Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunge waitwa Dodoma haraka

Bunge Pic Data Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania

Tue, 8 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba atawasilisha mapendekezo ya Serikali ya mpango na kiwango cha ukomo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2022/2023 kwa wabunge Ijumaa Machi 11, 2022 jijini Dodoma.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo Mawasiliano na Uhusiano wa Kimataifa cha Bunge leo Jumanne Machi 8,2022, wabunge wote wanatakiwa kufika jijini Dodoma Alhamisi Machi 10,2022.

Wabunge hao wanatakiwa kufika jijini Dodoma kwa ajili ya shughuli za kamati za kudumu za Bunge kabla ya kuanza kwa mkutano wa Bunge la bajeti Aprili 5, 2022.

“Watakapofika Dodoma watashiriki mkutano wa wabunge wote utakaofanyika siku ya Ijumaa tarehe 11 Machi, 2022,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Imesema katika mkutano huo, Waziri wa Fedha na Mipango atawasilisha kwa wabunge mapendekezo ya Serikali ya mpango na kiwango cha ukomo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Taarifa hiyo imesema hilo linafanyika kwa mujibu wa kanuni ya 116(1) ya kanuni za kudumu za Bunge toleo la Juni 2020.

Imesema baada ya mkutano huo kamati zitaendelea na shughuli zilizopangwa kwa mujibu wa kanuni iliwemo kamati ya Bajeti itachambua mapendekezo hayo ya Serikali kwa mujibu wa kanuni.

Pia amesema kamati tisa za kisektra kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyotengewa bajeti mwaka 2021/2022.

Aidha, imesema Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo itapokea taarifa ya utekelezaji wa maazimio kuhusu sheria ndogo zilizowasilishwa wakati wa mkutano wa tatu na wa nne wa Bunge pamoja na kuchambua sheria ndogo zilizowasilishwa wakati wa mkutano wa sita wa Bunge.

Taarifa hiyo imesema Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) itafanya ziara ya ufuatiliaji wa ufanisi na tija ya uwekezaji wa mitaji ya umma kwenye miradi mbalimbali ya kiuwekezaji.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live