Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunge watofautiana utaratibu mpya wa kupitisha bajeti bungeni

102463 Wabunge+pic Wabunge watofautiana utaratibu mpya wa kupitisha bajeti bungeni

Tue, 14 Apr 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Wabunge wametoa maoni tofauti kuhusu utaratibu mpya wa kupitisha bajeti bila ya kupitia vifungu, ambao umeanza kutumika katika mkutano wa bajeti unaoendelea jijini Dodoma.

Utaratibu huo wa upitishaji bajeti wa kutojadili kifungu kwa kifungu umeondoa haki ya mbunge kushika shilingi ya mshahara wa waziri kama njia ya kuzuia bajeti pale inapotokea hajaridhika na maelezo.

Badala yake sasa wabunge wanapitisha bajeti kwa kupiga kura kwa njia ya mtandao.

Mabadiliko hayo ni miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na Bunge kama njia ya kujikinga na mlipuko wa virusi vya corona, ambao pia umepunguza muda wa vikao hadi saa nne kila siku, kuanzia saa 8:00 mchana huku wabunge wakikaa katika kumbi tofauti.

Utaratibu mpya ulianza kutumika wakati wa kupitisha bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa wabunge kupiga kura kwa njia ya mtandao wakati mawaziri wakiendelea kujibu hoja zilizochangiwa.

Awali katika mikutano ya bajeti iliyotangulia, wabunge walipitisha kifungu kwa kifungu cha bajeti na katika baadhi ya hoja ama vifungu, mara nyingi ilitokea mivutano mikali na hasa baina ya mawaziri na wabunge.

Pia Soma

Advertisement
Akizungumzia suala hilo, mbunge wa Kinondoni (CCM), Maulid Mtulia alisema hayo ni madhara yanayotokana na dharura iliyosababishwa na hatua zilizochukuliwa kujikinga na ugonjwa wa corona.

“Una madhara huwezi kusema kuwa una faida. Madhara haya yanatokana na dharura ya hali ya tahadhari ya Covid-19. Lakini, utaratibu huo unafanywa kwa faida ya kulinda afya za wabunge. Tuvumiliane, tukubaliane na hali,” alisema.

Hata hivyo, Mtulia alisema bado wabunge wanayo nafasi ya kutoa maamuzi yao kwa kutumia kura zao iwapo wanaona bajeti haifai.

Alisema japokuwa baadhi ya wabunge watakosa fursa ya ufafanuzi, lakini kwa masilahi mapana ya nchi ni lazima kwa mazingira yoyote ile mkutano huo ufanyike.

Naye mbunge wa viti maalum (Chadema), Upendo Peneza alisema utaratibu huo mpya unaondoa mijadala na uwajibikaji wa mawaziri katika masuala mbalimbali ambayo wabunge hawakuridhika wakati mawaziri wakihitimisha hoja zao.

“Lakini, kinachofanyika hivi sasa wakati mawaziri wanajibu hoja wabunge wanaendelea kupiga kura, kwa hiyo hamna maana ya kushika shilingi tena. Utaratibu unakuwa umepotea kwa sababu ya utaratibu uliowekwa wa kujikinga na corona unaowafanya wabunge kukaa muda mchache bungeni,” alisema. Alishauri Bunge lipunguze uchangiaji na kuwapa nafasi wabunge kusikilizwa hoja zao wakati wa upitishaji wa bajeti kwa sababu huko nyuma imeonyesha mafanikio makubwa.

“Mfano kuna wabunge walishika shilingi ya mshahara wa waziri kwa kutaka majibu kuhusu wavuvi waliokamatwa katika operesheni zilizokuwa zinaendeshwa Ziwa Victoria hadi Serikali ilipotoa majibu katika suala hilo, nafasi ambayo haipo tena katika Bunge hili,” alisema.

Mbunge wa Malindi (CUF), Ally Saleh alidai kushangazwa kupitisha bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

“Juzi jina langu lilikuwa ni miongoni mwa wabunge ambao tulikuwa tuulize kuhusu mambo ya sera. Nilitaka kufahamu msimamo wa Serikali kuhusu suala la Tume Huru ya Uchaguzi. Ninafahamu Chadema na CCM nao walipeleka majina ya wabunge hao waliotaka kuhoji katika fungu hilo,” alisema.

Leo Bunge linaendelea na vikao vyake na bajeti ya Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais- Tamisemi itahitimishwa kwa kupigiwa kura.

Tamisemi imeomba kupitishiwa Sh7.02 trilioni kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo.

Chanzo: mwananchi.co.tz