Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunge watano waliong’ara mkutano wa 12 wa Bunge mjini Dodoma

17612 Pic+wabunge TanzaniaWeb

Mon, 17 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Wabunge watano waling’ara katika mkutano wa 12 wa Bunge uliomalizika wiki hii mjini Dodoma kutokana na hoja walizozisimamia kukitikisa chombo hicho cha kutunga sheria.

Miongoni mwa hoja zilizotikisa ni ile iliyosababisha kukwama kwa mara ya kwanza kwa Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali namba 2 wa mwaka 2018 tangu Bunge la 11 lianze.

Mkutano wa 12 ulianza Septemba 4 na kumalizika Septemba 14, huku miswada mitano ikijadiliwa na kupitishwa. Miswada hiyo ni ule wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali namba 2 na 3; wa Sheria ya Kulitangaza Jiji la Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi; wa Marekebisho ya Sheria ya Ubia wa Sekta ya Umma na Binafsi na Muswada wa Bodi ya Kitaalamu ya Walimu.

Hata hivyo wakati wa kipindi hicho cha Bunge wabunge watano walionekana hoja zao kutikisa mkutano huo ambao ni Halima Mdee (Kawe-Chadema); Saada Mkuya (Welezo-CCM); George Lubeleje (Mpwapwa-CCM); Khatib Said Haji (Konde –CUF) na Suzan Lyimo (viti maalumu-Chadema).

Mdee alitoa hoja ya utaratibu akitumia kanuni ya 77 ya Bunge alipozungumzia akidi ya wabunge waliotakiwa kufanya uamuzi kuhusu Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali kuwa haikutumia.

Hoja hiyo ilifanya muswada huo kukwama baada ya kushindwa kutimia kwa akidi hiyo hata pale uongozi wa Bunge ulipopiga kengele kuwataka wabunge waliokuwa nje ya ukumbi kuingia ndani ili kufanya uamuzi.

Kukwama huko kunaifanya hoja hoja hiyo kuwa ya kwanza kushindwa kutolewa uamuzi kama ilivyokusudiwa awali kwa sababu ya kutotimia kwa akidi tangu Bunge la 11 lianze Novemba 2015.

Awali akichangia Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) wa mwaka 2018, Mdee alisema kuwepo kwa kifungu kinachotaka migogoro inayotokana na miradi ya ubia kutatuliwa nchini kitawafukuza wawekezaji makini wa nje kuja nchini.

Alisema utaratibu wa kutumia mahakama za ndani pekee utawafukuza wawekezaji hasa kwa kuzingatia kuwa watatumia fedha zao wenyewe kwa asilimia 100.

Hoja hiyo ilizua mvutano kati ya Serikali ambayo ilitaka marekebisho hayo yabaki kama ilivyopendekeza huku kambi ya upinzani ikitaka kuondolewa kwa marekebisho ya kifungu hicho ili wawekezaji waweze kutumia mahakama za nje na za ndani.

Lubeleje na sukari

Akiomba mwongozo bungeni, mbunge wa Mpwapwa, Lubeleje aliihoji Serikali kwa nini wananchi wanaendelea kusumbuka kutokana na bei ya sukari kuwa juu nchini wakati bidhaa hiyo imejaa katika maghala viwandani.

Lubeleje alisema sukari inauzwa kati ya Sh2,600 hadi Sh3,000, lakini imejaa katika maghala ya viwanda vinavyoizalisha na kuhoji kwa nini watu waendelee kusumbuka kuinunua kwa bei hiyo badala ya Sh2,000. Hoja hiyo iliilazimu Serikali kutoa kauli kuhusu hali ya sukari nchini baada ya kufanya tathmini ikisema bidhaa hiyo inapatikana katika maeneo yote nchini.

Mkuya na kilio cha umeme

Akichangia Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali namba 3 wa mwaka 2018, mbunge wa Welezo, Mkuya alisema alitegemea suala la umeme unaokwenda Zanzibar kutozwa kodi ya ongezeko la thamani (Vat), lingekuwepo katika marekebisho hayo kama ilivyoahidiwa na Serikali katika mkutano uliopita wa Bunge.

Pia alilalamikia kuzuiwa nje ya jengo la Bunge kwa wawakilishi wa Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco), waliofika Dodoma kujadili suala hilo na Serikali.

Mkuya alinukuu maneno ya waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu, Jenista Mhagama yaliyopo kwenye taarifa rasmi za Bunge (hansard) kuwa sheria zinatakiwa kufanyiwa kazi ili kuliweka jambo hilo sawa na kwamba katika mkutano wa 12 liwe limemalizika.

“Mheshimiwa spika tuende wapi? Tuseme wapi? Hakuna hata taarifa ya kusema kuwa haya mambo yanaendelea. Mimi sikuwa na hoja naungana na Serikali kuhusu muswada, lakini nimekuwa disappointed (nimefadhaika) kuona marekebisho ya sheria ya Vat ama maelezo yake hayamo kama ilivyoahidiwa na Serikali.

Khatib na makontena

Mbunge wa Konde (CUF), Khatib alimpongeza waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alivyosimamia suala la kodi ya makontena ya mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda. Khatib alimtaka Dk Mpango aendelee kumbana hadi haki ipatikane akisema, “alizoea kukutana na vingine sasa amekutana cheusi kimemtia doa..Rais (John Magufuli anapenda viongozi kama hao- ).” Alisema mbunge huyo akimaanisha Rais anapenda viongozi wanaosimamia sheria.

Lyimo na walimu

Akichangia Muswada wa Bodi ya Kitaalamu ya Walimu, mbunge wa viti maalumu, Lyimo aliwasilisha marekebisho ambapo pamoja na mambo mengine Serikali ilikubali uteuzi wa mwenyekiti wa bodi kufanywa na Rais badala ya waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia; kuweka uwakilishi wa sekta binafsi katika bodi na waziri mwenye dhamana kuwa na mamlaka ya kuongeza sifa za usajili na uteuzi wa wajumbe wa bodi kutozingatia uwakilishi wa shule binafsi.

Chanzo: mwananchi.co.tz