Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakongwe wataja siri ya kuchukua fomu CCM

4756382f8f1048f23bfed5dd6943f7de Fomu za kugombea CCM

Fri, 17 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WANASIASA wakongwe waliowahi kuwa wabunge kwa zaidi ya miaka 10 wamejitokeza tena kuchukua fomu kuwania nafasi mbalimbali huku wakiridhishwa na mazingira yaliyopo ndani ya Chama Cha Mapinduzi( CCM)ambayo yamefanikisha kupambana na rushwa na ubadhirifu.

Aliyekuwa mbunge wa jimbo la Kikwajuni kwa vipindi viwili kuanzia 2000 hadi 2010, Parmukh Singh Hoogan amechukua fomu kuwania nafasi ya ubunge huku akisema amevutiwa na mazingira mazuri yaliopo ndani ya CCM ya uwazi na demokrasia iliyotukuka.

Alisema katika kipindi cha uongozi wa Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli chama hicho kipo imara kikiwa kivutio kwa wananchi wengi hadi wapinzani ambapo rushwa na ubadhirifu imekomeshwa.

‘’Nimeamua kuchukua fomu kuomba ridhaa kuwania nafasi ya ubunge kwa tiketi ya CCM ambapo nimechukua fomu kuwania nafasi hiyo baada ya kuridhishwa na mazingira ya uwazi na mapambano ya rushwa yaliyofanyiwa kazi na Mwenyekiti wetu Rais Magufuli,’’alisema.

Aidha aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Welezo kwa tiketi ya CCM Saada Mkuya amebadilisha ‘gia angani’ na kuchukua fomu kuwania nafasi ya uwakilishi katika jimbo la Kikwajuni huku akilitosa jimbo lake la zamani. Mkuya alikuwa Waziri wa Fedha na Mipango katika Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete.

Anatarajiwa kuchuana na mwakilishi anayemaliza muda wake Nassor Salim Ali ‘Jazira’ ambaye tayari amechukua fomu kutetea jimbo hilo. Aidha aliyegombea nafasi ya urais kwa tiketi ya CCM na kuingia katika tano bora, Waziri wa Maji wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Professa Makame Mnyaa Mbarawa alichukua fomu kuwania nafasi ya ubunge katika jimbo la Mkoani Pemba.

Anawania nafasi hiyo mara ya tatu. Aliyekuwa mwakilishi wa jimbo la Makunduchi ambaye ni Waziri wa Nchi ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman amechukua fomu kuwania nafasi ya uwakilishi ambapo hiki kitakuwa kipindi cha nne.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa fomu hiyo katika Ofisi ya Wilaya ya Kusini Unguja, Suleiman alisema ametia nia kuwania nafasi ya uwakilishi kwa ajili ya kuendelea na mikakati ya kusaidia maendeleo kwa wananchi wa jimbo la Makunduchi.

‘’Nimetekeleza ilani ya uchaguzi ya jimbo kwa asilimia 100, bado nia yangu kuleta mabadiliko zaidi ya maendeleo katika sekta zote muhimu ikiwemo elimu,’’alisema.

Mwakilishi anayemaliza muda wake kutoka katika jimbo la Bumbwini, Mtumwa Peya amejitokeza tena kutetea nafasi yake ambapo alikabidhiwa fomu ya kuwania nafasi hiyo katika ofisi ya chama wilaya ya kaskazini Mahonda.

‘’Nimechukua fomu kuomba tena ridhaa ya kuchaguliwa na wananchi katika jimbo la Bumbwini, nimeongoza kwa kipindi kimoja nataka tena kuongeza ili nilete maendeleo,’’alisema.

Aidha Ussi Yahya Haji amechukua fomu kuwania nafasi ya uwakilishi kwa tiketi ya CCM kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

Chanzo: habarileo.co.tz