Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wadhamini wamwandikia barua Mbowe kumtaka Lissu arejee Tanzania

92413 Pic+lissu Wadhamini wamwandikia barua Mbowe kumtaka Lissu arejee Tanzania

Mon, 20 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wadhamini wa aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu wameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam nchini Tanzania kuwa juhudi walizofanya kuhakikisha mshtakiwa anafika mahakamani ni pamoja na kumwandikia barua Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Mdhamini huyo Robert Katula amedai hayo leo Jumatatu Januari 20,2020 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba wakati kesi hiyo ilipotajwa.

Lissu ambaye anakabiliwa na kesi ya uchochezi yuko nchini Ubelgiji alikokwenda kwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi Septemba 7, 2017 akiwa kwenye makazi yake Area D jijini Dodoma akitoka kuhudhuria vikao vya Bunge.

Desemba 19, 2019 Mahakama hiyo ilitoa amri kwa wadhamini hao kuhakikisha mshtakiwa huyo anafika mahakamani.

"Tumefanya juhudi ya kuwasiliana na mshtakiwa akasema anawasiliana na wakili wa chama baada ya hapo akawa kimya, tukalazimika kumwandikia Mbowe barua kwa kuwa ndiye aliyemtoa nje ya nchi," amedai Katula

"Wakati natoa ahadi ya kuhakikisha mshtakiwa anafika mahakamani sikujua kama atapigwa risasi lakini juhudi tulizofanya ikiwa ni kuwasiliana na mwenyekiti wake zinaweza kuzaa matunda," amedai

Pia Soma

Advertisement
Mdhamini huyo amewasilisha nakala ya barua aliyomwandikia Mbowe na kudai akishafika nchini Tanzania anaweza kumleta mahakamani.

Wakili wa Serikali,  Silvia Mitanto ameeleza jukumu la mdhamini ni kuhakikisha mshtakiwa anafika mahakamani ni la mdhamini mwenyewe.

"Wadhamini hawa walikubali kumwekea dhamana na kuridhia kama ni kujitoa wangejitoa kabla mshtakiwa hajaenda nje ya nchi," amedai Mitanto

Hakimu Simba amewataka wadhamini hao kuhakikisha mshtakiwa analetwa mahakamani kabla mahakama hiyo haijatoa amri nyingine.

"Usifikiri tutakusamehe jukumu lako ndilo hilohilo mtuletee mshtakiwa kwa kuwa jalada hili halijui hofu, huo ndio mkataba wako," ameeleza Hakimu Simba

Baada ya maelezo hayo Hakimu  Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 20, 2020 itakapotajwa tena.

Lissu na wenzake watatu wanakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Mbali na Lissu ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Bara washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni  Mhariri wa Gazeti la Mawio, Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehbooh.

Kwa pamoja washtakiwa hao, wanakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati  Januari 12 na 14, 2016 jijini Dar es Salaam, ambapo Jabir, Mkina na Lissu, waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar.’

Katika shtaka la pili wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi.

Chanzo: mwananchi.co.tz