Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wadau washauri mbinu zaidi madai ya Katiba

KATIBAAAA Wadau washauri mbinu zaidi madai ya Katiba

Sun, 26 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Siku moja baada ya Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata) na Mtandao wa Madeni na Maendeleo Tanzania (TCDD), kutangaza kampeni ya kukusanya saini milioni tano ili kuunga mkono mchakato wa mabadiliko ya Katiba, baadhi ya wadau wameshauri njia zaidi za kuibua mchakato huo.

Akizungumza juzi jijini Dar es Salaam, mjumbe wa bodi ya TCDD, Dk Camillus Kassala alisema baada ya kukusanya saini hizo watazipeleka Ikulu za Dar es Salaam na Chamwino Dodoma ili kufikisha ujumbe kwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Mbali na Rais Samia ambaye tangu awali alishaweka msimamo wa kutaka aachwe kwanza asimamishe uchumi kabla ya kujadili mchakato huo, hata viongozi wa CCM kwa nyakati tofauti nao wameshaeleza kutokuwa na dhamira ya kuendelezwa kwa mchakato huo kwa sasa.

Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 11 mwaka huu jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo alihoji;

“Wapi umeona wananchi wamebeba mabango wanataka Katiba mpya? Tuambiane ukweli? Zaidi ya sisi wanasiasa? Na sisi wanasiasa kwenye Katiba tunataka mambo makubwa mawili matatu; kwanza tume huru ya uchaguzi, niambie mwananchi tume ile inampelekea unga? Inampelekea ugali?’ alihoji Chongolo.

Lakini akizungumza jana kwa simu na Mwananchi, Katibu Mkuu wa Chadema John Mnyika, mbali ya kuunga mkono mkakati wa kukusanya saini za wananchi wanaounga mkono mchakato huo, alitahadharisha kuwa unaweza kuchelewesha kufikia lengo.

“Mkakati wa kukusanya saini sio jambo baya hata hivyo mkakati huo usitumike kama kisingizio cha kuchelewesha kuendeleza kazi ya mchakato wa katiba mpya kuendelea.

Wadau na mbinu zaidi

Kwa mujibu wa Mnyika, mbali ya kusubiri saini hizo, alishauri kila mmoja kwa njia mbalimbali aendelee kumshawishi Rais Samia Suluhu kupitia hotuba yake kwa Taifa ya kuuaga mwaka 2021 na kuukaribisha mwaka 2022, atangaze kuendeleza mradi na kazi ya Katiba mpya.

“Kaulimbiu yake ya kazi Iendelee iende sambamba na kauli mbiu ya Kazi ya Katiba mpya iendelee,” alisema Mnyika.

Alisema mkakati huo wa kumshawishi Rais kubadili kauli yake ya awali na kufungua ukurasa mpya wa Katiba mpya uhusishe pia viongozi wa dini katika mahubiri yao ya sikukuu ya Krismasi.

“Ni vyema Rais na wadau wote wakakumbuka kuwa kimsingi saini za wananchi zilishakusanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji (Joseph) Warioba kupitia mikutano na maoni yaliyotolewa Tume ilipozunguka maeneo mbalimbali nchini, alisema.

Kwa upande wake, wakili Jebra Kambole, alishauri kufanyika kwa ushawishi kwa mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao nchini, ili nao wawashawishi viongozi wa Serikali kuhusu mchakato huo.

‘‘ Inawezekana kuwashawishi mabalozi, kwa sababu wao ndio wanaotoa fedha za miradi ya maendeleo, waone namna Watanzania wanavyotaka Katiba mpya,’’ alieleza.

Naye, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa, aliunga mkono mkakati wa kukusanya saini akisema taasisi zilizoanzisha zina haki ya kufanya hivyo.

“Kwanza mchakato wa Katiba ulifikia hatua nzuri kuumalizia, kwa hiyo kwa kutumia nafasi hiyo tunaona kwamba ni jambo jema sana na viongozi wanatakiwa kutoa majibu ya kuridhisha kwa wananchi,” alisema.

ACT wasisitiza tume huru ya uchaguzi

Kwa upande mwingine, chama cha ACT-Wazalendo kimeendelea na kampeni yake ya kukusanya maoni ya wanachama wake kuhusu tume huru ya uchaguzi inayopigiwa chapuo na chama hicho.

Taarifa iliyotolewa juzi na Naibu Katibu wa Habari na Uenezi na Uhusiano wa Umma, Janeth Rithe ilimnukuu Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu aliyekuwa kwenye ziara mkoani Ruvuma, akisisitiza kuhusu madai ya tume hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live