Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunge kuongoza kampeni za CCM Mara

Sun, 15 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wajumbe waelezwa kuwa CCM inahitaji kusuluhisha mvutano na uhasama kati ya viongozi wa Serikali na chama Tarime

Musoma. Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara kimeunda timu maalumu ya kampeni itakayoongozwa na wabunge wa majimbo na viti maalumu ili kutafuta ushindi kwenye uchaguzi mdogo wa udiwani wa kata za Ikoma na Manchira wilayani Serengeti na Turwa, Tarime.

Mbunge wa Bunda, Boniface Getere ataongoza kampeni za Kata ya Turwa wakati Vedastus Mathayo wa Musoma Mjini atakuwa kata za Ikoma na Manchira.

Akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mara, mwenyekiti wa chama hicho mkoani humo, Samuel Keboye alisema timu hiyo itaongezewa nguvu na wabunge wa viti maalumu, madiwani, viongozi wa chama pamoja na wakuu wa wilaya zote za mkoa.

“Wakuu wa wilaya ni makada wa CCM; lazima watambue uchaguzi huu ni kipimo chao cha utendaji,” alisema Keboye.

Walioteuliwa kuwania udiwani kwa tiketi ya chama hicho ni Michael Kunani, Kata ya Ikoma, Charles Muyuga (Manchira) na Chacha Mwita (Turwa).

Kwa upande wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), mgombea wa Kata ya Ikoma ni Kennedy Hamisi na Kimani Makuru anawania udiwani Manchira.

Hata hivyo, Keboye aliwaambia wajumbe kuwa CCM inahitaji kusuluhisha mvutano na uhasama kati ya viongozi wa Serikali na chama wilayani Tarime ili kujihakikishia ushindi katika kata hizo.

“Ndugu mkuu wa mkoa, Tarime kuna shida inayohitaji kutatuliwa kwa sababu kuna mgawanyiko unaohatarisha ushindi wa chama. Viongozi wa Serikali na chama hawapikiki chungu kimoja,” alisema Keboye huku akimuangalia mkuu huyo wa mkoa wa Mara, Adam Malima ambaye ni mjumbe wa kikao hicho.

Keboye alisema: “Mimi na wewe (Malima) tukiwa viongozi wakuu wa chama na Serikali, lazima tuingilie kati.”

Akizungumzia uhasama kati ya viongozi wa Serikali, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) wilayani Tarime, Godfrey Francis alisema unatokana na ubabe wa viongozi wa Serikali wanaokichonganisha chama na wananchi.

Akizungumzia mtafaruku wa kiuongozi Tarime, Malima aliagiza kila mmoja kwa nafasi yake kutambua kuwa masilahi ya kwanza ni ya chama na Serikali kwa kuhakikisha CCM inashinda kata zote tatu mkoani humo.

Uchaguzi huo mdogo unafanyika Agosti 12 baada ya madiwani wake wa Chadema kutimkia CCM.

Chanzo: mwananchi.co.tz