Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wagombea wasuburi hukumu keshokutwa

972a812d391d4ffb8f103a050e142d3c Wagombea wasuburi hukumu keshokutwa

Sat, 18 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MAMIA ya wagombea wa ubunge na uwakilishi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamerejesha fomu tayari kwa kukabiliana na ‘hukumu’  ya mchujo itakayoanza keshokutwa. Aidha, baadhi ya wanachama waliochukua fomu, wameshindwa kuzirudisha katika muda wa ukomo uliopangwa, hali inayodhihirisha kujiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho, kilichoandika historia kutokana na wingi wa watu waliojitokeza, jambo ambalo halijawahi kushuhudiwa.

Takwimu zilizotolewa juzi na Rais John Magufuli, zinaonesha wanachama 8,205 walikuwa wamechukua fomu ya kugombea nafasi za ubunge na uwakilishi nchi nzima. Mkoa wa Dar es Salaam ulikuwa unaongoza kwa kuwa na wanacha CCM 829 waliokuwa wamechukua fomu, ukifuatiwa na Kagera wanachama 328, Arusha 320, Kilimanjaro 82 na Kusini Unguja 53.

Rais alisema kuwa waliochukua fomu kuwania ubunge katika majimbo hadi juzi walifikia 6,533, ubunge wa Viti Maalum ni 1,539 na walioomba nafasi za uwakilishi ni 133 na kufanya jumla ya wagombea 8,205.

Mbeya:

Taarifa za makatibu wa CCM wa wilaya zote za mkoani Mbeya, zilisema hadi jana mchana, waliojitokeza kuchukua na kurejesha fomu za kuwania ubunge kwenye majimbo mbalimbali ni  wanachama CCM 245. Katibu wa CCM Wilaya ya Rungwe, Clemence Mponzi, alisema Jimbo la Rungwe waliojitokeza ni wanachama 44  na Busokelo ni 25. Upande wa Mbeya Vijijini, Katibu wa CCM wilayani humo, Rehema Nzunye, alisema waliojitokeza ni 41. Jimbo la Kyela waliojitokeza, kwa mujibu wa Katibu wa CCM wa Wilaya, Lucas Nyanda, ni wanachama  41.

Katibu wa CCM Wilaya ya Mbarali, Abdallah Mpokwa, alisema walijitokeza wanachama 37. Katibu wa CCM Wilaya ya Mbeya Mjini, Gervas Ndaki, alisema waliojitokeza ni wanachama 34 na kwa upande wa Chunya, Katibu wa wilaya hiyo alisema wanachama waliojitokeza ni 23.

Dodoma:

Katibu wa CCM wa Mkoa wa Dodoma, Pili Mbanga alisema  wagombea  266 walichukua fomu huku zaidi ya asilimia 89 wakiwa wanaume. Kati ya hao, wanaume ni 239 na wanawake 27. Upande wa Umoja wa Wanawake (UWT) waliojitokeza ni 74, Umoja wa Vijana (UVCCM) 22 na Wazazi alijitokeza mmoja. Hakuna mwanamke aliyejitokeza majimbo ya Kibakwe na Kongwa.

Ruvuma:

Jumla ya wanachama 174 mkoani Ruvuma, wamejitokeza kupeperusha bendera ya chama katika majimbo nane. Katibu wa CCM Songea Vijijini, Mohamed Lawa alisema Jimbo la Songea Vijijini lenye majimbo mawili,

Peramiho wamejitokeza wagombea 13 na Madaba wagombea 10.

Katika jimbo la Nyasa, Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Abbas Mkweta alisema walijitokeza wanachama 13 na Jimbo la Namtumbo ni wanachama 32. Upande wa Wilaya ya Tunduru, Katibu wa CCM wa Wilaya, Kite Mfilinge alisema jimbo la Tunduru Kaskazini  ni wanachama 18  na Tunduru Kusini walijitokeza wanachama 11.

Katibu wa CCM Wilaya ya Songea Mjini, Juma Mpeli alisema 31 walijitokeza katika jimbo la Songea Mjini. Upande wa wilaya ya Mbinga, Katibu wa chama hicho wa wilaya, Domina Soko alisema Mbinga Vijijini walirudisha fomu wote 29.

Tabora:

Waliojitokeza mkoani Tabora ni 346, ambao kati yao 14 ni wanawake. Katibu wa CCM Mkoa wa Tabora, Solomon Kasaba alitaja jimbo na idadi ya wagombea kwenye mabano ni Tabora Mjini (53), Urambo (25), Igunga (36), Manonga (17), Ulyankulu (18), Kaliua (15), Nzega Mjini (12), Nzega Vijijini (19), Bukene (39), Sikonge (22), Tabora Kaskazini (25) na Igalula wanane.

Iringa :

Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Brown Mwangomale alisema waliojitokeza katika majimbo saba ni wagombea  319.

Walioingia mitini:

Katibu wa CCM wa Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Domina Soko alisema waliochukua fomu ni 20 lakini waliorudisha ni 17.  Katibu wa Umoja wa Wanawake (UWT)mkoani  humo, Rukia Mkindu alisema kati ya wanachama 40 waliochukua fomu, mmoja hakurudisha.

Dar es Salaam:

Waliochukua na kurejesha fomu kuwania ubunge mkoani Dar es Salaam ni wanachama 1,210. Wanagombea kwenye majimbo tisa na kati yao, watu wapatao 10 hawakurudisha fomu. Katibu wa CCM Wilaya ya Ilala, Idd Mkowa alisema wilaya hiyo ina majimbo matatu, ambapo  Jimbo la Ilala waliochukua fomu ni 35, Segerea 93 na Ukonga 146.

Mwanachama mmoja hakurejesha fomu. Katibu wa CCM Wilaya ya Temeke, Andrea Gwaje alisema wanachama 177 walichukua na kurejesha fomu. Kati yao, 86 ni wa jimbo la Temeke na mmoja hakurejesha. Katika Jimbo la Mbagala, waliorudisha fomu ni 91 na watano hawakurudisha.

Katibu wa CCM Wilaya ya Kinondoni, Mwasanguti wilaya hiyo ina majimbo mawili, ambapo wanachama 176 walirejesha fomu katika Jimbo la Kawe 81 walirejesha fomu Jimbo la Kinondoni.

Aidha, Katibu wa CCM Wilaya ya Ubungo, Chief Yaredi alisema 277 walichukua na kurejesha fomu katika majimbo mawili yaliyopo, ambapo  170  Jimbo la Kibamba na 107 Jimbo la Ubungo.

Kilimanjaro:

Katibu wa CCM wa Mkoa wa Kilimanjaro, Jonathan Mabihya alisema wanachama tisa kati ya 497 waliochukua fomu kugombea Ubunge wa majimbo na viti maalumu, wameshindwa kurejesha fomu zao.

Manyara:

Katibu wa CCM Wilaya Babati Vijijini,  Filbert Mampwepwe alisema  wanachama 46 walichukua fomu, ambao kati yao sita ni wanawake. ‘Hukumu’ Jumatatu Kulingana na ratiba iliyotolewa hivi karibuni na Katibu Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, Julai 20 hadi Julai 22 itafanyika mikutano mikuu ya CCM ya majimbo au wilaya na wawakilishi, kwa ajili ya kupiga kura za maoni za wagombea wa ubunge na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Akizungumza na  HabariLeo jana, Katibu wa CCM wa Wilaya ya Nanyumbu, Didas Zimbihile alisema watafanya mkutano mkuu wa wilaya Jumatatu, kwa ajili ya kupiga kura za maoni za wagombea ubunge.

Alisema katika jimbo la Nanyumbu, waliochukua na kurejesha fomu  ni wanachama 16 ambao wote watapewa nafasi ya kujieleza kwenye mkutano mkuu, kabla ya kupigiwa kurakisha kujadiliwa, kabla ya kupata majina matatu ya kuwasilisha kwenye hatua nyingine.

Kwa upande wa mkoa wa Dar es Salaam, makatibu wa CCM wa wilaya zote, walisema kila kitu kitakwenda kwa mujibu wa ratiba ya chama ilivyoainisha, bila kujali idadi ya wagombea waliojitokeza.

Katibu wa CCM wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mabihya alisema baada ya kuhitimisha mchakato wa urejeshaji fomu, chama kitaanza mchakato wa kuchuja wagombea kulingana na kanuni, maadili na katiba .

Chama kinakwenda na utaratibu mpya wa kupata wagombea wa ubunge na uwakilishi, baada ya kubaini uliotumika mwaka 2015 ulikuwa na upungufu kutokana na kuacha mianya ya rushwa na uvunjifu wa taratibu Chini ya utaratibu zamani, mgombea ubunge alitakiwa kupita kata kwa kata na kwenye matawi kwa ajili ya kupigiwa kura za maoni.

Ratiba vikao Taarifa ya Polepole ya wiki iliyopita ilisema baada ya Juni 30, vikao vya kamati za siasa za majimbo, vitafanyika kujadili wagombea na kutoa mapendekezo yake kwa Kamati za Siasa za Wilaya. Agosti Mosi na Agosti 2 vikao vya kamati za siasa za wilaya, vitakaa kujadili wagombea na kutoa mapendekezo yake kwa kamati za siasa za mikoa.

Agosti 4 na 5 vikao vya kamati za siasa za mikoa, vitakaa na kujadili wagombea na kutoa maoni yake kwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya  Taifa (NEC) ya CCM  kwa Tanzania Bara. Kwa upande wa Zanzibar, watatoa mapendekezo kwa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa Zanzibar.

 

Chanzo: habarileo.co.tz