Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Walichosema CHADEMA kuhusu chanzo cha tatizo la machinga

Kigaila ED aibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Benson Kigaila

Wed, 22 Sep 2021 Chanzo: ippmedia.com

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kitafanya utafiti kuhusu wafanyabiashara wadogo, maarufu machinga, kufanya biashara katika maeneo yasiyokuwa rasmi ili kupata njia sahihi za kutatua vikwazo vilivyoibuka.

Akizungumza na Nipashe mkoani Dar es Salaam jana, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Benson Kigaila, alisema hawakubaliani na kile kinachofanywa na serikali kwa sasa na kusema ipo haja ya kulifanyia utafiti wa kina suala hilo kabla ya kutoa uamuzi.

“Suala la machinga ni kubwa sana, sisi tunalifanyia utafiti serious (makini), tunajua impact (athari) yake ni kubwa sana, tunajua kila mwaka nchi hii inazalisha vijana kutoka vyuo mbalimbali ambao hawana ajira.

"Tunajua nchi hii haizalishi ajira yoyote, nchi hii imekaa kiuchuuzi na ndiyo maana tunaongea habari ya machinga, maana yake machinga ni watu wanaouza vitu, huyu akimaliza atataka auze vitu na yule auze vitu sasa tutamuuzia nani?

"Sisi tutalifanyia utafiti mpana ili tukilisemea hili  suala kama msimamo wa chama ambao ni mpana uwe na majibu, hawa jamaa hawana jibu la hiyo kitu, sisi tunataka tutengeneze utafiti wa kutosha tujue shida, ukubwa wake na inaweza kukabiliwa namna gani," alisema.

Hivi karibuni Mbunge wa Kuteuliwa, Humphrey Polepole, aliyewahi kuwa Katibu Mwenezi wa CCM, alisema ni vyema kuzingatia uchambuzi wa wadau kuhusu uhakika wa kupata soko kwa bidhaa za machinga katika maeneo ambapo serikali imepanga kuwahamishia ili kutokuwarudisha nyuma kiuchumi.

Wiki iliyopita Rais Samia Suluhu Hassan, akiwaapisha mawaziri Ikulu mkoani Dodoma, aliagiza wakuu wa wilaya na mikoa nchini kuwapanga vyema na kuonya anayoyaona kwenye runinga ya ngumi, kupigana, kufukuzana, kuchafuliana na vitu kumwagwa kwamba sasa hataki kuyaona tena.

Tayari katika maeneo kadhaa nchini ikiwamo katika majiji ya Dar es Salaam na Mwanza tahadhari imeshatolewa kwa machinga ikiwamo kuweka mabango kuwazuia kufanya biashara katika mifereji ya maji, njia za wapita kwa miguu, hifadhi za barabara na mbele ya maeneo ya taasisi za umma kama shuleni.

*Imeandaliwa na Enock Charles, Leyla Joho (TUDARCo) na Polin Lugaziya (SJMC).

Chanzo: ippmedia.com