Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wagombea Vijana ACT-Wazalendo wachuana vikali jukwaani

Act Wazalendo Vijana Mchuano.png Wagombea Vijana ACT-Wazalendo wachuana vikali jukwaani

Wed, 28 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baadhi wagombea uenyekiti wa ngome ya vijana ya ACT- Wazalendo wamesema upungufu uliyojitokeza katika utawala wa ngome unaomaliza muda, ni miongoni mwa sababu zilizowasukuma kuwania kiti hicho kinachoshikiliwa na Abdul Nondo anayemaliza muda wake.

Walisema hayo jana jioni, Februari 27, 2024 katika mdahalo wa ngome wa vijana wa ACT- Wazalendo, uliofanyika ukumbi wa Haikainde Hichilema uliopo makao makuu ya chama hicho Magomeni, jijini Dar es Salaam. Uchaguzi wa ngome hiyo utafanyika kesho Alhamisi, Februari 29, 2024.

Wakati hao wakieleza hayo, wagombea wengine wamesema watatumia uzoefu wao kuongoza ngome hiyo kwa miaka mitano.

Wagombea wa uenyekiti wa ngome walioshiriki mdahalo huo ni pamoja na Nondo (anayetetea nafasi hiyo), Julius Massabo, Ruqayya Nasir na Petro Ndolezi.

Ndolezi alikuwa kwanza kufungua dimba la kunadi sera zake, akisema upungufu uliojitokeza katika utawala wa Nondo, ndio sababu iliyomfanya kuwania uenyekiti ili kuipeleka ngome ya vijana mbele zaidi na kuwa kimbilio la vijana wote wa Tanzania.

Katika maelezo yake, Ndolezi aliyekuwa katika timu ya sekretarieti ya Nondo, amesema atatumia uzoefu wake wa siasa alioupata kwa nyakati tofauti ndani ya chama hicho, ili kuongoza ngome ya vijana.

Ndolezi amesema ameitumikia ACT- Wazalendo kwa nyakati tofauti ikiwemo kushiriki operesheni za kuimarisha uhai wa chama hicho.

"Nimeamua kubeba dhamana ya uenyekiti ngome za vijana, ili nitumie maono yangu ya kuunganisha vijana, endapo nikifanikiwa tutaendeleza mazuri yote yaliyofanywa na uongozi wa ngome unaomaliza muda wake, upungufu uliojitokeza tutayafanyia kazi.

"Tutahakikisha ngome ya vijana inakuwa kimbilio la vijana wote wa Tanzania, sambamba na kuifungua ngome ya vijana ndani ya nje ya nchi," amesema Ndolezi ambaye ni Waziri Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Wakati Ndolezi akieleza hayo, Massabo aliyekuwa kwenye timu ya sektarieti ya Nondo, amesema yupo tayari kuchukua dhamana ya uenyekiti wa ngome akidai upungufu uliojitokeza katika utawala wa ngome unaomaliza muda wake ndio sababu iliyomvutia.

"Upungufu uliojitokeza ni sababu iliyonivuta kuwania kiti hichi, ngome iliyopita ilikosa ubunifu ikiwemo kutafuta vyanzo mbadala vya mapato ya kujiendesha katika shughuli za kujiimarisha kuanzia katika ngazi ya chini.

"Tunawajibu wa kujenga ngome ya vijana imara kitaasisi kuanzia kata hadi taifa, nipo tayari kubeba maono, taswira na haiba ya kuongoza ngome, tutajenga hamasa ya kuhamasisha vijana kushiriki uchaguzi asilimia 70 wa ugombea udiwani wawe vijana," amesema Massabo.

Massabo na Ndolezi ni miongoni mwa viongozi walioondolewa katika utawala wa Nondo kwa nyakati tofauti wakidaiwa kushindwa kutimiza majukumu yao kwa ufanisi.

Hata hivyo, Nondo amejivunia utendaji kazi wa miaka minne wa kuongoza ngome hiyo, akisema anawania nafasi hiyo kwa mara nyingine, ili kuijenga zaidi ngome ya vijana ya ACT- Wazalendo. Amesema katika kipindi cha uongozi wake amefanya makubwa yanayopaswa kuendelezwa.

Amesema walianza ngome ya vijana mwaka 2020 kwa miaka miwili ya mwanzo hawakupewa ruzuku hata Sh10 na chama hicho, lakini walifanya kazi kufika maeneo mengi.

Nondo amesema katika kukabiliana na changamoto hiyo, walianzisha mradi wa kadi za vijana zilikuwa zikilipiwa na wanachama.

"Endapo nitachaguliwa tena nitatoa mafunzo ya kuwajengea uwezo vijana wa chama hiki, kuongeza wigo wa mapato na kutetea maslahi ya vijana katika vikao mbali mbali vya chama," amesema Nondo.

Ruqayya ambaye ni mgombea mwanamke pekee katika nafasi hiyo, amesem anagombe nafasi hiyo kwa sababu ya mbalimbali ikiwemo uongozi katika unaomaliza muda wake kukabiliwa na ukata wa fedha katika kujiendesha, lakini wahusika wameshindwa kuwa wabunifu.

"Kukosa mikakati bora kwa mwenyekiti anayemaliza muda wake umefanya ngome kushindwa kufanya uenezi wa katika maeneo mengi ya Tanzania.

"Nitatumia uzoefu wangu wa kisiasa wa kuongoza ngome hii, naamini kwenye nafasi hii nina uwezo mkubwa wa kuimarisha zaidi ngome hiyo kuanzia tawi hadi taifa," amesema Ruqayya.

Amesema iwapo atachaguliwa na wajumbe mwenyekiti wa ngome hiyo atahakikisha wanatengeneza vyanzo vya kudumu vya fedha, ili kufanya kazi kwa weledi mkubwa zaidi kuimarisha ngome hiyo.

"Nataka kuifanya ngome kuwa kimbilio la vijana wote Tanzania na sehemu yao ya kusemea yale yanayowakabili, nitaongoza ngome itakayohakikisha inalinda rasilimali za Taifa na kupinga rushwa," amesema.

Leo Jumatano, Februari 28, 2024 kutakuwa na mdahalo wa wagombea uenyekiti, ngome ya wanawake.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live