Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunge wastaafu wamlilia Magufuli

3ceb5aabb499c8cd65fb5a800e4ee6b4.jpeg Wabunge wastaafu wamlilia Magufuli

Tue, 23 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WABUNGE wastaafu waliowahi kufanya kazi na Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli wamesema taifa limepoteza shujaa aliyefanya kazi kwa kuweka mbele uzalendo wa kulipenda taifa lake kwa moyo wa dhati.

Wakizungumza mjini hapa jana, Mbunge wa zamani wa Kikwajuni, Parmukhi Hoogan Sigh alisema uwezo na ubunifu wa Magufuli ulianza kujionesha pale alipokuwa Waziri wa Ujenzi ambapo bungeni alionesha uwezo mkubwa katika kujibu maswali, hoja na kufafanua mambo yanayohusu wizara yake.

Alisema nyota ya Magufuli ilizidi kung’ara pale alipochaguliwa kuwa Rais ambapo alikuja na kauli mbiu ‘Hapa kazi tu’ huku akitekeleza na kusimamia miradi mikubwa ya miundombinu kwa ajili ya kuijenga Tanzania.

Hoogan alisema mikakati hiyo iliiwezesha Tanzania kuingia katika uchumi wa kati kutokana na juhudi zake za kupambana na ubadhirifu, kuziba mianya ya rushwa na vita dhidi ya ufisadi.

“Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepoteza kiongozi shujaa, hodari, mzalendo aliyewapenda wananchi wake wa rika tofauti wazkiwemo wamachinga na alitilia mkazo watu wafanye kazi,” alisema.

Mbunge wa zamani wa Jang’ombe, Mohamed Rajab Soud alisema anakumbuka uwezo wa Magufuli ambaye wakati alipokuwa Mbunge alikuwa akihudumu katika Kamati ya Bunge ya Ujenzi na Miundombinu.

“Aliweza kujibu kwa ufasaha hoja mbalimbali za wabunge waliochangia bajeti yake huku akionekana wazi kukidhi kiu ya wabunge.”

“Tunamkumbuka sana Magufuli ambaye alikuwa Mbunge mwenzetu, tunakumbuka uwezo wake wa kujibu hoja ambazo ndiyo zilizomwezesha kuwa Rais,'' alisema.

Aliyekuwa Mbunge wa Chwaka kwa muda wa miaka 20, Yahya Kassim Issa aliwataka Watanzania kuendelea kumkumbuka kiongozi wao huyo kwa mambo makubwa aliyoyafanya katika kipindi cha uhai wake na kuwa mfano wa kuigwa katika kuleta maendeleo.

Alisema aliingia bungeni pamoja na Magufuli ambaye alionesha uwezo mkubwa na haraka alichaguliwa kuwa Naibu Waziri na baadaye kupanda ngazi hatua kwa hatua hadi kufikia kuwa Rais.

“Njia pekee ya kumuenzi kiongozi wetu huyu ni kuiga kauli yake ya ‘Hapa Kazi Tu’ ambayo inajenga ari kwa Watanzania kupenda kufanya kazi kwa maslahi ya taifa na watu wake,” alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz