Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanasiasa wapongeza mchakato wa uchaguzi Kenya

766e0c74df00f9afb1b4e267a5d432fe Wanasiasa wapongeza mchakato wa uchaguzi Kenya

Wed, 17 Aug 2022 Chanzo: Habari Leo

Vyama vya siasa nchini vimepongeza mchakato wa uchaguzi nchini Kenya na kusema wanapaswa kujifunza kuungana na kushirikiana katika uchaguzi na kuweka maslahi binafsi pembeni ili kufanikiwa.

Aidha, vimesema Tanzania inasomo la kujifunza la uhuru na uwazi wa Tume ya Uchaguzi na mchakato mzima wa wagombea ulivyoendeshwa hadi kupata matokeo hayo ambayo yanapunguza malalamiko kwa wananchi kwani waliona mchakato jinsi ilivyoenda hadi mwisho.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) imemtangaza Mgombea wa Muungano wa Kenya Kwanza, Dk William Ruto (55) ni mshindi akiwashinda wagombea wengine watatu.

Wakizungumza na HabariLEO kwa nyakati tofauti jumatatu Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu alisema uchaguzi wa mwaka huu umeonesha Kenya imekua kidemokrasia na imejifunza kutokana na uchaguzi wao uliopita.

“Demokrasia imekua, Kenya inaonesha imejifunza kutokana na uchaguzi uliopita, vyama vya siasa vimeshirikiana sio chama kimoja ndio kilisimama kwenye uchaguzi ni mkusanyiko wa vyama vingi, hivyo vyama vya siasa vya Tanzania vinafunzwa kuweka maslahi binafsi pembeni na kuungana ili kushinda,” alisema Shaibu.

Alisema mapinduzi ya mfumo wa usimamizi wa uchaguzi Kenya kwa mwaka huu umetoa somo kwa Tanzania kujifunza jinsi ya kuendesha chaguzi zake kwa uwazi zaidi na kusema imani yao ni kuwa baadhi ya viongozi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), walioshiriki uangalizi wa uchaguzi Kenya kama timu ya kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), watakuwa wamejifunza uwazi wa uchaguzi.

“Nimefuatilia na kufanya ulinganishi wa uchaguzi wa Kenya ulioisha sasa na ule uliopita, tumeona demokrasia imeimarika, huu wa sasa uwazi ulitawala, vurugu au ghasia hazikuwepo, ukiacha taarifa za Azimio kutokubali matokeo, uwazi ulitawala,” alisema Shaibu.

Alisema ingawa wajumbe wanne wa IEBC kutokubaliana na maamuzi ya tume hiyo, hiyo imeonesha uhuru mkubwa wa mawazo na maoni na hilo ni jambo la kujifunza kwa Tanzania na kusema bahati nzuri hatua zimeshaanza kuchukuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

“Wajumbe wanne wa tume ya uchaguzi Kenya hawakukubaliana na matokeo ya tume, huo ni uhuru wao ambao nasi tunapaswa tujifunze, lakini bahati nzuri tumeanza michakato ya kuboresha tume yetu ya uchaguzi,” alisema Shaibu.

Aliongeza: “Rais Samia ameunda kikosi kazi na kusema kama kuna changamoto zirekebishwe, imani yetu tutafanikiwa hilo.”

Alisema ACT-Wazalendo inawashauri Wakenya watangulize maslahi mapana ya taifa lao na sio vyama vyao ili kuepuka machafuko na vurugu ambazo hazina msingi kwa Wakenya.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mrema akizungumzia mchakato wa uchaguzi nchini Kenya, alisema umetoa mafunzo mengi kwa Tanzania kuanzia mchakato wa kuchukua fomu hadi kuzirejesha.

“Tumeshuhudia wagombea wa vyama mbalimbali wakichukua na kurejesha fomu za uteuzi bila kusikia kuna wagombea wamenyimwa fomu, kunyang’anywa na ama wasimamizi kukataa kupokea fomu au kusikia fomu zimepotea,” alisema Mrema.

Alisema wagombea wote walinadi sera zao bila kuingiliwa na mamlaka mbalimbali au mikutano yao kuvurugwa huku vyombo vya habari vikitimiza wajibu wao kwa kuhabarisha umma kwa usawa.

Alisema Tanzania ina cha kujifunza kuwa na Katiba bora itakayounda tume huru ya uchaguzi, taasisi imara na ambazo haziingiliwi na dola na kuwa wazi kuanzia mchakato wa fomu hadi kuhesabu kura.

Aidha, alisema matumizi ya teknolojia katika kutangaza matokeo yamesaidia kupunguza malalamiko ya wananchi kwani matokeo yalijumlishwa kwa uhuru na hivyo kutoa haki kwa wagombea.

“Tanzania inatakiwa ichukue yale yote mazuri na kuyaboresha zaidi ili tuweze kuwa na chaguzi bora zaidi, huru na za haki kwa maslahi mapana ya nchi yetu,” alisema Mrema.

Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Chama cha NCCR-Mageuzi, Joseph Selasini alisema wanapongeza kwa hatua iliyofikiwa na Wakenya kwa kuendesha uchaguzi kwa uhuru na amani.

“Tunapongeza hatua iliyofikiwa na wenzetu kuendesha uchaguzi wa uhuru na amani, ukilinganisha na uchaguzi wa mwaka 2007 ulioleta vurugu, mwaka huu umeenda kwa amani tumeshuhudia uwazi wa hali ya juu,” alisema Selasini.

Alisema uchaguzi huu wameshuhudia hakukuwepo na mwingiliano wa vyombo vya dola bali vilisaidia kufanya ufanyike kwa amani na huku wagombea wakijinadi kwa uhuru na kuungwa mkono na wananchi.

“Tanzania tuna cha kujifunza, kwanza Katiba yetu na tume ya uchaguzi virekebishwe, Rais Samia ameanza kwa kuunda kikosi kazi, hivi ni vilio vya wananchi wengi na ndio hitaji lao, vikitekelezeka chaguzi zetu zijazo zitakuwa huru zaidi na haki itatendeka,” alisema Selasini.

Chanzo: Habari Leo