Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wahariri walivyoibana Nec kuhusu makada, ma-DED, mawakala wa vyama vya siasa

63909 Pic+ded

Sun, 23 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

“Nec hakuna shabiki wa chama na hakuna mwanachama yeyote wa chama cha siasa, kama ikitokea basi anabanwa na sheria.” Ni kauli ya Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Jaji Semistocles Kaijage.

Haikuwa rahisi kwa Jaji Kaijage kutoa majibu hayo kwa kuwa lilipoulizwa kwa mara ya kwanza kuhusu kuwapo kada wa CCM ndani ya NEC alisema; “Nilisahau kuwaambia haturuhusu kuuliza maswali yanayomlenga mtu.”

Jaji Kaijage aliwaalika wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari kuzungumzia kuanza mchakato wa kuboresha Daftari la Kudumu la Wapigakura, hata hivyo wakati wa mjadala ndipo yalipoibuka maswali kuhusu makada ndani ya Nec, Ma-ded kusimamia uchaguzi na suala la mawakala wa vyama vya siasa hasa wa upinzani.

Mmoja wa wahariri alimuuliza Jaji Kaijage kwamba kwenye meza kuu walipokaa makamishna wa Nec kuna kada wa CCM ambaye amewahi kuwa katibu mwenezi wa chama nafasi ambayo anayo Humphrey Polepole kwa sasa. Huku akimtaja kwa jina Omari Ramadhan Mapuri; “hivi kweli...utakuwa tayari kumtangaza mgombea wa upinzani mshindi kama mgombea wa chama chako akishindwa?”

Swali hilo lilimfanya Jaji Kaijage awatangazie wahariri wote waliohudhuria mkutano huo kwamba hairuhusiwi kuuliza swali linalomlenga mtu binafsi.

Mhariri aliyeuliza swali hilo aliamua kuliacha kwa kusema analiondoa kwa kuwa anaona limeanza kuleta shida.

Pia Soma

Lakini, alipotoa nafasi kwa mhariri mwingine kuulizwa swali, naye alirejea kuuliza tena kuhusu kamishna huyo kwamba haki itatendeka vipi ikiwa mmoja wa makamishna (naye huku akimtaja kwa jina) kwamba ni kada wa CCM.

Jaji Kaijage safari hii akanona ni vema kujibu japo kwa ufupi kwamba watendaji wote wa Tume huwa wanakula viapo viwili, kwanza kiapo cha kutunza siri na pili kiapo cha kutenda haki.

Kwa hiyo makamishna wote walioteuliwa wanalazimika kufuata sheria za Tume na zile za nchi.

Hata hivyo, alipotoa nafasi kwa mhariri mwingine kuuliza swali naye swali lake la pili lilikuwa ni kuhusu kamishna kada huku akimtaja kwa jina kwamba haoni kama kuna haki itatendeka. Jaji Kaijage aliona kama ni msumari wa moto unaoendelea kushindiliwa kwenye Tume yake, hivyo aliamua kujibu kwa kirefu huku akitumia maneno yenye busara na kufanya marejeo ya historia ya Watanzania wengi.

Anasema makamishna wa Tume waliokuwa makada wanabidi wafuate sheria za Nec zinazowakataza kuwa wanachama wa vyama vya siasa.

“Wengine wana historia mbalimbali na pia kutegemeana na wakati na umri wao. Wanaongoza Tume ni Watanzania haohao ambao zamani walikuwa wanachama wa Tanu ni haohao hakuna wengine watakaokuwa na historia tofauti,” anasema.

Jaji Kaijage anasisitiza kwenye Tume hakuna mwanachama hai wa chama cha siasa, kama alikuwa mwanachama sheria za Tume zinambana.

Pia, Jaji Kaijage anasema kwenye Tume kuna fomu za kujaza zikiwataka kutangaza kwamba siyo tena viongozi wa chama cha siasa. “Maadili nayo yanawabana. Nec hakuna shabiki wala hakuna mwanachama yeyote wa chama cha siasa, kama ikitokea basi anabanwa na sheria.”

Vilevile, Jaji Mary Longway ambaye ni kamishna wa Tume naye alilitolea majibu hoja kuhusu Mapuri kwamba hawezi kutangaza matokeo, hata kama mgombea anayemshabikia atakuwa ameshindwa, atakachofanya ni kuumia moyoni tu.

Kuhusu ma-DED

Licha ya Jaji Kaijage kuimaliza hoja hiyo, bado aliulizwa swali kuhusu uamuzi wa Mahakama Kuu wa kubatilisha vifungu vya 7 (1) na 7 (3) vya Sheria ya Uchaguzi kama watavitumia kwenye Uchaguzi Mkuu ujao.

Akijibu swali hilo, Jaji Kaijage anasema Nec inaongozwa kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi na kwamba mahakama ilitimiza wajibu wake kwa kubatilisha vifungu vilivyolalamikiwa na kwamba vifungu hivyo havitatumika katika utekelezaji wa majukumu ya Tume.

Vifungu vyote hivyo vinawataja wakurugenzi wa jiji, wakurugenzi wa manispaa, wakurugenzi wa miji na wakurugenzi wa wilaya (ma-DED) kwamba watakuwa wasimamizi wa uchaguzi katika maeneo yao.

Kutotumika kwa vifungu hivyo vilivyomo kwenye Sheria ya Uchaguzi kumetokana na uamuzi wa Mahakama Kuu wa kuvibatilisha kwa kuwa vinakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Mei 10, 2019 jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu, Atuganile Ngwala, Dk Benhajj Masoud na Firmin Matogolo lilitoa uamuzi huo.

Kiongozi wa jopo hilo, Jaji Ngwala alisema vifungu 7(1) na 7(3) vya Sheria ya Uchaguzi vinakiuka Katiba kwa kuwa vinakwenda kinyume na matakwa ya kikatiba ya uhuru wa Tume ya Uchaguzi.

Katika hukumu hiyo, Jaji Ngwala alisisitiza kuwa sheria hiyo haihakikishi kuwa wakurugenzi hao watakuwa huru katika utekelezaji wa majukumu yao.

Jaji Ngwala alisema ameridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mdai kuwa wakurugenzi wengi ni wana CCM kwa kuwa wakurugenzi 74 ambao orodha yao imewasilishwa mahakamani ni wanachama wa chama hicho.

Hukumu hiyo ilitokana na shauri lililofunguliwa mahakamani hapo na mwanaharakati Bob Chacha Wangwe dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) akipinga wakurugenzi hao kuwa wasimamizi wa uchaguzi kwa niaba ya Nec pamoja na mambo mengine akidai ni wateule wa Rais ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM.

Hata hivyo, Jaji Kaijage alifafanua kuwa wasimamizi wa uchaguzi huwa wanaapishwa kwa viapo viwili, cha kwanza ni kutenda haki kwa mujibu wa sheria za uchaguzi na pili ni kutunza siri.

Anasema pia wasimamizi wa uchaguzi wakiwamo wakurugenzi wakati wa kupewa kazi hiyo wanatakiwa kutoa tamko la kukana uanachama kwa chama anachokiunga mkono na hivyo kuaminika kuwa atatenda haki.

Jaji Kaijage alitoa mfano wa uchaguzi wa udiwani wa kata 43 kwamba kuna mkurugenzi alilalamikiwa na Nec haikumteua kusimamia uchaguzi.

Akisisitiza hilo, Kamishana wa Nec, Asina Omari alitoa mfano mwingine kwamba kuna baadhi ya wasimamizi wanapotakiwa kutoa tamko la kukana uanachama wao huwa hawakubali na hivyo Nec haikuwateua kusimamia uchaguzi.

Mawakala wa vyama

Wahariri pia walimuuliza Jaji Kaijage namna Nec iliyojipanga kufanya kazi na mawakala wa vyama vya siasa ili kuepuka malalamiko ambayo mengine yalisababisha maumivu kwa wananchi wengine ambao hawakuhusika na masuala ya uchaguzi wala hawakuwa wanasiasa.

Mfano wa maumivu kwa wananchi wasiohusika ni mauaji ya mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT), Aqulina Akwilini aliuawa kwa kupigwa risasi wakati wafuasi wa Chadema na viongozi wao walipoandamana kwenda Nec kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi kudai barua kwa wasimamizi wao kwenye uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kinondoni.

Malalamiko ya mawakala wanaoteuliwa na vyama vyao kusimamia uchaguzi mengi yanahusu kutopewa barua za kutambuliwa na Nec kusimamia uchaguzi au kupewa kwa kuchelewa.

Hata hivyo, Jaji Kaijage akijibu hilo anasema kuna tatizo linalofanywa na baadhi ya vyama vya siasa kwa kutowasilisha malalamiko kwa wakati au kupitia kwenye ngazi husika za kamati ya maadili.

Anasema tatizo la vyama vya vingi vya siasa vinapokuwa na malalamiko badala ya kuyafikisha kwenye sehemu husika, wao huamua kuitisha mikutano ya waandishi wa habari kulalamika au kuruka ngazi ya vikao vya maadili na kuamua kwenda ngazi ya taifa.

Jaji Kaijage anasema wakati mwingine vyama vinashindwa kuwasilisha malalamiko kwa wakati na hivyo kushindwa kupata haki yao kama walikuwa na malalamiko yenye ushahidi wa uliotimia.

Alitoa mfano wa malalamiko ya mawakala waliofukuzwa kwenye uchaguzi wa marudio katika Jimbo la Monduli mkoani Arusha kwamba vyama havikufuata utaratibu wa kupeleka majina ya mawakala mapema. Badala yake siku ya uchaguzi vikapeleka mawakala vituoni bila kupitia Nec ili kupewa utaratibu ikiwamo kula kiapo.

Anasema hakuna aliye juu ya sheria , wakiwamo wakurugenzi, Nec, vyama vya siasa na wananchi, hivyo msimamizi wa uchaguzi atakayefanya uonevu wa makusudi atachukuliwa hatua za kisheria.

Pia, msimamizi atakayesababisha matokeo ya uchaguzi kutenguliwa kutokana na uzembe wake naye atachukuliwa hatua za kisheria

Chanzo: mwananchi.co.tz