Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waliokatwa CCM watema nyongo

Waliokatwa CCM.jpeg Waliokatwa CCM watoa ya moyoni

Tue, 15 Nov 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waliotemwa kwenye kinyang’anyiro cha nafasi ya wenyeviti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ngazi ya mikoa na jumuiya zake, wamesema wanakubaliana na uamuzi, baadhi wakisema Mungu ndiye hupanga viongozi.

Pia wamesema wataendelea kuwa na imani thabiti na msimamo wa kukitetea chama hicho bila kuchoka.

Kati ya waliotemwa katika kinyang’anyiro hicho ni waliowahi kuwa wabunge, James Lembeli na Henry Shekifu na waziri wa zamani, Philip Marmo.

Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu jana, aliyeomba kuteuliwa kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Lembeli alisema, hajapokea matokeo rasmi kutoka mawasiliano ya chama hicho zaidi ya kuona kwenye mitandao ya kijamii.

"Nimeona kwenye mitandao ya kijamii orodha ya majina ya waliopitishwa na ambao hawajapitishwa kugombea nafasi hiyo. Jina langu liwepo au lisiwepo nitaendelea kuwa Lembeli, imani na msimamo wangu utakuwa ule ule," alisema na kuongeza:

"Kuna mtu kaja hapa kunipa pole baada ya kuona mtandaoni namuuliza ya nini, mimi kwenye kugombea kuna mambo mawili upate fursa na kuwaongoza wana CCM na Watanzania kwa ujumla, fursa ninayo maana nimeshawahi kuwa kiongozi na hadi sasa nawawakilisha Watanzania kwenye bodi moja duniani."

SHINYANGA

Jana Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Donald Magesa, alitaja majina ya wagombea wa nafasi ya mwenyekiti yaliyopitishwa na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, akiwataja waliopitishwa ni Mabala Mlolwa ambaye anatetea kiti chake kwa awamu nyingine, akichuana na Costantine Nkuba na Eneza Kanuya.

TANGA

Mkoani Tanga, Henry Shekifu aliyejitosa kwenye kinyang’anyiro hicho kwa mara ya tatu mfululizo na jina lake halikurudi.

Katibu wa CCM mkoani humo, Suleiman Charasi, alisema majina ya wagombea yaliyorudi katika nafasi ya Mwenyekiti ni Mathias Mkingwa, Derrick Kazoba na Rajabu Abdallah (aliyekuwa ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Pangani).

SINGIDA

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Alhaj Juma Kilimbah ni kati ya wanachama watano ambao majina yao yalikatwa kutetea nafasi hiyo.

Kilimbah aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida kipindi cha 2017 hadi 2022, hajateuliwa na Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa (NEC) kutetea nafasi hiyo.

Katibu wa CCM Mkoa wa Singida, Lucy Boniface, akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, alisema kati ya wagombea wanane walioomba kuteuliwa kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida walioteuliwa na NEC ni watatu pekee.

Aliwataja walioteuliwa kuwa ni Yusuph Mwandami, (Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Singida), Martha Mlata (mbunge mstaafu) na Amani Ray ambaye ni mkandarasi.

Baadhi ya wanachama ambao ambao hawakuteuliwa na NEC ni pamoja na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa, Kilimbah, Katibu Mkuu mstaafu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Erasto Sima.

Uteuzi wa wagombea wa nafasi za ngazi ya mkoa na Jumuiya za CCM ulifanywa Novemba 13, mwaka huu na kikao cha NEC chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan.

KILIMANJARO

Mwenyekiti wa sasa wa chama hicho mkoani hapo, Patrick Boisafi ni miongoni mwa majina yaliyorudi huku akichuana na Golden Swai na Alphonce Temba.

Boisafi anatetea nafasi hiyo kwa awamu ya pili mfululizo.

Akizungumza kwa njia ya simu, Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Jonathan Mabihya, alisema wagombea wawili, Swai na Temba ni mara yao ya kwanza.

DODOMA

Katibu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Pili Agustino, alitaja walioteuliwa nafasi ya Mwenyekiti kuwa ni Godwin Mkanwa (anayetetea nafasi yake), Adam Kimbisa (aliwahi kuwa Mwenyekiti mwaka 2012 hadi 2017 na Mbunge mstaafu wa Bunge la Afrika Mashariki) na Brigdea Jenerali Augustine Gailanga.

Nafasi ya NEC ni Ismail Jama, Dayana Ngurumo, Ahid Senene, Felista Bura, Donald Mejitii na Nicolaus Haule.

ZANZIBAR

Wagombea uwenyeviti wa zamani majina yaliyorudi na mikoa yao ya kichama kwenye mabano ni Talib Ali Talib (Mjini), Muhamed Rajab (Magharib), Iddi Khamis Ali (Kaskazini Unguja), Mberwa Hamad Mberwa (Kusini Pemba) na Yussuf Ali Juma (Kusini Pemba)

MANYARA

Simon Lulu ni miongoni mwa walioteuliwa kugombea nafasi ya Mwenyekiti Mkoa wa Manyara akitetea nafasi hiyo kwa mara nyingine, huku akichuana na Mkuu wa wilaya wa zamani, Peter Toima na Fraiten Kwahhison.

Majina ya wagombea ambayo hayakurudi ni Omary Kwaang’ na waziri wa zamani, Philip Marmo.

GEITA

Walioteuliwa ni Said Karidushi (anayetetea kiti chake), Daud Sunzu, Kasendamila Nabaya na Wanselho Siwale. Kwenye nafasi ya ujumbe wa NEC, waliopitishwa ni Adeline Kabakame, Lameck Mgasha na Evarist Gervas (anayetetea kiti hicho).

UVCCM

Vian Nchimbi aliyekuwa anawania nafasi ya Mwenyekiti wa UVCCM alisema vijana wote waliojitokeza kuwania nafasi hiyo, wana sifa zote za kuongoza, hivyo ni muhimu kukubali kuwa ni nafasi inayowaniwa na ni mmoja tu anayetakiwa.

Nchimbi ambaye ni Meneja Miradi wa Kampuni tanzu ya CCM iitwayo Jitegemee Trading akiwa tawi la Dodoma, anasema uamuzi uliofanywa na vikao vya chama ni uamuzi wa wanaCCM wote.

"Pamoja na kwamba tunafanya uchaguzi wa viongozi, lakini Mungu ndiye anayeamua ni nani awe kiongozi na kwa wakati gani, hivyo wale ambao wapependekezwa ni uamuzi wa Mungu pia," alisema Nchimbi.

Alisema anawatakia heri wote waliopendekezwa, kwa kuwa lengo la vikao ni kuhakikisha jumuiya hiyo inasonge mbele na kufika salama kule inakokwenda na kwamba mchato mzima ulienda vizuri.

Japhary Kubecha aliyekuwa anawania nafasi hiyo ndani ya UVCCM, alisema amepokea kwa moyo mkunjufu uamuzi wa vikao vya chama kupendekeza majina mengine ya vijana wanaowania nafasi ya mwenyekiti wa UVCCM taifa huku jina lake likikatwa.

Anasema alikuwa miongoni mwa wanachama 200 waliojitokeza kuwania nafasi hiyo, akisisitiza si busara kulazimisha kuteuliwa.

"Niwapongeza viongozi wa chama chetu kwa busara, hekima, maarifa ya kiuongozi ambavyo wametumia kuteua majina hayo, kwani wanatambua hitaji la kisiasa na hali ya kisiasa tulionayo kwa sasa," anlisema Japhary.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live