Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanawake wahimizwa kumweka madarakani Rais mwanamke 2025

2ec43491ea6c546af4fa7ea27756ac0c Wanawake wahimizwa kumweka madarakani Rais mwanamke 2025

Wed, 22 Sep 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MWENYEKITI wa Chama cha Wabunge Wanawake (TWPG), Shally Raymond, amewataka wanawake vijana kujitokeza kwa wingi kupiga kura utakapofi ka uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 ili waweze kufanikisha kumuweka madarakani rais mwanamke kwa njia ya demokrasia.

Pia amewataka wanawake vijana kushiriki kikamilifu katika kukomesha vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia hususani vinavyofanywa kwa wanawake.

Shally alitoa wito huo juzi wakati akifunga mafunzo yaliyowakutanisha wanawake vijana 30, yaliyoandaliwa na Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA) kwa kushirikiana na Kituo cha Usuluhishi (CRC), Young and Alive Initiative pamoja na Shirika la Mawasiliano Barani Afrika (FEMNET).

Mwenyekiti huyo wa TWPG, alisema maandalizi ya uchaguzi mkuu mwaka 2025 yanapaswa kuanza mapema hivyo wanawake lazima wajipange ili waweze kumweka rais mwanamke madarakani itakapofika muda huo.

“Mwaka 2025 wanawake tuna jambo letu hivyo tujipange na muda ukifika tujitokeze kwa wingi,” alisisitiza.

Mwenyekiti huyo ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), alisema ni vyema wanapotaka kuwa viongozi wakajitahidi kujifunza zaidi kwa waliowatangulia, kutoa ujuzi wa wenzao pale wao wanapokuwa wamefanikiwa kwa kuwaelekeza wenzao njia walizopita mpaka kufikia mafanikio.

Alisema mtu anapokuwa kiongozi hatakiwi kuwa mchoyo kwa kuwaelimisha wenzake kuhusu masuala ya uongozi.

Kuhusu ukatili na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia vilivyopo katika jamii, alisema kila mmoja ana jukumu la kuhakikisha vitendo hivyo vinakoma hususani kwa wanawake na watoto.

Alisema wao kama wanawake vijana wanaojiandaa kuwa viongozi wa kesho lazima wayajue masuala hayo na kushiriki kikamilifu kuyatokomeza.

“Pamoja na kuwajibika kwenye majukumu yenu ya kazi na familia hakikisheni mnashiriki katika kulinda haki zenu, pia msimamie na masuala hayo maana sifa ya mwanamke ni kutochoka licha ya kuwa na majukumu mengi,” alisema.

Akizungumza kuhusu ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Godfrey Sansa, alisema baadhi ya watu wanadhani ushiriki wa wanawake ni lazima uwe wa siasa, lakini ipo haja ya wanawake kuwa washiriki wa mabadiliko kuanzia ngazi ya jamii.

Alisema kwamba, haki ya mwanamke inaweza kulindwa endapo mwanamke atakuwa sehemu ya mchakato wa haki hizo. Naye Mwanasheria kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Fausta Mahenge, alisema bado mwamko wa wanawake kushiriki kugombea nafasi za uongozi uko chini.

Aliwataka wanawake kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali na kutekeleza masharti pindi wanapoteuliwa kugombea.

Pia aliwashauri wanawake kuanza kugombea nafasi ndogo ili wawe na uzoefu na kisha kugombea nafasi za juu.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki waliopata mafunzo hayo, Navina Mutabazi, alisema wanawake wanapopewa nafasi za uongozi sio huruma bali wanastahili kutokana na mazingira ya sasa.

Alisema ipo haja kuanzia sasa wanawake kuibeba na kutembea na ajenda ya mwanamke na jinsia ili kufikia ajenda ya taifa ya usawa wa jinsi

Chanzo: www.habarileo.co.tz