Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakuu vyombo vya ulinzi, wastaafu washuhudia kiapo cha Dk Tulia

Tulia Kiapo Vymb Wakuu vyombo vya ulinzi, wastaafu washuhudia kiapo cha Dk Tulia

Tue, 1 Feb 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama na baadhi ya viongozi wastaafu leo wamehudhuria mkutano wa uchaguzi wa Spika wa Bunge jijini Dodoma.

Wakuu hao wa vyombo vya Ulinzi na Usalama waliohudhuria kwenye uchaguzi uliofanyika leo Jumanne Februari Mosi 2022 jijini Dodoma, ni pamoja na Mkuu wa Majeshi na Ulinzi (CDF), Venance Mabeyo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Siro, Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), Diwani Athuman, Kamishna wa Jeshi la Magereza, Meja Jenerali Suleiman Mzee na Kamishna Jenerali wa Idara ya Uhamiaji, Dk Anna Makakala.

Wengine ni Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, John Masunga na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Salum Hamdun na Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Gerald Kusaya.

Katika uchaguzi huo pia ulihudhuriwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Katanga, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zuber Maulid, wakuu wa Mikoa ya Mbeya na Dodoma na Mameya wa majiji hayo.

Viongozi wastaafu waliohudhuria uchaguzi huo ni pamoja na Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda pamoja na Maspika wastaafu Anna Makinda na Pius Msekwa.

Spika Tulia pia aliwatambulisha viongozi mbalimbali waliohudhuria katika kikao hicho cha uchaguzi wakiwamo; wabunge wastaafu, viongozi wa CCM, dini, machifu, viongozi wa bodaboda Mbeya pamoja na kundi kubwa la marafiki aliosema walikwenda kushuhudia uchaguzi huo.

Dk Tulia ameibuka mshindi kwa asilimia 100 katika uchaguzi huo ambao umeshirikisha wagombea 9 kati yao wanawake walikuwa wawili ambao ni Dk Tulia Akson (CCM) na Maimuna Kassim (ADC).

Awali akitangaza matokeo, Mbunge wa Jimbo la Isimani, William Lukuvi ambaye alikuwa mwenyekiti wa uchaguzi huo alisema Dk Tulia ameshinda kwa asilimia 100 akijizolea kura zote za wabunge 376.

“Dk Tulia Ackson huyu ni mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) amepata kura zote 376,” alisema Lukuvi huku wabunge wakishangilia.

Lukuvi alisema wapiga kura walikuwa wabunge 376 na hakuna kura iliyoharibika huku wagombea wengine wote nane wakiwa hawajapata kura.

Wagombea wengine waliokuwa wakichuana na Dk Tulia ambaye alikuwa Naibu Spika wa Bunge ni pamoja na Abdullah Mohamed Said (NRA), Aivan Maganza (TLP), Daivd Mwaijojele (CCK) na Georges Busungu (ADA-TADEA).

Wengine ni Kunje Ngombale Mwiru (SAU), Maimuma Said Kassim (ADC), Ndonge Said Ndonge (AAFP) na Saidoun Abrahamu Khatibu.

Wabunge wamefanya uchaguzi wa Spika kutokana na kujiuzulu kwa aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai Januari 6, 2022.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz