Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakerwa na wanasiasa wanaotoa lugha za vitisho

Ec204d39e0430e8b3bb5dd15d6b44bf9 Wakerwa na wanasiasa wanaotoa lugha za vitisho

Sun, 25 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

JUMUIYA ya viongozi wanawake kutoka vyama mbalimbali vya siasa, wamelaani tabia ya baadhi ya wanasiasa nchini kutoa lugha za vitisho.

Wamesema tabia hiyo inaweza kusababisha uvunjifu wa amani wakati huu wa kampeni za lala salama kuelekea uchaguzi mkuu.

Walisema hayo katika mkutano maalumu kwa ajili ya uhamasishaji wa makundi mbalimbali kushiriki katika uchaguzi huo.

Mratibu wa jumuiya hiyo, Saumu Rashid alisema kumekuwepo na lugha za vitisho zinazotolewa na baadhi ya viongozi, jambo alilodai kuwa linaweza kuhatarisha amani iliyopo nchini.

Aliwataka watanzania kutumia haki yao ya kikatiba kujitokeza kupiga kura kwa amani na utulivu ili kuliacha taifa salama, kwa kuwa suala hilo ni la mpito linalotokea kila baada ya miaka mitano.

Alisema kimsingi kauli kama hizo zinazojitokeza katika majukwaa ya kisiasa, zinaweza kuvunja umoja wa watanzania uliodumu tangu uhuru. Aliwaomba watanzania kuwaepuka watu wa aina hiyo.

“Mara nyingi zinapotokea vurugu sisi wanawake na watoto ndio waathirika wakubwa, hivyo tunaomba watanzania kuacha kushabikia kauli zozote zinazotolewa na viongozi hao ambao kwetu tunaona kuwa hawalitakii mema taifa letu,”alisema Saumu.

Alisema wanawake kutoka vyama mbalimbali vya siasa, wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha amani ya taifa hili inalindwa wakati wote hata baada ya uchaguzi kumalizika, kwa kuwa jukumu la kufanya hivyo ni la kila mtanzania.

Mratibu wa Taifa wa Wanawake wa Chama cha UMD, Mwajuma Noti alisema suala la kutunza amani ni jukumu la kila mtanzania. Alisisitiza kuwa itikadi za vyama, zisiwafanye watanzania kubaguana na badala yake washirikiane kuilinda.

Alilitaka jeshi la polisi kuwa macho na wavunjifu wote wa amani na kuwachukulia hatua wanaokwenda kinyume na utaratibu, ili kuilinda amani ya taifa hili.

Aliipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa usimamizi mzuri wa mchakato mzima wa uchaguzi tangu kuanza kwake hadi sasa unapoelekea ukingoni. Alitaka watanzania kujiandaa na kutumia haki yao ya kikatiba, kupiga kura Oktoba 28 mwaka huu.

Chanzo: habarileo.co.tz