Pazia la uchukuaji na urejeshaji fomu za kusaka uongozi katika kanda nne za kiuongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), linafunguliwa rasmi leo Ijumaa Aprili 12 hadi 22, saa 10 alasiri.
Nafasi zinazowaniwa ni mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa kanda, mweka hazina na katibu wa kanda. Kanda hizo ni Victoria, Magharibi, Nyasa na Serengeti zinazounda mikoa ya Mwanza, Kagera, Simiyu, Shinyanga, Mbeya, Iringa, Njombe, Mara, Rukwa, Katavi, Tabora, Songwe na Kigoma.
Kwa mujibu wa tangazo la uchaguzi lililotolewa leo na Naibu Katibu Mkuu (Bara), Benson Kigaila limeeleza kuwa fomu za kuwania nafasi hizo zitapatikana kwa makatibu wa mikoa na tovuti ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini.
Tangazo hilo limefafanua kuwa gharama za fomu hizo ni Sh100,000 huku likisema nafasi nyingine zinazogombaniwa ni mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Chadema (Bazecha) wa kanda, makamu mwenyekiti, katibu na mweka hazina wa baraza hilo.
Nafasi nyingine ni mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), makamu mwenyekiti, katibu na mweka hazina wa baraza hilo. Katika ngazi ya Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) ni mwenyekiti wa kanda, makamu mwenyekiti, katibu na mweka hazina.
Uchaguzi wa uongozi wa kanda unatarajiwa kufanyika mwezi ujao na kanda nne kati ya 10 zimekamilisha mchakato wa kusimika uongozi kuanzia ngazi ya chini hadi mkoa. Kufunguliwa kwa pazia hilo kunatoa fursa kwa watia nia mbalimbali kuchukua fomu hizo za kusaka uongozi.
Miongoni wa vigogo wanaotajwa kuchukua fomu ni pamoja na aliyekuwa mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi 'Sugu' atakayechuana na Mchungaji Peter Msigwa anayetetea uenyekiti wa kanda ya Nyasa. Wengine ni mwenyekiti wa Bavicha, John Pambalu atakayekabiliana na Ezekiah Wenje katika Kanda ya Victoria.
Mchuano mwingine utakuwa katika kanda ya Magharibi utakaowakutanisha mawakili Dickson Matata na Peter Madeleka, wakati kanda ya Magharibi wanaotajwa kuutaka ubosi ni Emmanuel Ntobi, John Heche, Gimbi Masaba na Lucas Ngoto.