Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wamuenzi Nyerere kwa kujenga ofisi ya chama

Ofisi Za CMM Wamuenzi Nyerere kwa kujenga ofisi ya chama

Thu, 13 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Bagamoyo,Alhaj Abdul Sharifu ameeleza wakati Taifa likikumbuka miaka 23 ya Baba wa Taifa, muasisi Mwalimu Julius Nyerere, viongozi wa CCM wilayani humo wamuenzi kwa kukijenga chama kwa kuwa na ofisi za chama kuanzia ngazi ya matawi na kata.

Akizungumza na viongozi na wanachama wa CCM huko Talawanda, Sharif alisema katika suala la uongozi, maadili ya uongozi ni jambo ambalo Mwalimu Nyerere aliloliweka mbele, miongoni mwao ni viongozi ambao wanaweza kukidhi matarajio ya watanzania na wanaCCM.

Alieleza, jukumu la wanaCCM ni kuimarisha na kukijenga Chama ili kukiondoa kwenye utegemezi kwa kuongeza ofisi zao na Kuwa na vitega uchumi.

"Namnukuu Watanzania wanataka mabadiliko, wasipoyapata ndani ya CCM, watayapata nje ya CCM,"

Sharif alikitaka chama hicho kuendelea kusimamia Serikali na miradi mbalimbali ya kimaendeleo inayoanzishwa kwenye Maeneo Yao kwa maslahi ya wananchi.

Katika hatua nyingine alitaka viongozi kuanzia matawi ,kata na wilaya kuguswa na falsafa ya kukijenga chama na kukiondoa kwenye utegemezi kwa kuhakikisha wanaandaa mpango kazi kuhakikisha wanajenga ofisi za Chama ili kuondokana na utegemezi wa kukodi.

Sharif alieleza, alishaanza utekelezaji huo kipindi kilichopita ambapo kati ya maeneo aliyohakikisha yanajengwa ni pamoja na kujenga ofisi ya chama eneo la Mandela ofisi ambayo ipo katika hatua ya umaliziaji.

Alieleza , atashirikiana na kamati ya siasa wilaya kuhakikisha wanatekeleza ahadi walizozitoa kwa wanaCCM.

"Naahidi kila kilicho ndani ya uwezo wangu binafsi nitakitekeleza, pia pamoja na viongozi wenzangu tutaendelea kusimamia malengo hayo, ili chama kiendelee kuheshimika," alisema Sharifu.

Vilevile, Sharif alieleza Mwalimu Nyerere alisimamia umoja na mshikamano pia hivyo alieleza wakati wakimuenzi na kumkumbuka wote wadumishe umoja, upendo na mshikamano ili kuimarisha chama wilaya ,kata hadi matawi na shina.

Nae Katibu Mwenezi CCM Wilaya ya Bagamoyo, Ramadhani Lukanga, aliyechaguliwa hivi karibuni, alisema kuwa ujenzi wa Ofisi za chama kila kata ni wa lazima.

Alisema hawatowaonea haya watu wachache watakaodhohofisha juhudi za chama, chini ya Mwenyekiti wa Taifa Samia Suluhu Hassan.

"WanaCCM wenzangu kwanza niwashukuru kwa kumchagua Sharifu kuendelea kuongoza chama chetu, nami kuona nafaa kukisaidia chama, nawashukuru sana," alisema Lukanga.

Pamoja na hayo, Lukanga alisema atatembelea kata zote lengo kuhamasisha ujenzi huo, na kwa kuunga kupitia umoja wao itawezekana.

Diwani wa Kata ya Talawanda Ramadhani Biga alimpongeza Sharifu pamoja na Kamati ya siasa wilaya, kwa kuanza ujenzi wa Ofisi kata.

Malota diwani wa Kiwangwa nae aliahidi ushirikiano kwa viongozi hao, huku akisema wanaCCCM kata wataendelea kuwaunga mkono ili malengo yaweze kufikiwa.

Ujenzi wa Ofisi za chama hicho Talawanda na Mwetemo gharama zote za fundi zinalipwa na Mwenyekiti AbdulSharif.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live