Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunge kujadili biashara, ugaidi Afrika

2de020d71738a505b9e14aade72432ff Wabunge kujadili biashara, ugaidi Afrika

Mon, 6 Sep 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKUTANO wa nne wa Bunge unaendelea jijini Dodoma na kwa mujibu wa ratiba, leo utajadiliwa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wa mwaka 2021. Kesho wabunge wanatarajiwa kujadili Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali Namba tano wa mwaka 2021.

Keshokutwa ni Azimio la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Viwango vya Afya ya Mimea, Wanyama na Usalama wa Chakula na Alhamisi kutakuwa na Azimio la Kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).

Ijumaa, kabla ya kutolewa hoja ya kuahirisha, wabunge watapitisha azimio la kuridhia Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi wa Mwaka 2021.

Kikao cha kwanza cha mkutano huo Agosti 31 kilianza na kuwasilishwa taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.

Kamati hiyo iliwatia hatiani na kupendekeza Mbunge wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima na Mbunge wa Ukonga, Jerry Silaa wasihudhurie mikutano miwili ya Bunge. Bunge lilikubali pendekezo hilo

Kwenye mkutano huu ambao umekuwa na tahadhari kubwa dhidi ya ugonjwa wa covid-19, pia kuliwasilishwa miswada ya Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali namba mbili na namba nne, ikajadiliwa na kupitishwa na wabunge.

Muswada mwingine uliowasilishwa na kupitishwa katika wiki ya kwanza ya mkutano ni wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Usajili wa Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu wa mwaka 2021.

Kuhusu tahadhari dhidi ya covid-19, Bunge limepunguza muda wa kuanza kwa vikao vyake; Sasa vinaanza saa 8:00 mchana hadi saa 1:00 usiku hatua inayolazimu kutumia saa tano badala ya saba na nusu kama ilivyokuwa katika utaratibu wa kawaida.

Spika wa Bunge, Job Ndugai alitangaza utaratibu huo katika kikao cha kwanza na kwamba kuzingatia hilo kipindi cha maswali na majibu ni dakika 60 badala ya 90. Ili kupunguza msongamano bungeni, sasa zinatumika kumbi mbili, Pius Msekwa na ukumbi mkubwa.

Wabunge wamesisitiza kuvaa barakoa kipindi chote wanachokuwa katika kumbi isipokuwa wenye tatizo la kiafya ambao wataruhusiwa baada ya kupata idhini ya Spika.

Kwa msingi huo wa tahadhari ya covid-19, wageni wanaofika kutembelea Bunge wala mafunzo hawaruhusiwi isipokuwa wenye shida za kiofisi, maofisa wa serikali wanaofuatilia shughuli za Bunge na waandishi wa habari.

Chanzo: www.habarileo.co.tz