Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunge wacharuka, wadai kanuni za Mawaziri haziendani na sheria

Bunge La Tanzania Wabunge wacharuka, wadai kanuni za Mawaziri haziendani na sheria

Wed, 2 Nov 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wabunge watatu wamezilalamikia kanuni zinazotungwa na mawaziri baada ya wao kupitisha sheria kuwa haziendani ya sheria wanazozitunga na hivyo kuibua malalamiko kutoka kwa wananchi kama ilivyotokea kwenye tozo za miamala ya kieletroniki.

Wabunge hao ni Miraji Mtaturu (Singida Mashariki-CCM), Innocent Bilakatwe (Kerwa-CCM) na Stella Fiyao (Viti Maalum) ambao walisema wakati wakichangia Muswada wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi wa mwaka 2022.

Mtaturu amesema sheria hiyo ni nzuri lakini utungaji wa kanuni hizo uendane na sheria iliyopitishwa ili kuepuka malalamiko kutoka kwa wananchi.

“Pamoja na sheria hii kuwa nzuri na tumekuwa tukipitisha hapa, kumekuwa na changamoto ya kanuni, niombe sana kwenye eneo hili na sisi tunamuamini Waziri, sheria ikitungwa nzuri iende hivyo hivyo na kanuni ziwe nzuri,”amesema.

Mtaturu amesema eneo la utungaji wa kanuni linaweza kuwa mwiba mwingine katika utekelezaji wa sheria zinazopitishwa na bunge.

“Tumekuwa tukipitisha baadhi ya sheria lakini ile nafasi ya kutengeneza kanuni huwa inakwenda kuharibu kabisa sheria, matokeo yake wabunge tunaulizwa mlipitishaji sheria hii, kumbe kanuni imekwenda kuharibu kabisa maudhui mazima ya sheria ambayo tumepitisha hapa,”amesema.

Kwa upande wake, Stella amesema mambo ya kanuni, wabunge wamekuwa hawahusiki na hivyo wanatunga sheria salama na rafiki kwa wananchi wao lakini mtu anakwenda kuumizwa na kanuni ambazo hazijapitiwa na wabunge.

“Kwa hiyo hapa tunakwenda kutengeneza tatizo, ili twende sawa sheria hizi zikawe salama na rafiki kwa wananchi wetu ni vyema kwenye utungaji wa kanuni tukaangalia maslahi mapana ya wananchi,” amesema.

Naye Bilakatwe amesema kuwa wanatunga sheria vizuri lakini kanuni zinakuwa za ajabu na hivyo wabunge kuonekana wametunga sheria za ajabu.

“Ndio hata mambo yaliyoonekana kwenye tozo, tunaonekana watu wa ajabu. Inaonekana wabunge hakuna kitu chochote tulichokifanya. Nishauri Bunge ndio tunaletewa miswada kutunga sheria. Sasa tuwe na nguvu ya kuleta kanuni ambazo Serikali inakwenda kuzitunga ili tujue kile sisi tumekipika kinapakuliwa vipi,”amesema.

Amesema lazima Bunge lisimame kuhakikisha kanuni zinazotungwa na Serikali zinakuwa nzuri kama sheria wanazozitunga.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live