Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wachache wajitokeza kupiga kura Dar, maoni tofauti yatolewa

85636 Pic+uchaguzi Wachache wajitokeza kupiga kura Dar, maoni tofauti yatolewa

Sun, 24 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati mwenendo wa watu kujitokeza kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa nchini Tanzania ukionekana kusuasua, baadhi ya wananchi wamesema sintofahamu iliyojitokeza katika mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu hadi uteuzi wa wagombea ndiyo imechangia hali hiyo.

Mchakato wa uchukuaji wa urejeshaji wa fomu za uteuzi ulikumbwa na sintofahamu baada ya wagombea wa vyama vya upinzani kujikuta wakizikosa na hata wale waliofanikiwa kuzipata walikwama kuzirejesha baada ya kukuta ofisi za serikali zikiwa zimefungwa.

Kitendo hicho, kililalamikiwa na viongozi wa vyama vya upinzani ambao  waliitaka Serikali ya Tanzania kuchukua hatua madhubuti ili kunusuru hali hiyo ya wagombea wao kushindwa kuchukua na kurejesha fomu za uchaguzi wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji.

Hata hivyo, baadhi ya vyama vya upinzani vya CUF, Chadema, NCCR- Mageuzi, ACT- Wazalendo na Chaumma vilitangaza kujitoa katika mchakato wakidai kutoridhishwa na mwenendo wake hasa baada ya asilimia kubwa ya wagombea wao kuenguliwa kwa kukosa sifa.

Uchaguzi wa Serikali za mitaa kwa mkoa wa Dar es Salaam, unafanyika katika mitaa miwili ukiwemo wa Muhalitani Tandale huku katika eneo la Buguruni mchakato huo ulifanyika mtaa wa Malapa kwa nafasi ya wajumbe pekee.

Mwananchi leo Jumapili Novemba 24, 2019  lilifika katika mojawapo ya kituo cha kupigia cha kura cha Machuchuni kilichopo mtaa wa Buguruni Malapa na kukuta mchakato wa upigaji kura ukiendelea huku idadi ya watu ikiwa ndogo.

Ismail Matola mmoja wa wakazi wa mtaa wa Malapa, akizungumza na Mwananchi baada ya kupiga kura amesema mwamko mdogo katika mchakato huo tofauti na chaguzi nyingine za huko nyuma.

"Nadhani watu wameshindwa kujitokeza kwa sababu hawakuridhishwa na namna mwenendo wake ulivyokuwa kuanzia uchukuaji na urejeshaji wa fomu za uteuzi. Serikali ijipange vyema kwenye chaguzi zijazo kuhakikisha zinakuwa na usawa," amesema Matola

Kwa upande wake, Hamis Bakari amesema idadi ya watu kujitokeza katika mchakato huo itakuwa ya kusuasua kwa namna mwenendo wa uchaguzi huo ulivyokuwa ikilinganisha na chaguzi zilizipita.

"Sijapenda mwenendo wa  mchakato huu ulivyokuwa ndio maana siwezi kushiriki upigaji wa kura. Mfano hapa Mtaa wa Malapa wanaogombea nafasi za ujumbe tu na vyama vinavyoshindana ni CCM na ADC, niende nikafanye nini,” alihoji

Wakati Bakari akieleza hayo, Said Bashari alikuwa na mawazo tofauti akisema mchakato unakwenda vizuri na watu watajitokeza kwa wingi kupiga kura kilichowakwamisha ni hali ya hewa ya mvua.

"Mchakato unakwenda vyema na ukifika kituo hauchukui dakika 10 umeshamaliza kupiga kura kwa namna walivyojipanga wahusika. Pia, tunashukuru jeshi la polisi kwa kuimarisha ulinzi," amesema Bashari.

Bashari amegusia suala la vyama kujitoa akisema hawajatendekea haki wanachama wao waliotaka kugombea na kupigiwa kura katika nafasi mbalimbali za uchaguzi huo.

Naye Fatuma Omary amesema ameridhika na namna uchaguzi huo unavyokwenda akisema ushindani utakuwepo kwa wagombea wa  nafasi za ujumbe wa mtaa wa Malapa kwa sababu wanajuana.

Hata hivyo, mtaa wa Muhalitani  mgombea wa  nafasi ya uenyekiti mtaa huo, kwa tiketi ya CCM Said Makamba amesema Novemba 18, 2019 alipewa barua na msimamizi msaidizi wa uchaguzi ikimtaarifu kuwa amepita bila kupingwa yeye na wajumbe wake.

"Nilipozindua kampeni Novemba 17,2019 kesho yake nikapewa barua ya kuambiwa nimeteuliwa baada ya washindani wa vyama vya CUF, Chadema na ACT- Wazalendo kujitoa. Sasa hivi nipo nyumbani nasubiri kuapishwa tu," amesema Makamba.

Chanzo: mwananchi.co.tz