Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunge wachangiwa Sh800milioni Dar

14963 Wabunge+pic TanzaniaWeb

Sat, 1 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wabunge wanawake wamechangiwa Sh800milioni katika hafla ya kuchangia ujenzi wa vyoo vya mfano kwa watoto wa kike iliyoandaliwa na umoja wa wabunge wanawake nchini.

Kiasi hicho cha fedha kilitangazwa jana usiku Agosti 31, 2018 baada ya kumalizika kwa hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi wa taasisi za Serikali, kampuni za biashara na wadau wa maendeleo.

Akizungumza na MCL Digital, mwenyekiti wa kamati maandalizi ya hafla hiyo, Profesa Anna Tibaijuka amewashukuru watu wa kada mbalimbali jijini Dar es Salaam kwa kuunga mkono kampeni hiyo, kwani pia itawasaidia watoto wa kiume.

Amesema hadi sasa fedha zilizopatikana ni Sh2.3bilioni na zinazohitajika ni Sh3.2bilioni.

Amesema katika uchangiaji huo wapo waliotoa fedha taslimu na wengine kujitolea vifaa vya ujenzi huku mbunge wa Chalinze (CCM), Ridhiwani Kikwete akijitolea  kujenga vyoo jimbo la Bagamoyo na Chalinze.

Mwenyekiti wa umoja huo, Magreth Sitta aliwaomba wananchi kuendelea kuchangia ili kuweza kujenga vyoo hivyo vya mfano katika majimbo 264 ya uchaguzi  nchini, kubainisha kuwa ujenzi wa choo kimoja gharama yake ni Sh11milioni.

Vitu mbalimbali pia viliuzwa katika hafla hiyo, zikiwemo picha za waasisi wa Taifa na za kupamba majumbani huku kiingilio kikiwa Sh100,000.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama; Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako; Spika wa Bunge, Job Ndugai; Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai na Spika mstaafu Anne Makinda ambaye alikuwa mgeni rasmi, akimuwakilisha Rais John Magufuli.

 

 

 

 

Chanzo: mwananchi.co.tz