Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waliochoma bendera, kuvamia ofisi za CUF wapelekwa mahakamani

48714 Cufpic

Tue, 26 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chama cha Wananchi (CUF) kimefungua kesi dhidi ya watu walioshiriki kuchoma bendera na kubadilisha rangi za ofisi zake visiwani na kuweka za Chama cha ACT- Wazalendo.

Kesi hiyo ya kiraia namba 16 ya mwaka 2019, imefunguliwa jana Jumatatu Machi 25, 2019 katika Mahakama ya Vuga iliyopo Mjini Unguja, Zanzibar.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Jumanne Machi 26, 2019  jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa chama hicho, Khalifa Suleiman Khalifa amesema wamekusanya ushahidi wote wa vitendo vilivyofanywa na wanachama wa ACT-Wazalendo ambao wamemfuata aliyekuwa katibu mkuu wa Cuf, Maalim Seif Sharif Hamad.

"Maalim Seif na viongozi wenzake wa CUF walitoa agizo kwamba bendera za CUF zishushwe. Kitendo cha kushusha bendera na kuzichoma ni uvamizi wa ofisi, ni jinai. Sisi hatukutaka kupambana nao kwa kuwa hatuna nguvu, lakini tunajua sheria ndiyo maana tumelifikisha suala hili mahakamani," amesema Khalifa.

Katibu mkuu huyo amewataka Wazanzibari kufuata sheria na kuachana na vitendo vya kukihujumu chama hicho kwa kubadilisha ofisi zake kuwa za ACT-Wazalendo, vitendo ambavyo amesema ni jinai.

"Kwa kuwa mimi ndiyo katibu mkuu mpya, nitahakikisha kwa uwezo wa Mungu ninasimamia mali za CUF zinabaki kuwa mali za CUF,” amesema.

" Kuna usemi wao wanasema shusha tanga, pandisha tanga. Lakini wakumbuke wanaweza kuishia matanga.”

Kuhusu wabunge wa CUF ambao walikuwa upande wa Maalim Seif, Khalifa amewataka wafike ofisi za chama hicho kuonana na mwenyekiti, Profesa Ibrahim Lipumba ambaye aliahidi kushirikiana nao katika kukijenga chama hicho na kusahau tofauti zao.

Soma Zaidi>>>VIDEO: Wanaoshusha bendera za CUF, kupandisha za ACT waonywa

"Wabunge wale wajue kwamba waliingia bungeni kwa tiketi ya CUF wasidhani waliingia kwa tiketi ya Maalim Seif. Yote yamepita, tunachotaka wafike ofisini kumuona mwenyekiti wetu. Hatutakuwa tayari kuona wanatumia rasilimali za chama kuimarisha ACT Wazalendo," amesema Khalifa.

Lipumba atoa neno la faraja vigogo CUF kukimbilia ACT-Wazalendo

 



Chanzo: mwananchi.co.tz