Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wadau wamshukia Polepole kwa kauli yake

21923 Polepole+pic TanzaniaWeb

Fri, 12 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kauli iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM katika mtandao wa Twitter juu ya viongozi wa upinzani wanaotaka kuhamia chama hicho tawala kufanya haraka kabla ya Desemba, imeibua maswali na majibu kutoka kwa wananchi.

Polepole aliandika hivi karibuni katika ukurasa wake wa mtandao huo kuwa, wabunge wa upinzani wanaotaka kuhamia CCM mwisho wa kufanya hivyo ni Desemba 2018.

Aliandika, “Tumezingatia na tunaweka jitihada zetu zote katika kushughulika na utatuzi wa shida za watu wetu wa Tanzania. Mwaka 2018 ndio mwisho kwetu kufanya chaguzi ndogo za ubunge kwa wale wanaohama vyama vyao na kujiunga na CCM. Watakaoikosa round hii mbaki hukohuko tutakutana 2020.”

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kuhusu kauli hiyo, baadhi ya watu wamehoji sababu zilizomfanya kiongozi huyo kuweka muda wa kikomo kwa wabunge na madiwani wa upinzani wanaohama kwa madai ya kuunga mkono jitihada za Rais John Magufuli.

Salim Zige maarufu ‘Mzee Zig’ anayeishi jijini Dar es Salaam alisema kama kuna sababu nyingine ya kuhama upinzani, ukomo uliotangazwa haupaswi kuwapo.

“Kama kweli kuna nia ya dhati ya kuunga mkono jitihada za Rais Magufuli tuone baada ya ukomo wa chaguzi za marudio wataendelea kuhama? Kauli ya Polepole ni ya kisiasa au ni kwa sababu uchaguzi utakuwa haurudiwi,” alisema.

“Mfano huyu wa juzi (James Ole Millya-aliyekuwa mbunge wa Simanjiro-Chadema), alijua wazi akihama baada ya Desemba hatapata ubunge, kwa hiyo ameingia chama tawala anataka tena ubunge na atapata.”

Zige alisema wananchi wanaamini kuwa hamahama ya wabunge na madiwani itakwisha uchaguzi utakapofika.

Soma zaidi>Polepole: Wabunge wanaotaka kuhamia CCM mwisho Desemba 2018

Mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam, Asia Japhet alisema kama wabunge wote nchini watatokana na CCM, hakuna sababu ya kuwa na mfumo wa vyama vingi.

Naye Japhet Kanyika alisema Polepole yuko sahihi kulingana na malengo ya chama chao waliyojiwekea.

Hoja hiyo ya Polepole imemuibua kwa mara nyingine mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu ambaye amehoji uhalali wa hamahama hiyo.

“Katibu mwenezi wa CCM, Polepole amesema mwisho wa kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli za kuwaletea wananchi maendeleo ni Desemba 2018. Kwa nini zuio hilo la CCM linalingana ama kukaribiana na zuio la kikatiba na kisheria kwa chaguzi za marudio,” alihoji Lissu.

“Je, hii ni bahati mbaya tu au kuna njama iliyofichwa kwenye hii ratiba ya CCM na ratiba iliyowekwa na Katiba na sheria za uchaguzi?”

Lissu alisema, “kwani kujiuzulu ubunge au udiwani wa Chadema na baadaye kugombea nafasi zilezile kwa CCM ni njia pekee ya kumuunga mkono Magufuli? Kumbuka, John Shibuda wa Chadema na John Cheyo wa UDP walikuwa wakiunga mkono jitihada za Rais Kikwete lakini hawakuwahi kujiuzulu ubunge au uanachama wa vyama vyao.”

Mkazi wa Kinondoni, Sadik Malik alisema Polepole anawaita wabunge wengi wa upinzani kujiunga na chama hicho kabla ya mwaka haujaisha.

Alisema si ajabu wabunge na madiwani wengi wakajitokeza kuhamia CCM kama alivyohimiza.

“Chadema wamesema hawatashiriki chaguzi ndogo, sasa na CCM wakisitisha upokeaji wa wanaohama basi kutakuwa hakuna chaguzi ndogo. Mimi naona ni jambo jema kwa sababu tumechoka na hizi chaguzi,” alisema.

Fred Chito kutoka Kimara alisema CCM ndiyo wanaamua cha kufanya kwenye siasa za nchi hii kwa sababu wanamiliki dola.

Mbeya

Baadhi ya wananchi jijini Mbeya walisema hawaoni sababu za kuwa na kikomo cha madiwani na wabunge wa upinzani kuhama kwa madai ya kuunga mkono jitihada za Rais Magufuli.

Mkazi wa Uzunguni, Fred Aron alisema nchi haiwezi kwenda bila kanuni na sheria kwa sababu zilitungwa kwa ajili ya kutekelezwa.

“Sijajua Polepole katoa hiyo kauli ili iweje, kwa sababu sheria za nchi zipo wazi na kila mtu ana haki ya kuhama chama chake kwa muda anaotaka badala ya kupangiwa,” alisema Aron.

Issah Shomari alisema, “kauli ya Polepole kaitoa kutokana na utashi wake, hakuna sehemu yoyote kwenye katiba ya CCM wala ya nchi ulipowekwa ukomo mpinzani kukihama chama chake. Ni vyema viongozi wakatathmini kauli zao kabla ya kuzitoa hasa za masuala ya siasa.”

Mkazi wa kwa Mama John, Ibrahim Abdallah alisema Polepole amekurupuka.

“Akumbuke kuwa mtu kujiunga na chama ni haki yake wakati wowote akitaka anaweza kuhama,” alisema Abdallah.

John Biku, mkazi wa Ilomba alisema ni kawaida kwa viongozi wa Kiafrika kutoa matamko.

“Ni kawaida kwetu kusikia hayo japo naona hili ni tamko la kisiasa tu,” alisema.

Moshi

Baadhi ya wakazi wa Moshi walisema kauli hiyo inaashiria kuminywa kwa demokrasia.

Gadson Sadick alisema inaonyesha kuwapo kwa mpango uliokuwa ukiendelea wa kuwarubuni viongozi wa upinzani na ifikapo Desemba utakuwa umesitishwa.

Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema alisema, “ninamshukuru Polepole kwa kusema ukweli kuwa mpango wao wa kununua makada wa upinzani umekoma.”

Mwanza

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi jijini Mwanza walikuwa na mitazamo tofauti huku wengine wakiunga mkono wimbi la wabunge na madiwani kutoka vyama vya upinzani kuhamia CCM.

Walisema ni haki ya kila mtu kikatiba na kisheria kuhamia chama akitakacho, huku wengine wakipinga kwa madai kuwa uamuzi huo unateketeza mabilioni ya fedha za umma zinazotumika kwenye chaguzi ndogo.

Mmoja wa viongozi wa Chadema Kanda ya Ziwa, Tungaraza Jungu alisema kauli ya Polepole imedhihirisha uhalisia wa hila zinazofanyika kuwarubuni viongozi wa upinzani.

“Polepole na chama chake (CCM), wamekosa hoja ya kukijenga chao ndiyo maana wameamua kuwekeza katika kuwakurubuni wabunge na madiwani wa upinzani kwa ahadi ya vyeo vya kuteuliwa au kusimamishwa kuwania nafasi wanazojiuzulu na kuhakikisha wanashinda hata kama wapiga kura wamewakataa,” alisema Jungu.

Alimtaka Polepole na viongozi wengine wa chama hicho tawala kuelekeza nguvu kwenye kuisimamia Serikali kuongoza kwa kufuata Katiba na sheria ikiwemo kuruhusu mikutano ya kisiasa.

“Kama kweli CCM wanadhani wanakubalika kwa wananchi, basi waielekeze Serikali kuruhusu shughuli za kisiasa ili twende kwa wananchi kunadi na kushindanisha sera,” alisema Jungu.

Aliongeza kuwa, “hawawezi (CCM) kutamba eti wanakubalika wakati wamevizuia vyama vingine kufanya siasa huku wao wakitumia mikutano ya viongozi wa kitaifa, mikoa na wilaya kufanya siasa.”

Mkazi wa mtaa wa Mulungushi, Cresta Titus alisema ilikuwa sahihi kwa Polepole kuwapa muda wanaotaka kuhamia CCM ili kutoa fursa kwa chaguzi ndogo kufanyika na kumalizika kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika 2019.

Akizungumzia kauli hiyo, mkazi wa Igogo, Albinius Sosopi alisema anachofanya Polepole ni kuwaharakisha wabunge na madiwani wa upinzani wenye nia ya kuhamia CCM wafanye hivyo haraka.

Kwa upande wake, Cecy Juma, mkazi wa Nyakato alisema huenda kauli ya Polepole inawalenga baadhi ya wanasiasa wa upinzani wanaoonyesha nia au waliofanya majadiliano ya kuhamia CCM, lakini wanasita.

Arusha.

Akizungumza na Mwananchi mjini Arusha, mratibu wa Mtandao wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali mkoani humo (Angonet), John Bayo na mkurugenzi wa Haki za Binadamu wa CUF mkoani Arusha, Abdalah Shaban walisema kinachopaswa kufuatwa ni sheria na si tamko au kauli ya mtu mmoja.

Shaban alisema wanaohama vyama wanasema wanaunga mkono jitihada za Rais Magufuli na kama ni kweli hakupaswi kuwa na ukomo.

“Waendelee na mchezo wao, Polepole siyo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuna sheria kuhusu marudio ya uchaguzi,” alisema Shaban.

Bayo alisema wanaohama vyama wanazingatia haki yao kidemokrasia, lakini kuwawekea ukomo si sahihi, isipokuwa wanapaswa kuwaaga waliowachagua.

John Laizer aliiomba NEC kutoa kauli juu ya tamko la Polepole. Hata hivyo hakufafanua nini inachopaswa kuzungumzia.

Imeandikwa na Tumaini Msowoya, Cledo Michael (Dar es Salaam); Florah Temba na Maryasumta Eusebi (Kilimanjaro); Ipyana Samson na Yonathan Kossama (Mbeya) na Mussa Juma (Arusha)

Chanzo: mwananchi.co.tz