Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waitara asema gharama za kurudia uchaguzi hazimhusu, anataka ubunge

12047 Pic+waitara TanzaniaWeb

Wed, 15 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mbunge wa Ukonga kwa tiketi ya Chadema kabla ya kuhamia CCM, Mwita Waitara amesema suala la gharama za kurudia uchaguzi halimhusu bali anachotaka ni kuhakikishiwa ubunge wake.

Akizungumza katika mahojiano na Mwananchi leo Agosti 15, Waitara amesema ameamua kuhama baada ya kuona nafasi yake ya ubunge inatishiwa kutokana na kudorora kwa uhusiano kati yake na Mwenyekiiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Hata hivyo, Mbowe alipotafutwa kwa njia ya simu kujibu kauli hiyo, amesema hawezi kuzungumza kwa kuwa yuko kwenye kikao cha kamati kuu ya chama hicho.

Awali Waitara alipotangaza kuondoka Chadema Julai 28, Mbowe aliliambia Mwananchi kuwa hakuwahi kumzuia kugombea uenyekiti wala kuwa na ugomvi naye.

“Sitegemei mtu akiondoka Chadema akamsifu Mbowe, lazima atarusha mawe kwenye mti wenye matunda,” alikaririwa Mbowe.

Katika maelezo yake Waitara amesema alishatofautina na viongozi wa Chadema akiwamo Mbowe jambo lililohatarisha nafasi yake ya ubunge siku za usoni.

“Kuna mambo ndani ya chama yanafanya hata huo mchango wangu ndani ya Bunge uonekani si kitu,” amesema na kuongeza:

“Mwenyekiti amekuja Ukonga wakati wa Bunge, akapiga mahesabu akisema Waitara anaona ubunge unampa nafasi kubwa ya kusema makao makuu, anakuwa busy sana kuzungumza uchaguzi ndani ya chama.”

Amedai kuwa Mbowe aliunda timu ya kumchunguza ikiwa pamona na kuweka viongozi wa mashina, kata na jimbo wanaomtii yeye.

“Maana yake ukienda mkutano mkuu hao viongozi wa kata na jimbo ndiyo watakaopiga kura ya maoni. Maana yake mimi sitashinda, ina maana sitapitishwa, halafu nitaanza kutafuta huruma za Mwenyekiti ambaye nimeshakorofishana naye, sasa unashindaje?” amehoji Waitara.

Ameongeza: “Kwa hiyo nikaona huyu anataka nikisha kuwa dhaifu kwenye serikali za mitaa, huwezi kuwa na kauli.

Alipoulizwa kuhusu kurudia kwake uchaguzi kuna gharama ambayo ingeweza kutumika kwenye miradi ya jamii alisema hilo halimhusu.

 “Kodi ina matumizi yake na kila idara ina bajeti yake na Tume ya Uchaguzi ina bajeti yake. Sina ushahidi kwamba mradi umekwama kwa sababu tumekwenda kwenye uchaguzi, kwenye suala kwamba uchaguzi unafanyika au haufanyiki hilo halinihusu mimi,” amesema Waitara.

Huku akisisitiza kuulinda ubunge wake, Waitara amesema kama sheria zingeruhusu Mbunge kuendelea na nafasi yake bila kuwa mwanachama wa chama cha siasa, asingejiunga na chama chochote.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz