Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunge wataka jeshi lisitumike uchaguzi mkuu

Thu, 7 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WABUNGE wamelitaka jeshi kutokubali kutumika wakati wa Uchaguzi Mkuu, kutoa fedha za utafiti wa corona, kuongeza mishahara ya Suma JKT na ulipaji wa fidia wananchi waliochukulia maeneo yao.

Wabunge hao walitoa maoni yao wakati wa mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka huu wa fedha, na hotuba kuwasilisha bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Jennista Mhagama.

Mbunge wa Mtambile (Cuf), Masood Abdallah Salim, alisema kuwapo kwa magari hayo ni kuruhusu kutumika kutisha wananchi kwenye uchaguzi huku akihoji kama ni uchaguzi wa kiraia kwa nini magari ya jeshi yapite.

“Hakuna vita magari yasipitishwe mtaani, waacheni wananchi wachague, msiruhusu kuacha magari ya jeshi kutembea siku tano au wiki moja kabla ya uchaguzi,” alisisitiza.

Kuhusu janga la corona, mbunge huyo alitaka wizara hiyo kutoa taarifa za wapendwa wao ambao wako nchi mbalimbali kwa ajili ya kulinda amani.

“Tunajua corona imesambaa duniani na tuna askari wetu wako maeneo mbalimbali kulinda amani, ni vyema tukajua hali zao kwa sasa zikoje,” alisema.

Pia, alitaka wizara kutoa fedha za kulipa fidia wananchi kwenye maeneo yaliyochukuliwa na jeshi, kwa kuwa kumekuwa na ucheleweshaji kiasi cha wengine kufariki.

Alisema Suma JKT kwenye kitengo cha ujenzi na kwamba ni vyema ubora wa kazi zao wamejenga nyumba ngapi na ubora wake, ijulikane ni fedha kiasi gani imepatikana.

Kadhalika, alisema Suma JKT ambao wanalinda ni vyema idadi ikajulikana, huku kukiwa na malalamiko ya mishahara yao ambayo ni Sh. 190,000 kwa mwezi ambayo ni ndogo kwao.

“Ninaomba waongezewe kiasi hiki ni kidogo sana, wanalalamika wanapokuwa kwenye sehemu za ulinzi,” alisema.

Naye, Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Mariam Msabaha, aliiomba serikali kuwaangalia na kuwawezesha vizuri wanajeshi katika kipindi cha uchaguzi mkuu kwa kuwa wanalinda mipaka na huenda kukawa na wachokozi.

Aliiomba serikali kuwakopesha fedha ili wajenge nyumba uraiani kwa kuwa siyo vizuri wanapostaafu kwenda kuhangaika na maisha.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live