Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wagombea CCM Manyara kujulikana Julai 12

11181 Ccm+pic TanzaniaWeb

Tue, 10 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Babati. CCM Mkoa wa Manyara, inatarajia kutangaza majina ya wagombea udiwani wa kata tano za mkoa huo watakaopeperusha bendera ya chama hicho Julai 12 kwenye uchaguzi mdogo unatarajiwa kufanyika Agosti 12 mwaka huu.

Katibu wa CCM mkoa wa Manyara, Pazza Mwamlima akizungumza leo alisema mchakato wa ngazi ya kata na wilaya umeshafanyika na kilichobaki ni kamati ya siasa ya chama hicho kupitia majina hayo na kutangaza majina ya madiwani hao.

Waliokuwa madiwani Mathayo Semhanda (ACT-Wazalendo) kata ya Gehandu na Marco Martin (Chadema) Kata ya Masakta wote wa halmashauri ya Wilaya ya Hanang' kisha wakajiuzulu na kujiunga na CCM walishindwa kwenye kura za maoni ili waweze kugombea kata zao kwa tiketi ya CCM.

Hata hivyo, waliokuwa madiwani kwa tiketi ya Chadema, Nicodemus Tlaghasi wa kata ya Bagara mjini Babati, Justin Masuja (Hayderer) na Paul Axweso (Tumati) wote wa halmashauri ya wilaya ya Mbulu waliojiunga na CCM wameshinda uchaguzi huo kwenye kura za maoni.

Katika uchaguzi wa kura ya maoni wa CCM uliofanyika juzi kata ya Gehandu, Semhanda alipata kura tisa huku mshindi akiwa John Darema aliyepata kura 28 na kata ya Masakta, Martin alipata kura tatu na mshindi akiwa Aloyce Mathias kura 35.

Katibu wa jumuiya ya wazazi wilaya ya Mbulu, Ester Joel alisema kata ya Hayderer, Justin Masuja alishinda kwa kura 69 aliyemfuata kura nne na kata ya Tumati, Paulo Axweso alishinda kwa kura zote 55.

Katibu wa CCM wa wilaya ya Babati mjini, Fauswali Dauda alisema aliyekuwa diwani wa kata ya Bagara kwa tiketi ya Chadema, Nicodemus Tlaghasi ambaye ajiuzulu na kujiunga na CCM ameshinda kura ya maoni.

Dauda alisema Tlaghasi alipata kura 57 na kumshinda aliyekuwa diwani wa kata hiyo mwaka 2010/2015 Andrew Ombay aliyepata kura 35 kati ya wajumbe halali 92 waliopiga kura katika kata hiyo.

Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Hanang' Mathew Darema alisema huo si mwisho wa uteuzi kwani wao wameshamaliza nafasi yao ila uteuzi rasmi wa wagombea udiwani utafanywa na CCM ngazi ya mkoa.

"Kushinda kwenye kura ya maoni si mwisho wa uteuzi, bado tunasubiria ngazi ya mkoa ambayo ndiyo itakayorudisha majina ya watakaopeperusha bendera ya CCM kwenye uchaguzi huo mdogo," alisema Darema.

Mkoa wa Manyara unatarajia kufanya uchaguzi mdogo wa madiwani Agosti 12 ili kuziba pengo la madiwani watano wa Chadema na ACT-Wazalendo waliojiuzulu wakidai kumuunga mkono mkuu wa mkoa huo Alexander Mnyeti na Rais John Magufuli.

Kwa mujibu wa taarifa ya uchaguzi mdogo iliyotolewa na tume ya Taifa ya uchaguzi, uteuzi wa wagombea utafanyika Julai 14 na kampeni ni kuanzia Julai 15 hadi Agosti 11 na uchaguzi utakuwa Agosti 12 mwaka huu.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz