Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wananchi wanavyowajibisha viongozi kupitia mitandao ya jamii

90268 Ananchi+pic Wananchi wanavyowajibisha viongozi kupitia mitandao ya jamii

Mon, 30 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Utawala ni matumizi ya mamlaka ya kisiasa, kiuchumi au kijamii katika kusimamia masuala ya nchi kwenye ngazi zote. Lakini utawala bora ni matumizi ya mamlaka ambayo yanakuwa na uwazi, uwajibikaji, ushirikishaji wa watu, ufanisi, tija, uadilifu usawa na unafuata utawala wa sheria.

Utawala bora unahusisha matumizi sahihi ya dola, matumizi mazuri ya rasilimali kwa faida ya wananchi, matumizi mazuri ya madaraka na kuhakikisha kuwa yanatumika kulingana na mipaka iliyowekwa na Katiba na sheria.

Katiba ya Tanzania ibara ya 8(1a) inaitambulisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii, na kwa hiyo wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi.

Kwa mujibu wa ibara hiyo, kazi ya Serikali ni kuhakikisha ustawi wa wananchi. Na hii ndiyo maana shirika la Oxfam limekuwa linatoa mafunzo ya utetezi kwa wanavijiji ili kuongeza uwajibikaji.

Mfano, ni mafunzo yalitolewa wilayani Kibondo, Kigoma ambapo katika mafunzo hayo, wananchi wamepewa uelewa wa matumizi ya mitandao ya jamii katika kueleza kero zao ili mamlaka za Serikali zizishughulikie.

Miongoni mwa waliopata mafunzo ni Jesca Sogomba kutoka Kijiji cha Bitulana, ambaye anasema mafunzo hayo yameiamsha jamii na imeanza kudai uwajibikaji kwa viongozi waliowachagua.

“Awali tulikuwa hatujawahi kusomewa mapato na matumizi wala mikutano hadhara ya kijiji ilikuwa haifanyiki. Lakini baada ya mafunzo tulijikusanya na kuwajulisha viongozi wa vijiji na kudai mikutano.

“Tangia hapo mikutano mpaka ya vitongoji inafanyika. Wananchi wakapata fursa ya kuhoji mapato na matumizi,” anasema Jesca.

Anataja pia ujenzi wa miundombinu kuwa kijiji chao hakikuwa na barabara inayokiunganisha na vijiji vingine.

“Hatukuwa na barabara inayotuunganisha na kijiji cha Mengo, hivyo watu walipita vichochoroni. Tulichukua picha za kero hiyo na kuzituma kwenye mitandao ya jamii. Baada ya picha kusambaa, ile barabara ikatengenezwa, japo bado daraja halijakamilika,” anasema.

Anasema pia wamejifunza kushiriki uchaguzi na kuwabaini viongozi bora.

Ushuhuda kama huo unatolewa na Brighton Kahiri kutoka kijiji cha Mengo akisema alihamasika kuingia kwenye mpango wa utetezi baada ya kuona viongozi wa kijiji wanatumia vibaya madaraka yao.

“Mfano ni kiwanda kilichopo hapa kijijini cha kuchakata mihogo kilichelewa kupata umeme licha ya mwenye kiwanda kuomba sana Tanesco.

“Baada ya kuingia kwenye kazi hii nilikipiga picha na kuiweka mtandao wa Twitter. Baada ya viongozi wa Tanesco kuiona walinipigia simu, nikawapa maelekezo ya kilichotokea. Yule meneja wa Tanesco wilaya aliandikiwa barua akiambiwa kama hawezi kupeleka umeme aandike barua ya kuacha kazi,” anasema Kahiri.

Anaendelea, “Kazi nyingine niliyofanya ni ya mtendaji kata aliyekuwa akinyanyasa wananchi, kila mwananchi aliyeomba barua ya udhamini lazima aombwe hela. Yule mtendaji sasa amesimamishwa kazi.”

Mtetezi mwingine ni Loyce Jumanne kutoka kijiji cha Kigendeka ambaye ni katibu wa watetezi mkoa wa Kigoma anasema amefanikiwa kuhoji maendeleo ya vijiji baada ya kuhamasishwa na mafunzo hayo.

“Awali kulikuwa na mnara (wa simu) uliojengwa kijijini kwetu, ulikuwa umemilikishwa kwa mtu binafsi wakati ni mali ya umma. Nilipoingia kwenye uraghibishi nilifuatilia suala hilo, nikiwashirikisha diwani na mtendaji wa kijiji. Tulikaa vikao na kujadili mpaka suala likafikishwa mahakamani na tukashinda kesi. Kwa sasa mapato yanaingia kwenye mfuko wa kijiji,” anasema.

Mtetezi mwingine, Jonas Ngarama kutoka kijiji cha Mengo, anasema awali alikuwa mwenyekiti wa kamati ya shule ya Msingi Kanyiha, nafasi iliyomwezesha kujua kero kwenye shule yao.

“...Shule kwa mfano, ilikuwa imeezekwa kwa nyasi na imejengwa kwa matofali ya udogo. Tulikaa kikao na kuonana na mbunge, akatwambia tuandike barua tuipeleke ofisi yake jimboni.

“Niliwaambia walimu waandike barua lakini hawakuandika. Nami nilifuatilia bila mafanikio. Mwishowe tukalifuata shirika la Save the Children wakaja kutusaidia na kujenga baadhi ya majengo.

Chanzo: mwananchi.co.tz