Shinyanga. Wabunge wa CCM Mkoa wa Shinyanga wanaopita kwenye kata na kuandaa safu za wagombea wao wa udiwani wameonywa kuacha mara moja tabia hiyo vinginevyo watachukuliwa hatua kali za kinidhamu huku madiwani wakitakiwa kutoa taarifa na kuacha kuwafumbia macho. Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne Machi 3, 2020 na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa(NEC), Gasper Kileo mbele ya makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ally Idd kwenye mkutano wa ndani wa chama hicho na kubainisha kuwa taarifa zao zote wanazo. Kileo amesema kuna baadhi ya wabunge hawakujitokeza kushiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa lakini wamejipanga na fedha zao kwenye Uchaguzi MkuU. “Wabunge wengine tunawaita kwenye vikao hapa matokeo yake wanakwenda makao makuu kutuletea maelekezo, napenda niwaambie huko mnakwenda kujichora, kwani yote yanayoendelea kwenye majimbo yenu na kata tunayajua na tunayo mezani,”amesema Kileo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack amewataka wana CCM kuacha makundi na kuwa kitu kimoja ili kuweza kupata ushindi wa asilimia 100 kwenye Uchaguzi Mkuu, huku akibainisha wapo baadhi yao wamefunga mafundo ukiwaona wamependeza lakini ukifungua pazia utawakuta wamegawanyika. Balozi Idd ambaye ni mlezi wa CCM Mkoa wa Shinyanga aliwaonya wabunge wanaowapelekea fitina wenzao ili wasichaguliwe wabunge wa viti maalumu kwani kila mtu anatekeleza majukumu yake na kufafanua kuwa wabunge wa viti maalum ni wabunge wa mkoa mzima hawazuiliwi kwenda kutoa msaada sehemu yoyote kwenye mkoa.