Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wamerudi kwa wananchi

77578 Pic+wamerudi

Sat, 28 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kuna wimbi la viongozi kuwaangukia wananchi. Bila shaka ni wajibu wao, lakini kasi yao inaonekana kutofautiana na hali ilivyokuwa miaka michache iliyopita na wachambuzi wanahusisha na uchaguzi.

Mawaziri sasa wanazunguka mikoani wakiwa katika makundi kuzungumza na wafanyabiashara, wawekezaji na wananchi na kusikiliza shida zao na kuwapa majibu au kujadili njia za kutatua.

Na si hilo tu, siku nne zilizopita, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitangaza uamuzi wa Baraza la Mawaziri wa kufuta mapori 12 tengefu ili ardhi yake igawiwe kwa wananchi kwa ajili ya makazi na kilimo.

Mwezi uliopita, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola akiwa ziarani mkoani Kilimanjaro, aliagiza waendesha bodaboda na pikipiki za magurudumu matatu, maarufu kwa jina la Bajaji kote nchini kutobughudhiwa na polisi.

Kama vile kuna wimbi la viongozi na watendaji wa Serikali kujishusha kwa wananchi kutokana na kauli na matendo yao, hivi ndivyo unavyoweza kutafsiri kile kinachoendelea.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi wakiwamo viongozi wa dini wamechukulia hali hiyo kwa tahadhari wakihofia huenda ni mbinu za kisiasa za kupata ushindi serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu 2020.

Pia Soma

Advertisement
Aliyekuwa askofu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Martin Shao alisema ni vizuri wameanza kujishusha, lakini akataka wajishushe nyakati zote.

Baadhi ya viongozi wa kisiasa walitaka moyo huohuo wa kujishusha, uende mbali zaidi kwa viongozi kujitokeza hadharani kukemea maovu yaliyozalisha chuki nchini ikiwamo utekaji na utesaji.

Tofauti na mawaziri ambao kwa siku za karibuni wanaonekana kusogea zaidi kwa wananchi, viongozi watatu wa juu; Rais John Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wao wamekuwa wakifanya hivyo tangu walipoingia madarakani.

Mathalani, Rais amekuwa akisisitiza wajasiriamali wenye mtaji wa chini ya Sh4 milioni wasitozwe kodi yoyote huku akitaka wakulima wanaosafirisha mazao yasiyozidi tani moja wasitozwe ushuru.

Mbali na hilo lakini ni wiki iliyopita tu Rais aliwakoromea watendaji wa Serikali mkoani Dar es Salaam, akiwamo mkuu wa mkoa, Paul Makonda kwa kutosimamia miradi ya maendeleo.

Rais alifanya ziara ya kushtukiza kwenye mradi wa Machinjio ya Kisasa Vingunguti na kuzuia wananchi wasitozwe kodi hadi mradi utakapokamilika na kuagiza ukamilike kabla ya Desemba.

Katika siku za karibuni, Rais amesikika hata akiwajia juu wateule wake wakiwamo mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi kwa kushindwa kusimamia miradi yenye tija ya moja kwa moja kwa wananchi.

Kujishusha huko hakujaishia kwa Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu tu, lakini hata mawaziri, manaibu na wakuu wa mikoa sasa wameanza kujishusha kwa wananchi wakiiga staili ya viongozi wakuu wa nchi.

Siku nne zilizopita, Majaliwa alitangaza uamuzi wa Baraza la Mawaziri wa kufuta mapori tengefu 12 na ardhi hiyo sasa itagawiwa kwa wananchi kwa ajili ya makazi na kilimo.

Hii maana yake ni kwamba migogoro mingi ya ardhi, angalau sasa itatulia na wananchi wamebaki na kicheko.

Mwezi uliopita, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola alifanya ziara mkoani Kilimanjaro na kuagiza waendesha bodaboda na pikipiki za magurudumu matatu maarufu kwa jina la Bajaji kote nchini kutobughudhiwa na polisi nchi nzima.

Lugola aliwataka polisi kutokamata pikipiki zao na kuzipeleka vituo vya polisi, bali wawaandikie faini kama ilivyo kwa wamiliki wa magari ambazo watazilipa ndani ya wiki moja na si kuzikamata.

Naye Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro amekiri hadharani kuwa kuna mahali Jeshi la Polisi linakosea, akitoa mfano wa matukio mawili yaliyotikisa nchi ya mauaji ya Akwilina Akwiline, aliyekuwa akisoma Chuo cha Usafirishaji (NIT) na David Mwangosi, mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten, kuwa chombo hicho cha dola hakikutimiza wajibu wake ipasavyo.

Baadhi ya mambo ambayo yamekuwa kero kwa wananchi ni wafanyabiashara kulalamikia kunyanyaswa na viongozi wa mikoa na wilaya, wawekezaji kuwekwa mahabusu, Jeshi la Polisi kudaiwa kuwabambikia kesi wananchi, huku wanasiasa wakililaumu jeshi hilo kwa kushindwa kuwadhibiti maofisa wake wanaoonyesha mapenzi yao kwa chama tawala hadharani.

Malalamiko hayo na wimbi la viongozi kuwarudia wananchi limeibua maoni tofauti kutoka kwa wananchi, ambao baadhi wamesema huenda sasa wameanza kumuelewa Rais John Magufuli, ambaye amekuwa akilalamika kuwa wasaidizi wake hawamuelewi.

Na wengine wanasema vitendo hivyo ni dalili kuwa uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwakani umekaribia.

Lakini Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Sima ametetea kitendo cha mawaziri kufanya ziara pamoja akisema unalenga kujua changamoto zinazowakabili na kuzitatua.

Alisema uamuzi huo ni sawa na kupeleka huduma karibu kwa wananchi, ambao wanataka maamuzi kutolewa na mawaziri moja kwa moja licha ya uwepo wa watendaji wengine kama wakuu wa mikoa na wilaya.

“Yanayofuata sasa ni maamuzi ambayo yanahitaji ofisi ama mawaziri kueleza ndio maana tumekuja sasa, badala ya mwananchi kwenda Dodoma au Dar es Salaam tunakuja moja kwa moja kumsikiliza ili tuweze kuyafanyia kazi maoni au malalamiko yake,” alisema Sima akiongea na Mwananchi mkoani Mtwara ambako ameenda pamoja na mawaziri wenzake watano.

Naye kada wa CCM na mbunge wa zamani wa Vunjo (2005-2010), Aloyce Kimaro alisema hali hiyo inatokana na wasaidizi wa Rais kuanza kumuelewa kuwa anataka watatue kero za wananchi. “IGP ametoa hotuba bomba sana na ni wakati kwa kila kamanda wa polisi wa mkoa kujipima kama anatosha katika kusimamia sheria na anatenda kwa mujibu wa PGO (Sheria za Polisi),” alisema.

‘Isiwe kwa ajili ya uchaguzi’

Hata hivyo vitendo hivyo vya watendaji serikalini kurudi kwa wananchi kumeibua maoni tofauti.

Askofu mstaafu wa KKKT, Dk Martin Shao amepongeza hatua ya watendaji wa Serikali walioaminiwa na wananchi kujishusha, lakini akatahadharisha kuwa isiwe ni kwa ajili ya uchaguzi.

“Kama wanashuka ni vizuri sana ila isiwe ni kwa sababu tunaelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu 2020. Tusijishushe Tukilenga kipindi maalumu tu cha uchaguzi,” alisema.

“Viongozi wa Serikali washuke wawahudumie wananchi muda wote na nyakati zote. Wakati wote Serikali itimize wajibu wake. Tukilenga uchaguzi tu hatutawatendea haki wananchi.”

Lakini mkurugenzi wa mawasiliano wa Chadema, John Mrema pia alihusisha kujishusha huko na uchaguzi wa viongozi serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu 2020. “Uchaguzi wa serikali za mitaa umebakiza mwezi mmoja tu na Uchaguzi Mkuu kama mwaka mmoja hivi. Wamefanya tafiti wamegundua hasira za wananchi. Wanajaribu kupooza hasira zao,” alidai.

“Leo polisi wanakiri waziwazi tulikosea kwenye suala la Akwilina, lakini leo tuna viongozi wanahangaika mahakamani. Tunategemea kauli nyingi tamutamu za kubembeleza,” alisema.

David Butinini, mtumishi mstaafu wa Serikali anayeishi Iringa, alisema viongozi wanajishusha kwa vile wamebaini baadhi ya wananchi hawaelewi kile wanachokifanya kwa kuwa maisha hayabadiliki.

“Wako kwenye dilemma (njiapanda) fulani na kama kweli wanajishusha basi waruhusu uhuru wa kweli wa kujieleza maana kama wanamuenzi Nyerere hata yeye aliruhusu hili,” alisema Mzee Butinini.

Katibu mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi alisema kinachotokea sasa ni mwenendo wa kawaida wakati uchaguzi unapokaribia.

“Huku ni kuwaghilibu wananchi wajione wana thamani. (Viongozi) Wanafahamu ni lazima watarudi kuomba kura mwezi mmoja tu ujao na mwakani kwenye Uchaguzi Mkuu. Wasipopiga magoti watapataje kura?” alihoji Muabhi.

Chanzo: mwananchi.co.tz