Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunge wakoshwa na kasi ya Magufuli

4fee4e920cedc5dc931a4ff4efeae04c Wabunge wakoshwa na kasi ya Magufuli

Fri, 5 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

JITIHADA za Rais, John Magufuli kuboresha huduma za jamii, zimewavutia wabunge na kueleza kuwa kiongozi huyo ameandika historia katika nia yake ya kuboresha maisha ya Watanzania.

Wabunge hao walieleza bungeni jana pia nia yao kutaka kuona tatizo la ajira linakuwa historia.

Pia walisisitiza umuhimu wa serikali kupitia upya mfumo wa elimu nchini kwa kuzingatia elimu inayomuandaa mtu kujiajiri na si kuajiriwa.

Walisema hayo wakati wakichangia hoja ya hotuba ya Rais Magufuli, aliyoitoa bungeni Novemba 13 mwaka jana wakati akizindua Bunge la 12.

Walitaja maeneo yanayohitaji kuboreshwa katika miaka mitano ijayo kuwa ni elimu, miundombinu, maji, afya na ajira.

Mbunge wa Viti Maalumu, Dk Rita Kabati (CCM), aliipongeza serikali kwa jitihada iliyozionesha katika eneo la sekta ya afya kwa kipindi cha miaka mitano ikiwa ni pamoja na kujenga zahanati 1,998, vituo vya afya 487 na hospitali za wilaya 99.

"Maboresho haya yameanza kuleta mafanikio ambapo vifo vinavyotokana na uzazi kwa sasa vimepungua ambapo mwaka 2015 vifo vilikuwa 11,000 lakini mwaka jana vimefikia hadi 3, 000," alisema Kabati.

Mbunge wa Ukonga, Jerry Slaa (CCM), alisema Rais Magufuli kwa miaka mitano amefanya kazi kubwa ikiwemo kuboresha huduma za jamii, pato la taifa kukua, mfumuko wa bei kutopanda lakini pia hata shilingi ya Tanzania haijashuka thamani.

"Katika huduma za jamii kazi kubwa imefanyika vituo vya afya, zahanati na hospitali zimejengwa na tumeona. Ila naomba niweke wazi sasa tuna kazi kubwa kumsaidia Rais ili aweze kutimiza malengo yake aliyojiwekea," alisema Slaa.

Mbunge wa Viti Maalumu, Latifa Juakali (CCM) alisema Rais Magufuli amefanya kazi kubwa nchi nzima ikiwemo afya, miradi ya maji na miundombinu

"Asiye na macho haambiwi tazama,"alisema na kuongeza kuwa pamoja na kazi kubwa iliyofanywa na serikali katika eneo hilo, bado mfumo wa elimu unaotolewa nchini haumuandai kijana kuajirika au kajiajiri.

"Naishauri Wizara ya Elimu kuiandaa mitaala inayoendana na wakati, kwa mfano kwa sasa nchi yetu iko katika uchumi wa kati, je tumewaandaaje vijana wetu kuendana na kasi ya uchumi wa kati? alihoji.

Mbunge wa Nanyamba, Abdallah Chikota (CCM), alisema kwa upande wa Mtwara zao kuu ni korosho, hivyo aliiomba serikali kuhakikisha wakulima wa zao hilo wanapatiwa pembejeo za kutosha ili wazalishe kwa wingi.

Mbunge wa Mbogwe, Nicodemus Maganga (CCM) alizungumzia tatizo la rushwa ambalo ameeleza kuwa kwa sasa linazidi kukua kuliko miaka ya nyuma.

"Nchi yetu kila mmoja anatamani tuwe na mabilionea wengi lakini hatuwezi kuwa mabilionea, kwa sababu rushwa kwa sasa imepanda bei, mwaka 2000 nilikuwa dereva, rushwa ilikuwa ni 2000 sasa imepanda na kufikia 10,000," alieleza

Alisema wasomi wengi nchini ndio wanaoisababishia nchi hasara hususani katika halmashauri hivyo ameiomba serikali iwachukulie hatua watendaji wanaojihusisha na rushwa.

Chanzo: habarileo.co.tz