Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wagombea CHADEMA waanza kusaka kura

Wagombea CHADEMA Wagombea Chadema waanza kusaka kura

Sat, 18 May 2024 Chanzo: Mwananchi

Siku moja baada Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuteua majina ya watakaowania uongozi katika kanda nne kwenye uchaguzi utakaofanyika Mei 29, 2024 baadhi ya wagombea wamefunguka walivyojipanga kusaka kura, huku wengine wakianza kampeni kupitia mitandao ya kijamii.

Jana Ijumaa Mei 17, 2024 Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alitoa orodha ya wagombea wa kanda hizo waliopenya katika usaili uliofanywa na kamati kuu iliyoketi kuanzia Mei 11 hadi 14.

Kanda zitakazofanya uchaguzi ni Serengeti yenye mikoa ya Mara, Shinyanga na Simiyu, Magharibi (Tabora, Katavi na Kigoma), Nyasa (Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe na Rukwa) na Victoria (Mwanza, Kagera na Geita).

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi Digital leo Jumamosi Mei 18, 2024 baadhi ya wagombea hao wamesema baada ya majina yao kupitishwa, kinachofuata ni kuanza kampeni kwa wajumbe watakaoingia katika vikao vya kufanya uamuzi wa kuchagua.

Mgombea uenyekiti wa Kanda ya Magharibi, Dickson Matata amesema kazi iliyopo mbele yake ni kwenda mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi kusaka kura zitakazomwezesha kuibuka kidedea katika uchaguzi huo.

Amesema amejipanga kuwazungukia wapiga kura katika mikoa hiyo, kwa lengo la kuwaomba wamchague katika uchaguzi huo, lakini pia atatumia mitandao ya kijamii kufanikisha azma yake ya kusaka kura.

“Nakishukuru chama kwa kuniamini na kunipa nafasi ya kugombea uenyekiti wa Magharibi yenye majimbo 25, nina wajibu mkubwa katika kuhakikisha nina shinda na miongoni mwa vipaumbele vyangu ni kusimamisha wagombea katika maeneo yote,” amesema Matata.

“Niliomba nafasi kwa sababu kuu mbili, mosi natamani migogoro iishie kati ya viongozi na viongozi, hili nitakwenda kulisimamia nitakaposhika usukani, nataka kuleta umoja na mshikamano miongoni mwa wanachama wa Chadema.”

Matata ambaye kitaaluma ni mwanasheria amejinasibu kuwa ana uzoefu wa kutosha kwenye kanda hiyo, akisema awali alitumikia ukatibu wa kamati ya sheria na haki za binadamu kwa miaka kadhaa, hivyo anaijua vema nafasi anayoomba kuiongoza.

Matata amesema wakati akihudumu nafasi hiyo, migogoro ndani ya kanda ikitokea walikuwa wanashirikiana pamoja katika utatuzi na kila kitu kinakuwa sawa, hivyo anataka kurudisha nguvu na umoja huo endapo atafanikiwa kuibuka mshindi.

“Kuna haja ya kuunganisha watu na viongozi wa Chadema katika mikoa mitatu kwa manufaa ya chama, nikishirikiana na timu ya viongozi wenzangu nimedhamiria kurejesha umoja wa kanda kwa manufaa ya chama chetu.” Amesema Matata.

“Kanda yetu ni kama imelala hakuna mikutano inayofanyika, sasa nakwenda kuamsha amsha endapo nitafanikiwa, ili kuongeza morali ndani ya chama.”

Mei 14, Kamati Kuu ya Chadema, iliwapitisha wagombea wote wanne wa Kanda ya Magharibi wanaowania uenyekiti. Ni kanda pekee ambayo wagombea uenyekiti wanne wamepitishwa.

Matata amesema hana hofu yoyote na ushindani utakaojitokeza akisema ndiyo demokrasia katika chaguzi.

“Wanachama wanafahamu wanataka nini, hivyo wana uamuzi wa kumchagua mtu atakayewasaidia kuipeleka kanda mbele zaidi, nimejidhatiti kutumia nguvu zangu zote kuiongoza kwa weledi na ufasini endapo nitafanikiwa kushinda Mei 29,”amesema Matata.

Matata atachuana na mawakili wenzake wawili Ngassa Mboje, Gaston Garubindi anayetetea kiti hicho na Mussa Martine. Nafasi ya umakamu wapo Massanja Katambi na Rhoda Kunchela.

Naye, Kunchela ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Katavi, amesema yupo vizuri ameshaanza kampeni tangu jana, baada ya majina yao kuwekwa hadharani.

Kunchela amesema ameshaanza kuzungukia wapigakura kwa njia mbalimbali zikiwamo za mitandao ya kijamii.

“Kuna njia nyingi za kuomba kura, unaweza kwenda moja kwa moja kuonana na wajumbe au ukatumia mitandao ya kijamii, cha msingi ni kujua wapigakura wako ni aina gani na wangapi wanatumia mitandao ya kijamii.

“Natumia njia zote ili kuwafikia wapiga kura, kwa hatua niliofikia hadi chama kuniamini sina mashaka nipo vizuri,” amesema Kunchela aliyewahi kuwa mbunge wa viti maalumu 2015/2020.

Kwa upande wake, Garubindi amesema kampeni zake zinatofautiana na washindani wake, akisema yeye anakwenda kwa wapiga kura kuwapa mrejesho wa mambo alioyahidi na kuyatekeleza katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake.

“Unapotetea nafasi kampeni zako lazima ziwe tofauti, sasa ninapokwenda kuzungumza na wapigakura jukumu namba moja ni kupeleka mrejesho wa mambo niliotekeleza, kama halijatekeleza kwa nini?

“Jambo la pili kuzungumza ulinzi na usalama wa chama na tatu namna nitakavyoivusha Chadema katika chaguzi zinazofuata za Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwaka 2025,” amesema Garubindi.

Kama ambavyo Mwananchi iliwahi kuandika, awali uchaguzi wa kanda Chadema, uliwagawa baadhi ya makada waliounda kambi zao za wagombea wanaowaunga mkono.

Hiki ndicho kinajitokeza hivi sasa kwa makada kuwapigia kampeni kwa kuambatanisha vipeperushi yenye picha zao katika mitandao ya kijamii bila kificho.

Miongoni mwa vipeperushi vinavyosambazwa na makada wa Chadema ni vya John Pambalu anayechuana na Ezekia Wenje katika kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ atakabiliana na Mchungaji Peter Msigwa kanda ya Nyasa.

Vipeperushi vingine ni vya Matata, vinavyosambazwa kwenye makundi ya WhatsApp na akaunti za X za makada hao kwa lengo kuwaombea kura, lakini wagombea husika wapo mstari wa mbele kuvisambaza.

Akizungumza na Mwananchi Digital Sugu ambaye ni mbunge wa zamani wa Mbeya Mjini, amesema wanaruhusiwa kuanza kampeni baada ya usaili kukamilika na hatua inayofuata kuwafikia wapigakura.

“Uchaguzi huu wapigakura wake sio wale wa umma, bali wapo ndani ya chama. Katika kanda yetu wapigakura hawazidi 120, nimeshaandaa njia za kuwafikia kama sehemu ya kuanza rasmi kampeni za kuomba au kuthibitisha,” amesema Sugu.

Chanzo: Mwananchi