Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunge kujadili vipaumbele 6 kujenga uchumi

B9e210938abe7cb57cd68f016a792b51.jpeg Wabunge kujadili vipaumbele 6 kujenga uchumi

Thu, 8 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba leo anatarajiwa kuwasilisha bungeni Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano wa mwaka 2021/2022 hadi 2025/2026.

Mkutano wa Tatu wa Bunge la 12 ambalo ni maalumu kwa Bajeti ya Serikali, utakaokamilisha shughuli zake Juni 30, mwaka huu kupisha mwaka wa fedha unaoanza Julai Mosi, mwaka huu.

Wakati akiwasilisha mpango huo kwa wabunge wote hivi karibuni, aliyekuwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alitaja vipaumbele sita vya mpango huo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ambao umelenga kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu.

Alisema uandaaji wa mapendekezo ya serikali ya mpango umezingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Ilani ya CCM kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, hotuba za Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli wakati akizindua Bunge la 12, sera na mikakati mbalimbali ya kisekta, kikanda na kimataifa.

Vipaumbele vitakavyozingatiwa katika mpango huo ni Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (JNHPP), kuboresha Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL); ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa; makaa ya mawe ya Mchuchuma na Chuma – Liganga ikijumuisha ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa kutoka Mtwara hadi Mbambabay na matawi ya Mchuchuma na Liganga.

Pia ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima hadi Tanga, Mradi wa Kuchakata Gesi Asilia kuwa Kimiminika (LNG), miradi ya umeme wa maji ya Ruhudji na Rumakali, uchimbaji wa madini ya nickel na ujenzi wa madaraja makubwa na barabara za juu za Daraja la Kigongo – Busisi, Tanzanite na Interchange ya Kamata, Dar es Salaam.

Dk Mpango alisema pia ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Mbegani, ununuzi wa meli za uvuvi, Kiwanda cha Sukari Mkulazi, utafutaji wa mafuta, Mradi wa Magadi Soda – Engaruka; kuongeza rasilimali watu yenye ujuzi adimu na maalumu kwa maendeleo ya viwanda na ustawi wa jamii; kanda maalumu za kiuchumi.

Kipaumbele cha pili ni kuchochea uchumi shindani na shirikishi kwa ukarabati wa njia kuu ya reli ya kati; ununuzi wa injini na mabehewa; ujenzi wa barabara za kufungua fursa za kiuchumi na kuunganisha nchi jirani.

Pia kuondoa msongamano mijini na kuboresha barabara za vijijini; ujenzi wa madaraja makubwa ikiwemo madaraja ya New Wami (Pwani), Kitengule (Kagera), Kirumi (Mara) na Mkenda (Ruvuma); ujenzi na ukarabati wa meli kwenye maziwa makuu ikijumuisha MV Mwanza Hapa Kazi Tu, MV Liemba na MV Umoja.

Alisema pia uboreshaji wa bandari za Dar es Salaam, Tanga, Mtwara na bandari za maziwa makuu; miradi ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme mijini na vijijini; mapinduzi ya TEHAMA ikijumuisha mradi wa mkongo wa taifa wa mawasiliano na kutekeleza mradi wa Tanzania ya Kidigitali.

Kipaumbele ya tatu ni kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma ambapo lengo ni kuendeleza viwanda vinavyolenga kuongeza uzalishaji na thamani ya mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na madini pamoja na kuzalisha bidhaa zitakazotumia malighafi na rasilimali zinazopatikana nchini.

Kipaumbele ya nne ni kukuza biashara na uwekezaji, eneo ambalo litajumuisha miradi ya kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji ikiwemo kuendelea kutekeleza Mpango wa Kuboresha Biashara na Uwekezaji.

Kipaumbele cha tano ni kuchochea maendeleo ya watu. Miradi itakayotekelezwa inajumuisha kuimarisha miundombinu ya Hospitali ya Taifa Muhimbili; uboreshaji wa hosptitali za rufaa za kanda na za mikoa, halmashauri, vituo vya afya na zanahati; ununuzi na usambazaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi; kuimarisha huduma za tiba asili na tiba mbadala; kuendelea na udhibiti wa magonjwa yasiyoambukizwa

Pia kuendelea na utoaji wa elimu msingi bila ada; kuendelea na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu; kuendelea na uboreshaji wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika ngazi zote za elimu; kuendelea na kupanga, kipima na kumilikisha ardhi mijini na vijijini; kusimamia na kuendeleza rasilimali za maji; na kuendelea na utekelezaji wa programu za kulinda mazingira na kuhimili mabadiliko ya tabianchi.

Alitaja kipaumbele cha sita ni kuendeleza rasilimali watu eneo linalojumuisha programu na mikakati inayolenga kuendeleza maarifa na ujuzi wa rasimali watu nchini.

Katika mkutano huo wa Bunge, serikali inatarajiwa kuwasilisha na kujadili bajeti kuu yake kwa mwaka wa fedha 2021/2022 inayotarajia kutumia Sh trilioni 36.26 ikiwa na vipaumbele vya ukuaji uchumi, utawala bora na maendeleo.

Bajeti ya mwaka huu ni ongezeko la asilimia nne kutoka mwaka jana ya Sh trilioni 34.88. Ongezeko hilo la asilimia nne linatokana na mahitaji ya Mfuko Mkuu wa Serikali ikijumuisha malipo ya deni la serikali.

Kwa mujibu wa mwongozo wa bajeti uliotolewa na serikali Februari mwaka huu na kusomwa bungeni na aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria ambaye sasa ni Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu, ongezeko hilo limetokana na mahitaji ya upandishwaji wa madaraja ya watumishi na ajira mpya.

Chanzo: www.habarileo.co.tz