Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunge wafuturishwa Dodoma "tunarudisha shukrani kwao" (+picha)

WhatsApp Image 2021 05 05 At 22.09.01 1 660x400.jpeg Wabunge wafuturishwa Dodoma "tunarudisha shukrani kwao" (+picha)

Thu, 6 May 2021 Chanzo: millardayo.com

Leo May 5, 2021 Siku chache zikiwa zimesalia kabla ya kumalizika kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, Benki ya CRDB imetoa futari kwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumzia katika hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Bunge na kuhudhuriwa na wateja wa Benki hiyo, Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson ameipongeza na kuishukuru Benki ya CRDB kwa kuandaa futari hiyo kwa wateja sambamba na kutenga zaidi ya Shilingi Milioni 100 kusaidia mahitaji ya futari kwa vituo vya watoto wanaoishi katika mazingira.

“Kwa mlichokifanya leo kwa waheshimiwa wabunge pamoja na wadau wenu wengine wa hapa Dodoma inadhihirisha ni kwa jinsi gani ambavyo Benki ya CRDB ipo karibu na jamii na hususan wadau wake lakini zaidi mlichofanya kwa wenye watoto wenye uhitaji ni kikubwa sana chenye kustahili pongezi na kuigwa na wengine ” alisema Mh. Tulia.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela amesisitiza kuwa benki hiyo inawachukulia wateja wake wote kama sehemu ya familia yake, hivyo Mwezi huu Mtakatifu unatoa fursa ya kushirikiana kuboresha mahusiano kwa kushiriki pamoja katika ibada ya funga na futari.

“Tunaendelea kutumia kipindi hiki pia kuonyesha shukrani zetu kwao kwa kuendelea kuichagua benki yetu; wakati huo huo tunaendelea kutekeleza wajibu wetu kwa jamii kwa kugusa makundi yenye mahitaji  maalum,” alisisitiza Nsekela.

Nsekelea alisema mbali na kufuturisha wateja, Benki ya CRDB pia imekuwa ikitoa msaada wa futari kwa vituo vya kulelea watoto vyenye uhitaji mkubwa. Mwaka huu Benki ya CRDB imetenga kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya kusaidia futari kwa vituo vya kulelea watoto 40 katika kanda zote nchini huku ikitarajia kufuturisha wadau wake wa Zanzibar mwishoni mwa wiki hii.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay amewashukuru wateja wa Benki wakiwemo wabunge kwa kushiriki katika futari hiyo na kuendelea kuiunga mkono Benki na kuiwezesha kuendelea kufanya vizuri sokoni.

Futari hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Spika wa Bunge, Mheshimiwa Job Ndugai pamoja na mawaziri mbalimbali wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania sambamba na Sheikh Mustafa Shaaban, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambae aliiongoza dua ya kuiombea Benki ya CRDB kwa kufuturisha katika kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani.



























Chanzo: millardayo.com