Uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi kusitisha kwa muda usajili wa vyama vipya ili kupisha uhakiki wa vilivyopo umewaibua wadau, wakimtaka kutumia busara katika uamuzi huo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam jana baada ya kikao kazi kilichoandaliwa na msajili kutoa elimu kuelekea uhakiki wa vyama vilivyopo unaotarajiwa kuanza Julai 20, mwaka huu, walisema mpango huo unawashangaza, ikizingatiwa tangu mwaka 2014 hakuna chama kipya kilichopata usajili.
Juzi, Jaji Mutungi wakati anafungua kikao hicho cha viongozi wa vyama vya siasa, alisema usajili wa vyama vipya 18 utafanyika baada ya kumalizika uhakiki na wanapaswa kusubiri kwa kuwa hautachukua muda mrefu.
“Itashangaza sana kuanza usajili wa vyama vipya kabla ya kufanya uhakiki wa vilivyopo kama viko safi; vipya 18 vinapaswa kusubiri hadi kazi hii iishe tutavisajili wala hatujakataa kuvisajili,” alisema Jaji Mutungi.
Pia, alisema wanaohitaji usajili wa vyama vipya waache kuwa na woga na taharuki na kuwataka waamini taasisi inayowasimamia haitamkatili wala kumuonea mtu.
Kufuatia kauli hiyo, Mwananchi lilizungumza na msajili mstaafu, John Tendwa ambaye alisema msajili anapaswa kutumia busara katika kutoa uamuzi juu ya hilo.
Alisema ni kipindi kirefu kimepita umma haujaona wala kusikia usajili wa muda au wa kudumu kwa chama chochote ukifanyika, jambo linalofikirisha.
Hata hivyo, aliwataka walioomba kusajili vyama vyao wawe na subira, inawezekana ofisi ya msajili imezidiwa na majukumu lakini italitekeleza hilo.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie alisema kitendo hicho kinaminya haki ya msingi ya mfumo wa vyama vingi na watu kujumuika, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.
“Kwa sababu watu wakiomba usajili wanaangalia vigezo na ili chama kisajiliwe, lazima kiwe na hoja kadhaa, kama wamekidhi matakwa kwa nini wasisajiliwe? Nafikiri angeangalia vigezo badala ya kuendela kuminya haki za watu,” alisema Dk Loisulie.
Awali, Makamu Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo, Dorothy Semu alisema demokrasia lazima iwe na mwendelezo, kila wakati inatakiwa kuwe na vyama vipya vinavyosajiliwa, vinavyotoka kwenye mfumo na vinavyoungana.
“Kazi ya usajili lazima iwe endelevu na si kusubiri na tukumbuke tangu kusajiliwa kwa ACT Wazalendo, hakuna chama kingine kilichosajiliwa, naamini kuna kundi la watu limekuja na mawazo mengine wapewe fursa,” alisema.
Mwenyekiti wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Hamad Rashid Mohamed alidai kuwa msajili hana mamlaka ya kuzuia usajili labda kama hatakuwa na rasilimali fedha.
“Suala la kusema usajili utaendelea baada ya uhakiki hilo si sahihi, labda kama hana watendaji wa kutosha kwa sababu kusajili chama lazima kifanyiwe uhakiki vilevile,” alisema.
Alisema masharti ya kuanzia mikoa 10 kuwa na wanachama kuanzia 200 kwa Tanzania bara na visiwani ni changamoto, ikizingatiwa na jiografia ya nchi ya gharama kufikia maeneo.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba alikuwa na mtazamo tofauti na wengine, akidai kinachofanywa na msajili ni sahihi kwa kuwa nchi bado ina vyama vingi na wenye mawazo mseto wachague kwa kwenda.
“Nchi ina vyama vingi na sioni kama kuna haja ya kuendelea kusajili vyama vingine, wakati vilivyopo bado vinahitaji watu na nafasi zipo isipokuwa wanapaswa kuangali wakajiunge na chama kipi kitakachoendana na falsafa wanazotaka,” alisema.
Mwanzilishi wa chama tarajiwa cha Independent People’s Party (IPP), Andrew Bomani alisema kutokana na msimamo wa msajili huyo wana mpango wa kutoa tamko kupinga utaratibu huo.
“Tunaandaa tamko linalolenga kupinga msimamo wake, tunamshangaa, haiwezekani aseme anasubiri kwanza uhakiki wa vyama vilivyopo wakati kazi yake ya msingi ni kusajili vyama,” alisema.
Bomani alisema barua ya kuomba usajili katika ofisi hiyo waliiwasilisha tangu Mei mwaka huu, kwa kipindi chote hajaweka tangazo kwenye magazeti hata vyama vingine anavyodai vimeomba usajili.