Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunge wamshukia DC Chemba, wadai amegeuka trafiki

51816 Dc+pic

Thu, 11 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Mbunge wa Chemba (CCM), Juma Nkamia na Maftah Nachuma wa Mtwara Mjini (CUF) leo wamemshukia mkuu wa wilaya ya Chemba mkoani Dodoma, Simon Odunga kwa madai kuwa utendaji wake wa kazi si mzuri.

Wakati Nkamia akisema mkuu huyo wa wilaya husimamisha magari barabarani saa sita mchana kama askari wa usalama barabarani, Nachuma amesema amekuwa akiwafukuza wenyeviti wa CUF wilayani humo.

Wametoa kauli hiyo leo katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora).

“Nikuombe mheshimiwa waziri unda tume kuchunguza matatizo ya wilaya ya Chemba. Nashukuru Mkuchuka (George Mkuchika-Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora)  upo hapa wewe ni mtu mzima tunaomba mtusaidie.”

“Matatizo ya Chemba yanaweza kutuletea matatizo mengine makubwa. Haiwezekani mkuu wa wilaya anasimama saa sita mchana barabarani anasimamisha magari kama trafiki,” amesema.

Amesema mbali na mkuu huyo wa wilaya, mkurugenzi wa halmashauri hiyo amejenga nyumba kwa miezi miwili na anataka kuchimba kisima cha kuuza maji wakati tayari kuna kisima.

“Tukiwambieni nyinyi hamtaki kuchukua hatua mnasubiri mpaka Rais (John Magufuli) aje? Undeni tume mchunguze mjue nani mwongo. Unapiga chapa ng’ombe milioni 290 lakini hakuna fedha, mbunge akisema wanasema ana majungu,” amesema Nkamia.

Kwa upande wake, Nachuma amesema, “Huyu mkuu wa wilaya ya Chemba badala ya kusimamia miongozo ya Serikali yeye kazi yake ni kuwafukuza wenyeviti wa kata wa CUF.”

“Ameshawafukuza tisa hadi sasa naomba kujua utawala bora tunaozungumza ni upi, demokrasia tunayoisema ni ipi?”

Amesema wakuu wa wilaya wameteuliwa kusimamia maendeleo ya wananchi lakini wanafanya kazi ya kuwafukuza wapinzani.



Chanzo: mwananchi.co.tz