Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Walemavu wataka haki kwenye kampeni, nafasi

62f29a3bf1af75b0c82ecbdccb41cd17 Walemavu wataka haki kwenye kampeni, nafasi

Mon, 12 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WALEMAVU nchini wameiomba serikali na wadau wote nchini kuelekea uchaguzi mkuu ujao wawashike mkono kuhakikisha kundi hilo linapata haki ya kushiriki kwenye kampeni, kuwania nafasi mbalimbali za uongozi na kushiriki kupiga kura bila vikwazo.

Akizungumza na HabariLEO mwishoni mwa wiki, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Wenye Ulemavu Tanzania (TNDA),Rehema Kingúngáro ambaye ana ulemavu wa kutoona, alisema watu wenye ulemavu wana haki sawa na wengine wasio nao katika kushiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba 28,mwaka huu.

“Tuna haki sawa na wale wasio na ulemavu, na ndio maana tunahitaji kusikwa mkono tushiriki katika uchaguzi huu, tunashukuru Serikali imefanya mengi kwetu kwa kuchagua wenye ulemavu ambao wana uwezo wa kuongoza na tumeona wakifanya vizuri, sasa kwenye uchaguzi huu tunaomba tusiachwe nyuma,”alisema.

Rehema ambaye kitaaluma ni mwalimu mwenye Shahada ya Uzamili ya Elimu, anafundisha Sekondari ya Pugu jijini Dar es Salaam,alisisitiza kuwa walemavu washikwe mkono washiriki kwenye kampeni kwani kujichanganya huku ni kutengeneza pia mtandao wa ushirika katika masuala mengi yakiwemo ya kukuza vipaji na masoko ya bidhaa watengenezazo.

Alisema TNDA, imepata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura kwa walemavu na kwamba wanafanya hivyo ila kikwazo ni kuwafikia idadi kubwa ya kundi hilo walio maeneo ya pembezoni na vijijini.

Alisema vikwazo vinavyowakuta walemavu nchini ni pamoja na kundi la wasiosikia lakini wanaona, bado katika kampeni hakuna watafsiri wa alama ili kuwawezesha kundi hilo kuelewa kinachozungumzwa, lakini pia wapo wasioweza kutembea ambao nao wanakosa elimu hiyo na kutegemea radio au televisheni .

Alisema pamoja na changamoto hizo na nyingine nyingi, uchaguzi huu kwa mara ya kwanza wamefurahi kusikia kwamba kundi la wasioona ila wanajua kusoma kwa kutumia braili watapata fursa ya kupiga kura kwa kutumia karatasi maalumu zenye maneno ya nukta nundu.

“Hili kwetu ni jambo jema, tunaishikuru Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na serikali kwa kutufikiria na kuona umuhimu wa kuleta karatasi zenye maandishi ya nukta nundu katika uchaguzi kwa ajili ya walemavu wasioona, ila tunaomba karatasi hizo pia zisambae maeneo yote isiwe kwa mijini tu’’,alisema Rehema.

Katibu Mtendaji wa TNDA, Noel Gumbo aliiomba NEC na serikali kuboresha miundombinu ili iwe rafiki kwao huku akitoa mfano kwamba katika kampeni za uchaguzi zinazoendelea, hakuna hata kipeperushi kimoja kilichoandikwa kwa maandishi ya nukta nundu ili kuwasaidia walemavu.

Chanzo: habarileo.co.tz