Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wagombea udiwani saba wa CCM Arusha wapita bila kupingwa

11456 Udiwani+pic TanzaniaWeb

Mon, 16 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Arusha kimepata mteremko katika kata saba kati ya 20  baada ya wagombea wake kupita bila kupingwa.

Kata sita kati ya hizo, wagombea wa chama hicho tawala wamepita bila kupingwa baada ya wagombea wa Chadema kushindwa kurejesha fomu huku katika kata nyingine mgombea wa Chadema akibainika kutojua kusoma.

Wakizungumza na MCL Digital leo Jumapili Julai 15, 2018, wasimamizi wa uchaguzi katika halmashauri ya Longido, Monduli na Ngorongoro wamesema baada ya wagombea hao kuondolewa taratibu za uchaguzi katika kata nyingine zinaendelea.

Msimamizi wa uchaguzi wilaya ya Longido, Jumaa Mhina amesema katika halmashauri yake mgombea wa  Chadema kata ya Alang'atadapash,  Isaya Laizer hakurejesha fomu.

"Katika kata hii CCM imemsimamisha Jacob Mollel kwa hiyo amepita bila kupingwa,” amesema.

Amesema katika  kata ya Kamwanga mgombea wa Chadema, Sakimba Alais  amewekewa pingamizi kwa madai ya kutojua kusoma.

Msimamizi wa uchaguzi halmashauri ya Ngorongoro, Raphael Siumbu amesema kati ya kata tano za halmashauri hiyo,wagombea wanne wa CCM wamepita bila kupingwa.

Amezitaja kata hizo kuwa ni Soitsambu, Pinyinyi, Ngoile na Ngorongoro, kwamba kata moja ya Alaitole mgombea wa Chadema alirejesha fomu.

"Katika hii kata mgombea wa Chadema amewekewa pingamizi lakini tunachunguza,”amesema.

Msimamizi wa uchaguzi halmashauri ya Monduli, Steven Ulaya amesema kati ya kata sita, kata mbili za Nararami na Loksale wagombea wa Chadema hawakurejesha fomu.

Hadi jana Chadema ilikuwa imesimamisha wagombea katika kata zote nne za  Jiji la Arusha, na nyingine mbili katika halmashauri ya Karatu na Meru.

Mwenyekiti wa Chadema mkoani hapa, Aman Golugwa amesema chama hicho kina  uzoefu na chaguzi za marudio na kinafuatilia kwa makini uchaguzi katika kata zote.

“Tunajua mizengwe inayoendelea ili kuondolewa kwa baadhi ya wagombea wetu lakini chama kinafuatilia,” amesema.

Akizungumza na MCL Digital, katibu mwenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Shaban Mdoe amesema chama hicho tawala kimejipanga kuibuka na ushindi katika kata zote 20.

Wagombea wa CCM katika kata 19 kati ya 20 za mkoani Arusha walikuwa madiwani wa kata hizo kwa tiketi ya Chadema kabla ya kujiuzulu na kuhamia CCM.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz