TANZANIA itafanikiwa kufikia uchumi wa viwanda kama itaweka mkazo wa kimkakati katika kuboresha na kuimarisha mnyororo wa thamani ya mazao kutoka shambani hadi viwandani.
Mnyororo huo unataka serikali ijikite katika kuhamasisha wananchi kutumia teknolojia katika kuzalisha mazao hasa ya mafuta, kuboresha miundombinu ya kusafirisha mazao toka shambani hadi sokoni na kujenga viwanda vya kuchakata karibu na wakulima ili kuuza mazao yaliyoongezwa thamani ndani na nje ya nchi.
Wakichangia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa miaka mitano 2021/22-2025/26 Bungeni walisema, hakuna maendeleo ya kiuchumi kama sekta msingi hizo hazitapewa msukumo wa kutosha.
Mbunge wa Kasulu Mjini, Augustine Hole (CCM) alisema serikali imehiza wananchi kulima mazao ya kuzalisha mafuta ikiwemo Kigoma, kulima michikichi, kinachotakiwa ni kupeleka viwanda vya kuchakata mafuta hayo.
Hole alisema hivi sasa mafuta yatokanayo na michikichi ni mekundu, inatakiwa kupeleka mashine za kuyasafisha ili kuwa katika ubora zaidi.
Alisema michikichi ni alama ya Kigoma hivyo himizo la serikali kwamba walime na wananchi wameitikia, kinachotakiwa ni kupeleka teknolojia ya kuboresha na kutumika kupunguza ombwe la mafuta nchini ambalo linafanya kuagiza nje ya nchi tani 365,000 kati ya mahitaji ya tani 570000 kutokana na kuzalisha tani 205,000 tu.
Hole alisema teknolojia ya viwanda vya kusafisha mawese vitasaidia kupandisha bei ya mafuta hayo ambayo sasa yanauzwa kwa Sh 10,000 kwa debe wakati alizeti iliyochujwa inauzwa Sh 35,000 kwa debe hilo hilo.
Mbunge wa Busega, Simon Lusengekile (CCM) alisema uzalishaji wa mazao kama pamba utafanikiwa kuchangia kuondoa ombwe la mafuta nchini kama miundombinu ya barabara itakuwa imeboreshwa ili kutoa mazao shambani na kufikisha kwenye viwanda vya kuchakata na kuzalisha mafuta.
Lusengekile alisema uwekezaji mkubwa unatakiwa katika kuboresha barabara ambazo zitachangia kusomba pamba kutoka shambani kupeleka kwenye viwanda na kuwa kutokana na mkoa wa Simiyu kuwa maarufu wa kuzalisha pamba, ilitakiwa serikali kujenga kiwanda cha kutengeneza vifaa tiba, dawa na viuatilifu ili kupunguza gharama za serikali kutumia zaidi ya Sh bilioni 147 kwa mwaka kuagiza viuatilifu nje ya nchi.
Alisema kiwanda hicho kitasaidia kutengeneza magozi ya pamba, mashuka, mablanketi, nguo za madaktari na wauguzi hapo Simiyu badala ya kuagiza nje ya nchi.
Mbunge wa Mbulu Vijiini, Flatey Massey (CCM) alisema uwekezaji unatakiwa kwenye sekta ya kilimo ambayo Watanzania zaidi ya asilimia 70 wapo huko ili pia kuongeza mchango wa sekta hiyo katika pato la taifa ambapo inachangia asilimia tatu tu.