Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunge wachefukwa na watumishi wa sekta ya Ardhi

Makoa Ally Makoa akichangia hoja bungeni

Thu, 10 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wabunge wameshauri bodi na mabaraza yanayoshughulika na usajili na nidhamu za watumishi wa Sekta ya ardhi yajielekeze zaidi katika kudhibiti maadili ya watumishi wa halmashauri ya Jiji la Dodoma ili kurejesha imani kwa wananchi.

Hayo yamebainishwa katika taarifa ya shughuli za Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii katika kipindi cha kati ya Januari mwaka 2021 hadi Februari mwaka 2022 iliyosomwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Ally Makoa bungeni.

Amesema kumekuwa na changamoto za upangaji, upimaji na umilikishaji ardhi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Amezitaja changamoto hizo kuwa ni malalamiko ya ukosefu wa maadili toka kwa watumishi wa halmshauri, kuwepo kwa makampuni ya kupima yenye utapeli, ukosefu wa elimu kwa wanachi na mgongano wa kimaslahi.

Makoa amesema changamoto hizo zimekuwa zikikwamisha na kupunguza kasi ya upimaji wa ardhi ambapo unaikosesha serikali mapato yatokanayo na gharama za upimaji na kuwanyima wananchi wa makundi tofauti haki ya kumiliki ardhi kisheria.

Amesema kutokana na changamoto hizo Bunge linaishauri Serikali kutekeleza mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na bodi na mabaraza yanayoshughulika na usajili na nidhamu za watumishi wa Sekta ya ardhi ijielekeze zaidi katika kudhibiti maadili ili kurejesha imani kwa wananchi na taasisi zinazohudumiwa na wataalamu hao.

“Kuweka mkakati wa kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi kabla na kipindi cha zoezi la upimaji na umilikishaji ili kuondokana na migogoro isiyo ya lazima,”amesema.

Pia ameishauri kampuni ambazo zilipewa kazi ya kurasimisha makazi katika Jiji la Dodoma na hazijakamilisha kazi hiyo kwa zaidi ya mwaka mmoja zitimize wajibu wao wa kisheria.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live