 191,152 kuchagua wabunge Ushetu, Konde

B3b578131c93a028ca7a057e83d5b156.png Wapigakura 191,152 kuchagua wabunge Ushetu, Konde

Fri, 8 Oct 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Takribani wapigakura 191,152 kesho wanatarajia kupiga kura za kuwachagua wabunge katika majimbo ya Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga na Konde kisiwani Pemba ambayo yanafanya Uchaguzi Mdogo huku vyama vitano vikisimamisha wagombea.

Pia kuna uchaguzi wa kujaza nafasi wazi za udiwani katika kata tatu ambazo ni Vumilia katika Halmashauri ya Wilaya ya Urambo, Neruma kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na Lyowa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imevipongeza vyama vya siasa vitano vilivyosimamisha wagombea.

Taarifa ya Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Semistocles Kaijage ilibainisha kuwa kampeni za wagombea zilianza Septemba 20 na kuhitimishwa jana. Alisema kampeni hizo zilifanyika kwa utulivu na kwa kuzingatia maadili ya uchaguzi.

“Tume inawapongeza wadau wa uchaguzi na wananchi kwa ujumla kwa kudumisha amani na utulivu. Bila shaka hali hiyo itaendelea kuwepo hadi shughuli za uchaguzi zitakapokamilika,” ilieleza taarifa hiyo.

Jaji Kaijage alisema wapigakura watatumia vituo 529 vya kupigia kura na kusisitiza wajibu wa vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi kuweka mawakala katika vituo vyota.

“Wajibu wa mawakala hao ni kulinda maslahi ya vyama vyao na wagombea na wakati wa utekelezaji wa majukumu yao vituoni, wanapaswa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi,” alieleza.

Jaji Kaijage alivikumbusha vyama vya siasa, wagombea, mawakala, wapiga kura na wananchi wote kwa ujumla kuzingatia kuwa hawatakiwi kufanya kampeni za aina yeyote baada ya muda unaotakiwa, kutumia alama za vyama vya siasa zinazoashiria kampeni kama ile vipeperushi, bendera, mavazi.

Pia watakaoruhusiwa kupigakura ni walio kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura wenye jimbo husika na mtaa husika na kwa waliopoteza vitambulisho vyao kutumia vitambulisho mbadala kama Kitambulisho cha Taifa, leseni ya udereva na pasipoti.

Chanzo: www.habarileo.co.tz