Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanachama wa Chadema watawanywa kwa mabomu ya machozi gereza la Segerea

98938 Pic+mabomu Wanachama wa Chadema watawanywa kwa mabomu ya machozi gereza la Segerea

Fri, 13 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Askari Magereza katika gereza la Segerea jijini Dar es Salaam wametumia mabomu ya machozi kuwatawanya wanachama wa Chadema waliokwenda kwenye gereza hilo kumtoa mwenyekiti wao, Freeman Mbowe.

Tukio hilo limetokea leo Ijumaa Machi 13, 2020  jijini Dar es Salaam  saa 7:30 mchana wakati wanachama na viongozi wa Chadema walipokwenda kumchukua Mbowe baada ya kukamilisha malipo ya faini ya Sh70 milioni.

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee aliwasili gerezani hapo akiwa na wanachama wengine na kuzuiwa na askari kuingia gerezani, jambo ambalo lilisababisha yeye na wenzake kushuka kwenye gari ili kuzungumza na askari hao.

Mwananchi lilishuhudia mazungumzo hayo lakini baada ya muda askari hao walianza kuwavuta huku wakiwataka kuondoka eneo hilo.

Askari hao waliwapiga na kuwakamata baadhi ya wanachama wa Chadema waliojaribu kusogea ili kukabiliana nao.

Hali hiyo ilizua taharuki na askari hao kuanza kufyatua mabomu ya machozi na kusababisha watu kukimbia ovyo.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement

Wanafunzi wa shule ya sekondari Magozani iliyopo jirani na gereza hilo waliokuwa wakitoka shule walikuwa miongoni mwa waliotimua mbio huku baadhi wakianguka na kunyanyuana kisha kuanza tena kutimua mbio.

Baadhi ya makada wa Chadema waliokuwepo eneo la tukio wamesema wataendelea kupigania haki ya mwenyekiti wao ambaye tayari ametimiza masharti yote.

"Mpaka sasa tumelipa faini ambazo zilitakiwa kulipwa lakini bado hawataki kumwachia huru mwenyekiti. Tunashindwa  kufahamu lengo lao hasa ni lipi," amesema kada wa Chadema, Said Hamza.

Chanzo: mwananchi.co.tz