Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wana CCM waanza kuchukua fomu kumrithi Nassari

49848 Pic+ccm

Mon, 1 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Wanachama watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamechukua fomu kuomba ridhaa ya chama hicho kupeperusha bendera katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki.

Uchaguzi huo unafanyika Mei 19, 2019 baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kuiandikia Tume ya Uchaguzi (NEC) kuwa jimbo hilo lipo wazi baada ya aliyekua mbunge wake, Joshua Nassari kukosa sifa.

Katibu wa CCM wilaya ya Meru, Kanuti Benedict akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Aprili Mosi, 2019 amesema wanachama watatu hadi saa 6:14 mchana walikua wamechukua fomu kuwania ubunge wa jimbo hilo.

Amewataja wanachama hao ni Rehema Peter Mrosso, Julius Wilfred Mungure aliyewahi kuwa mjumbe wa halmashauri Kuu (Mnec-Meru) na Dk John Pallangyo ambaye ni mwenyekiti wa wazazi mkoa wa Arusha.

"Niwaombe wanachama wengi zaidi kujitokeza kuchukua fomu huu ndio utaratibu wa kidemokrasia tulionao kwenye chama chetu ili tumpate mwanachama bora atakayewakilisha vizuri kwenye kinyang'anyiro kilichopo mbele yetu," amesema  Benedict.

Awali, Katibu Mwenezi wa CCM wilaya ya Meru, Joshua Mbwana alisema idadi ya wanaokusudia kuomba ridhaa ya chama inaweza kuwa kubwa kutokana na utendaji kazi wa Rais John Magufuli wa kuwahudumia wananchi.

"Utendaji kazi wa Rais Dk John Magufuli unamfanya kila mwana CCM kutamani kuwa mbunge kwa sababu ahadi atakazotoa ana uhakika zitatekelezeka," amesema Mbwana.

Mei 14, 2019, Spika wa Bunge, Job Ndugai alimuandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC) Jaji Semistocles Kaijage kumtaarifu kuwa Jimbo la Arumeru Mashariki lipo wazi kutokana na mbunge wake kutohudhuria vikao vya mikutano mitatu mfululizo bila taarifa.

Mikutano hiyo ni ule wa 12 wa Septemba 4 hadi 14 mwaka 2018, mkutano wa 13 wa Novemba 6 hadi 16 mwaka 2018 na mkutano wa 14 wa 29 Januari hadi Februari 9 mwaka 2019.

 

 



Chanzo: mwananchi.co.tz