Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunge watahadharisha asilimia 10 fedha za vikundi

873b38c7107dadb689ee88a91fd8cf30 Kamati yaonya ubadhirifu

Sat, 16 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Serikali za Mitaa imetahadharisha matumizi ya fedha za asilimia 10 inayotokana na mapato ya ndani ya halmashauri ikisema yasipowekewa utaratibu mzuri wa ufuatiliaji na usimamizi, hayatatoa tija iliyokusudiwa.

Akiwasilisha maoni ya kamati hiyo, Makamu Mwenyekiti wake, Denis Londo alisema kwa sasa taarifa za matumizi ya fedha hizo zinatofautiana kiasi cha kuleta mashaka kuhusu uaminifu katika matumizi yake. Alisema kukosekana kwa mfumo wa teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) katika usimamizi wa fedha hizo za asilimia 10, inaweza kuwa chanzo cha ubadhirifu wake.

Alizitaka halmashauri kuhakikisha zinasimamia vyema mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu na kwamba zoezi zima linahitaji kuboreshwa zaidi. Katika hatua nyingine, Londo alisema kwa mwaka wa fedha 2021/2022, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) iliidhinishiwa kukusanya Sh 916,445,409,198.50.

Hata hivyo, hadi kufikia Februari 2022, Sh 615,603,870,037.65 ndizo zilikuwa zimekusanywa sawa na asilimia 67.17 ya lengo. Kwa upande wa ukusanyaji wa maduhuli kwenye mikoa, alisema taarifa zilionesha kuwa, hadi kufikia mwezi Februari 2022, mikoa yote kwa pamoja ilifika lengo la makusanyo kwa asilimia 75 huku Mkoa wa Mbeya ukiongoza kwa asilimia 98.04 ya lengo.

Aidha, Londo alisema Kamati ilitembelea miradi 10 ikiwamo miradi iliyotekelezwa kwa kutumia fedha zilizotolewa na serikali katika mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Covid-19.

Alisema ufuatiliaji wa kamati umeonesha kuwa zipo dalili kwamba, baadhi ya halmashauri hazikutekeleza miradi iliyopangwa kwenye bajeti zao za ndani, badala yake zimetumia fedha za Covid kuendeleza miradi hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live