Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

WanaCCM Mbeya waonywa kuhusu majungu kwa Spika

CCM Mbeya.jpeg WanaCCM Mbeya waonywa kuhusu majungu kwa Spika

Sun, 25 Dec 2022 Chanzo: Mwananchi

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema mkoa wa Mbeya unachelewa kupiga hatua kimaendeleo kutokana na kuwepo kwa makundi na majungu dhidi ya Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson.

Mhandisi Mahundi amesema hayo Jumamosi Desemba 24, 2022 kwenye mkutano maalum wa mwaka uliotishwa na Dk Tulia kutoa taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi kwa mwaka 2021/22 kwa wajumbe wa CCM wilaya ya Mbeya Mjini ikiwepo elimu, afya, maji na barabara.

Amesema Spika huyo licha ya kuwatumia wananchi katika jimbo lake, anakatishwa tamaa na maneno maneno yanayosemwa ambayo yanaleta majeraha ndani ya moyo wake.

“Sisi viongozi tuna mioyo yenye nyama sasa maneno maneno yamekuwa yakitukatisha kwani tunapojitoa kwa ajili ya wananchi wengine wanaibuka na ya kwao, tufike wakati tubadilike ili mkoa uweze kupiga hatua kama mikoa mingine,” amesema.

Amesema ufike wakati wanaCCM kufanya kazi kwa pamoja kwa kushirikiana na viongozi ndani ya chama na kuachana na maneno ili kufanikisha kufikia malengo kwa Mkoa wa Mbeya hususan Jiji la Mbeya kufanya vizuri kwenye miradi ya Maendeleo

“Naomba tunapoaga mwaka 2022 kuingia mwaka 2023 tufungue ukurasa mpya wa kumtunza Spika ili tuweze kupiga hatua na kuepuka maneno ya kumuumiza ambayo hayana tija kwa mustakabali wa nchi na wanaMbeya,” amesema.

Kwa upande wake, Dk Tulia amewataka na kukemea tabia za majungu na badala yake wanaojihusisha wajikite katika kujenga taifa na kama wanaumizwa na utendaji wake wasubiri uchaguzi mkuu 2025.

Amesema kumekuwa na tabia ya baadhi ya watu wasiopenda maendeleo wanapoona viongozi wakiwemo wakitaifa wakifanya kazi nzuri kwa jamii, wao wanapambana kutengeneza majungu na kukosoa utendaji ili kuleta mkanganyiko usio na faida kwa jamii.

Amewataka wananchi kuendelea kumuunga mkono ili aweze kuwatimizia mahitaji yao ikiwemo uboreshaji wa miundombinu, elimu, afya n.k kwa kushirikiana na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa CCM, wilaya, Humphrey Msomba amekemea tabia ya majungu na fitna dhidi ya Spika na kwamba kama chama kiko nyuma yake na hakiko tayari kusimamisha mtu mwingine kugombea nafasi ya ubunge katika uchaguzi mkuu 2025.

“Kama chama hatotoweza kuvumilia na kuwatunza watu ambao wamekuwa kigeugeu kwa kumsema vibaya Mbunge ambaye ameleta mabadiliko katika Chama ikiwepo ukarabati wa majengo na Ukumbi wa Mikutano kwa gharama ya zaidi ya 80 Milioni”amesema.

Mjumbe wa CCM kata ya Mabatini, Tumaini Joram amesema hawako tayari kumpoteza mbunge wa Mbeya mjini kwa kusikiliza maneno ya watu wenye chuki binafsi ambao walishindwa kukitetea chama.

Chanzo: Mwananchi