Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanasheria wakoleza ishu ya Chipukizi CCM

Siasaa Ccmmmmm.jpeg Wanasheria wakoleza ishu ya Chipukizi CCM

Sat, 23 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baadhi ya wanasheria wamekoleza majadala wa watoto kugombea nafasi za kisiasa wakisema si sahihi, badala yake waachwe wasome hadi watakapofikisha umri wa miaka 18 kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa.

Hatua hiyo imekuja kutokana na mkutano mkuu wa tisa wa chipukizi Taifa wa CCM uliofanyika Desemba 20 ambapo pamoja na mambo mengine ulifanya uchaguzi na Qayllah Bilal, mtoto wa msanii wa muziki wa kizazi kipya, Nurdin Bilal ‘Shetta’ kuchaguliwa kuwa mwenyekiti, huku nafasi ya makamu mwenyekiti akichukuliwa na Atka Hassan Juma.

Katika uchaguzi huo, nafasi za wajumbe wa kuwakilishi mikutano ya UVCCM zilichukuliwa na Isack Nchemba (Mjumbe wa Baraza kuu la UVCCM- Bara), Aiman Mohammed Baraza kuu la UVCCM-Zanzibar.

Uwakilishi wa nafasi ya ujumbe wa kamati ya uendeshaji Taifa kundi la wanawake alishinda Briana Mahiga, wakati kundi la wanaume akichukua Simba Jerry Silaa.

Baada ya uchaguzi huo, kuliibua mjadala katika mitandao ya kijamii, wapo waliopongeza, huku wengine wakipinga wakisema ni hatua hiyo kutengeneza makundi ndani ya jamii, si vema watoto wakaingizwa kwenye siasa mapema.

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi leo Desemba 22, Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Anamringi Macha amesema kilichofanyika ni malezi ya kuwajengea ujasiri, akisema kama mtu anadhani kuna mahali kuna shida apeleke mawazo yake.

 “Ni kama kufikirishana kwamba jambo hili lipo, mtoto hawezi kwenda shule kabla ya kufikia umri sahihi, lakini anaweza kuanzia shule ya awali, hivyo hili jambo ni makuzi, afadhali uwakuze katika misingi hii kuliko kubaki mitaani kufanya mambo yaliyo kinyume na maadili.

“Hakuna kingine wanachokifanya bali ni kuwajengea ujasiri wa kuzungumza mbele za watu, unajua kuna mtoto wa darasa saba au kidato cha kwanza ukipeleka mbele za watu hawezi kuongea?” amehoji.

Macha amesema uchaguzi huo wa chipukuzi sio wa kwanza, bali ni baada ya kupita kwa miaka mitano na kwamba hana shida maoni ya watu kwa sababu wana haki ya kuzungumza, lakini wasiseme kama jambo hilo ni la kwanza kutokea.

Macha amesisitiza kama mtu ana maoni, apeleke mawazo yakem si kusema watoto hawajafikisha miaka 18 akitolea mfano kuwa huko mtaani kuna watoto wanafanya mambo ya ajabu chini ya umri wao, hivyo CCM kuwachukua na kuwalea misingi hiyo hakuna ubaya.

Wanasheria

Akizungumza na Mwananchi leo, Desemba 22, 2023 wakili Aloyce Komba amesema sheria ya vyama vya siasa inaeleza ili uwe mwanachama wa chama cha siasa, lazima uwe na miaka 18, lakini CCM inafanya mambo ambayo aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, miaka iliyopita hakufurahishwa nayo.

“Nimejiuliza hawa chipukuzi wanaoshirikishwa wanakuwa wanachama au? Ushauri wangu CCM waachane na mambo ya kushirikisha vijana kwenye siasa, bali waachwe wafundishwe darasani.

“Tusiwaingize kwenye uitikadi kwa sababu ni mbaya kutokana ngazi ya umri wao, katika mpira wa miguu hakuna ubaya, lakini kwenye siasa hapana,” amesema Komba.

Naye, Wakili Philpo Mwakilima amesema kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa iliyofanyiwa mabadiliko mwaka 2019, kilichofanywa na CCM si sahihi.

“Kimsingi kwa sheria hii ya vyama vya siasa, ilifuta shughuli na masuala ya chipukizi, kama wanafanya au kuendeleza wanakiuka utaratibu kwa sababu hawakupaswa kufanya,” amesema Mwakilima.

Hata hivyo, Wakili Frank Chundu amekuwa na maoni tofauti akisema ingawa sheria imemtaka ili mtu awe mwanachama lazima afikishe miaka 18, ila ndani vyama vya siasa kuna watoto hao wamesajiliwa kama wanajumuiya wa chipukizi, jambo ambalo si kosa.

“Mfano katika Kanisa Katoliki kuna Uwaka (Umoja wa Wanaume Kanisa Katoliki) na Uwawata (Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania) wanakuwa na jumuiya zao za watoto wakiishi maisha ya kikanisa.

“Kwa hiyo kwenye vyama vya siasa wanalea hawa ili kuishi wakikua wajue katika siasa kuko hivi na hivi, lakini kimsingi sheria ya vyama vya siasa inakataza mtu kuwa mwanachama wa chama cha siasa chini ya miaka 18, sasa kama watoto wana kadi ni kosa,” amesema Chundu.

Kauli ya hayati Magufuli

Wakati mjadala huo ukiendelea, video ya aliyekuwa Rais wa awamu ya Tano, hayati John Magufuli aliyeshauri kuondolewa kwa chipukizi katika mfumo wa CCM Julai 23, 2016 alipokuwa akikabidhiwa uenyekiti wa CCM kutoka kwa mtangulizi wake, Jakaya Kikwete.

“Hivi katika zama hizi tunahitaji mtoto wa miaka minane hadi 15 kuwa chipukizi kwa ajili ya kumtumia katika siasa badala kumuacha asome?

“Kama kutakuwepo chipukuzi wa CCM, ikianzishwa chipukuzi wa Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi –wakati huo)? Je wakianzishwa chipukizi wa TLP, NCCR-Mageuzi na UDP je hawa watoto watasoma? Najaribu kutoa tu changamoto, sijatoa uamuzi kwa sababu upo kwenu,” alisema.

Jana, Madaraka Nyeyere, mtoto wa Rais wa kwanza wa Tanzania, hayati Julius Nyerere alikosoa suala la watoto kufanyiwa uchaguzi na kushauri waachwe hadi watakapofikisha umri wa kupiga kura ndipo wahusishwe na siasa.

Chadema washtuka

Akizungumza na Mwananchi jana, Desemba 21, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alielekeza Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), lililopewa jukumu la kuwa walezi wa watoto kiungozi na kutengeneza mfumo kama huo ambao wao waliuita Chemchem ya kukuza uongozi wa vijana wafuasi sio wanachama wenye umri kati ya miaka 12 hadi 17.

“Bavicha lirejee kuanza mchakato wa kuruhusu chemchem, ili tuwe na kitawi cha uongozi,” alisema Mnyika.

Alisema awali mfumo huo ulikuwepo, lakini kutokana na mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2019, waliuondoa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live